Na Hassan Hamad (OMKR) 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amewasisitiza waislamu nchini kuachana na tabia ya kugombania misikiti, kwani haisaidii kuendeleza dini hiyo. 
Amesema misikiti ni nyumba za Mwenyezi Mungu, hivyo hakuna sababu kwa waislamu kulumbana kwa sababu za kugombea uongozi au kutokana na tofauti ya kimadhehebu. 
Maalim Seif ametoa nasaha hizo wakati akifungua msikiti wa Ijumaa MASJIDIL AQSAA katika kijiji cha Kiboje Mkwajuni, Wilaya ya Kati Unguja. 
Amesema Uislamu ni dini yenye nidhamu kamili, na kuwataka waumini wa dini hiyo kufuata nidhamu hizo katika kuendesha mambo yao bila ya kukaribisha malumbano na mifarakano baina yao. 
Amewahimiza waislamu wa eneo hilo kuuimarisha na kuuendeleza msikiti huo kwa kuendeleza harakati za darsa, sambamba na kuwaandalia watoto muda wa kutosha kuweza kuhudhuria katika darsa hizo ili kuwajenga kimaadili. 
Amesema madrasa zina mchango wa kipekee katika kuwaandaa watoto na kuwakuza kuwa raia wema walioleleka katika maadili ya Kiislamu, na kwamba waislamu bado wana jukumu la kuzianzisha madrasa kwa wingi na kuhakikisha kuwa watoto wanapita katika darsa hizo kupata malezi sahihi. 
Amefahamisha kuwa hivi sasa Zanzibar inahitaji malezi mazuri kwa watoto na vijana kuliko wakati mwengine wowote, kutokana na matishio makubwa yanayojitokeza na kuvurugika kwa maadili mema. 
 Amewakumbusha waislamu kuchangia harakati za dini hiyo kwa kujenga na kuimarisha misikiti na madrasa, kwani kila mmoja ana wajibu wa kutoa mchango wake katika kuziendeleza nyumba hizo za Mwenyezi Mungu. 
Aidha Maalim Seif amewakumbusha waislamu kuendeleza umoja, maelewano, na mshikamano miongoni mwao, na kujiepusha na chuki miongoni mwa waumini wa dini hiyo na dini nyengine. 
Amesema serikali imefanya juhudi kubwa kuiwezesha jamii kuondokana na hasama, chuki na kudharauliana na badala yake kujenga mazingira ya umoja, mshikamano na maelewano, mambo ambayo yanapaswa kuungwa mkono kwa vitendo. 
Katika hatua nyengine Maalim Seif ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwa waangalifu katika kuwachagulia vyuo vijana wao, ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza ikiwa ni pamoja na kuporomoka kwa maadili . 
Amesema baadhi ya vyuo hasa vilivyoko nje ya nchi havina misingi mizuri ya malezi, na kwamba bila ya kuwa waangalifu jamii inaweza kupoteza wengi ambao hatimaye wanaweza kujitumbukiza katika vitendo viovu. 
“Chagueni vyuo vitakavyo wanufaisha vijana, sio kijana kwa sababu anakwenda kusoma nje ya nchi umkubalie tu, wazazi na walezi ni lazima mufuatilie kujua uhakika wa vyuo hivyo” alisisitiza. 
Akizungumza kabla ya hotuba ya Ijumaa, Sheikh Thabit Noman Jombo kutoka ofisi ya Mufti wa Zanzibar amewahimiza waislamu wa eneo hilo kuutumia msikiti huo kama sehemu ya kutolea taaluma. 
Amesema Zanzibar ilikuwa kitovu cha elimu katika nchi za Afrika Mashariki, na hakuna budi kuienzi historia hiyo kwa vizazi vya sasa na vijavyo. 
Mapema akisoma risala ya wazee wa msikiti huo Sheikh Abdalla Rajab, amewashukuru waliojenga msikiti huo mkubwa katika kijiji chao, na kuahidi kuutunza na kuweka darsa ambazo zitakuwa endelevu. 
Amesema uwepo wa msikiti huo ni faraja kwa wanakijiji na maeneo jirani, kwani pia wameweza kuondokana na shida ya maji safi na salama iliyokuwa ikiwakabili kwa kipindi kirefu.
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akifungua pazia kuashiria ufunguza rasmi wa MASJID AQSAA katika kijiji cha Kiboja Mkwajuni, Wilaya ya Kati Unguja.
  Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akipena mikono na  Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi, baada ya ugunguzi wa MASJID AQSAA na sala ya Ijumaa katika kijiji cha Kiboja Mkwajuni.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, viongozi wa dini ya kiislamu nchini pamoja na waislamu mbali mbali wakisikiliza hotuba ya Ijumaa iliyotolewa na Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhil Soraha (hayupo pichani) katika msikiti mpya wa  MASJID AQSAA ulioko Kiboja Mkwajuni. Kushoto ni Kadhi Mkuu Sheikh Khamis Haji akifuatiwa na Mufti Mkuu Sheikh Saleh Omar Kabi
 Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi, akitoa nasaha baada ya uzinduzi wa MASJID AQSAA Kiboje Mkwajuni.
Baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu walioshiriki katika ufunguzi wa MASJID AQSAA, Kiboje Mkwajuni.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwahutubia waumini wa dini ya Kiislamu waliohudhuria  ufunguza wa MASJID AQSAA katika kijiji cha Kiboja Mkwajuni, Wilaya ya Kati Unguja. 
Picha na Salmin Said, OMKR

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...