WAANDAAJI wa Tamasha
la Pasaka wamemualika Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi
kushuhudia tamasha la mwaka huu.
Mwenyekiti wa Kamati
ya Maandalizi ya Tamasha la Pasaka, Alex Msama alisema kwenye taarifa yake kwa
vyombo vya habari jana kuwa wamemualika Mzee Mwinyi kwa sababu ana historia
kubwa na tamasha hilo.“Mzee mwinyi alikuwa
mgeni rasmi kwenye tamasha letu la kwanza, hivyo tumemualika aje aone vijana
wake tunavyoendelea baada ya kutupa baraka wakati huo.
“Bado hatujapata
majibu, lakini naamini yatakuwa mazuri na atakuja kama mgeni wetu, maana
tumealika wageni wengi sana wakiwemo viongozi wastaafu, viongozi wa sasa na
makundi mbalimbali ya kijamii,” alisema Msama katika taarifa hiyo.
Mwaka huu
Tamasha la Pasaka linatimiza miaka 15 tangu kuasisiwa kwake na Kampuni ya Msama
Promotions ya Dar es Salaam na limekuwa likijiongezea umaarufu na kukubalika zaidi
kutokana na ubunifu wake wa kufanya maadhimisho ya Sikukuu za Pasaka na
Krismasi kwa umahiri na mguso wa kiroho kupitia matamasha hayo.
Umaarufu
wa matamasha hayo pamoja na mambo mengine, unatokana na ukweli kuwa yamekuwa
yakifanyika kwa ubunifu na umakini mkubwa huku kila mwaka yakiongezeka na
kubadili waimbaji mbalimbali wa nyimbo za Injili wa ndani na nje ya nchi.
Baadhi ya
nyota waliowahi kutumbuiza katika matamasha hayo ni marehemu Angela Chibalonza
kutoka Kenya, nguli wa kutoka Afrika Kusini, Solly Mahlangu ‘Obrigado’, Sipho
Makhabane na Rebeka Malope.
Wengine
ni Ephraim Sekeleti kutoka Zambia, Ambassadors of Christ (Rwanda), Faraja
Ntaboba na Solomoni Mukubwa (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo), 24 Elders
(Uganda) na Anastazia Mukabwa (Kenya).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...