Na Bashir Yakub.
Sheria ya ardhi ni pana na ina mambo mengi. Kila nikipata nafasi huwa najitahidi kueleza japo machache ili watu waweze kuelewa masuala mbalimbali kuhusu ardhi. Ardhi ni rasimali nyeti mno na hivyo ni tatizo kubwa kuishi bila kujua mambo ya msingi na ya kisheria kuhusu ardhi. Kutokujua ni moja ya sababu inayopelekea umaskini wakati utajiri upo mikononi mwako na upande mwingine husababisha migogoro ya ardhi inayoongezeka kila kukicha huku watu wakizidi kupata hasara.
Nimewahi kuandika kuhusu namna ya kisheria ya kujua iwapo ardhi unayonunua ina mgogoro au hapana, nikaandika kuhusu vitu gani viwe ndani ya mkataba wako wa manunuzi ya ardhi ili usitapeliwe na mikataba ya ardhi kwa ujumla, nikaandika kuhusu namna nyepesi ya kubadili/kupata hati/leseni ya makazi unaponunua ardhi na mengine mengi kuhusu ardhi. Leo naeleza kitu kingine muhimu katika sheria ya ardhi ambacho ni dhamana(mortgages) ambazo unaweza kutumia kupatia mkopo iwapo unahitaji mkopo.
1.NINI MAANA YA DHAMANA.
Kifungu cha pili cha Sheria Ya Ardhi kinasema kuwa dhamana ni hali ya mtu, taasisi au chombo chochote kuwa na maslahi katika ardhi inayomilikiwa na mtu mwingine au chombo kingine, maslahi ambayo yanatokana na deni au mkopo. Maana yake ni kuwa ardhi ni yako lakini kitendo cha mtu mwingine au taasisi nyingine kuwa na maslahi ndani yake na maslahi ambayo yanatokana na kuwapo kwa deni au mkopo basi hiyo ndiyo dhamana.
Ieleweke wazi kuwa dhamana haihusishi umiliki na wala haina uhusiano na umiliki. Dhamana ni dhamana na mmiliki anaendelea kuwa mmiliki. Dhamana haiondoi haki ya umiliki( right of occupancy).
2.VITU AMBAVYO WAWEZA KUWEKA DHAMANA NA KUPATA MKOPO.
Watu wengi wamekariri kwa kujua kuwa dhamana katika masuala ya ardhi ni lazima iwe hati ya nyumba, barua ya toleo( offer) au leseni ya makazi. Ni kweli vitu hivi hutumika kama dhamana lakini si hivi tu ambavyo vyaweza kutumika kama dhamana. Vipo vitu vingine ambavyo vyaweza kusimama kama dhamana na mtu akapata mkopo kama ambavyo tutaona hapa.
( A ) MKATABA WA PANGO.
Kisheria mkataba wa pango ni nyaraka halali ambayo mtu anaweza kuitumia kuombea mkopo katika taasisi ya fedha. Mkataba wa pango ni yale makubaliano ya kawaida kati mwenye nyumba na mpangaji. Mkataba wa pango ni nyaraka muhimu sana japo watu wengi huwa hawaipi uzito zaidi ya kuamini kuwa inalinda uhusiano kati ya mwenye nyumba na mpangaji. Ni vyema sasa kujua kuwa mkataba wa pango hauishii kulinda mahusiano ya mwenye nyumba na mpangaji tu isipokuwa ni nyaraka ambayo ikitumika vyema yaweza kuwa zana ya kukuza uchumi wako.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...