Ofisi ya waziri Mkuu kupitia Idara ya Uratibu wa Shughuli za maafa
imewasilisha Mkakati wa Mawasiliano wa kukabiliana na maafa kwa mkoa
wa Mtwara. Mkakati huo umetayarishwa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba
kunakuwa na Mtiririko unaoeleweka wa taarifa za tahadhari kabla ya
maafa, wakati wa maafa na baada ya maafa kutokea.
Mkakati huo umezingatia majanga ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa
mara na kusababisha madhara makubwa mkoani Mtwara. Majanga hayo
ni; Ukame, mafuriko na mlipuko wa kipindupindu.
Akizungumza wakati wa warsha ya kuwasilisha mkakati huo maafa mkoani
Mtwara tarehe 23 Aprili, 2015, Katibu Tawala Msaidizi (Uchumi na
Uzalishaji) Mkoani Mtwara, Bw. Johansen Bukwari alifafanu kuwa mkakati
huo utaongeza nguvu ya jamii kuwa na utayari wa kukabiliana na majanga
yanayowakabili ili kuokoa maisha na mali zao.
Bukwari, “Halmashauri za Mtwara Mikindani na Vijijini zimekuwa na tatizo
la kukumbwa na mafuriko, ukame na magonjwa ya mlipuko mara kwa mara
kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, ujenzi katika maeneo hatarishi
pamoja na miundombinu duni, kupitia mkakati huu kila mmoja wetu kwa
kuzingatia nafasi aliyonayo ataweza kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi.”
Awali akimkaribisha Katibu Tawala katika warsha hiyo, Mkurugenzi Idara
ya Uratibu wa shughuli za Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Brig.Jen. Mubazi
Msuya alieleza kuwa uwepo wa mkakati huo mkoani Mtwara unawezesha
ufanisi wa hatua zilizokuwa zinachukuliwa na serikali mkoani humo za
kukabiliana na maafa.
“Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuhakikisha madhara
yaliyotokea mkoani Mtwara hayajirudii ikiwa ni pamoja na kutoa elimu
kuhusu athari za ujenzi na kuendesha shughuli za uchumi katika maeneo
hatarishi, umuhimu wa usafi wa mazingira matumizi ya mbegu
zinazostahimili ukame pamoja na kuzuia ujenzi katika maeneo hatarishi”
alisema Msuya.
Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Ufadhili wa Shirika la Kuhudumia Watoto la
Umoja wa Mataifa (UNICEF), imeweza kuandaa mpango huo unaolenga
kuboresha menejimenti ya maafa katika ngazi ya mikoa nchini.
Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu shughuli za Maafa ofisi ya Waziri Mkuu, Brig.Jen. Mubazi Msuya (wa pili kulia) akifuatilia majadiliano wakati wa uwasilishaji wa Mkakati wa Mawasiliano wa kukabiliana na maafa kwa mkoa wa Mtwara tarehe 23 Aprili, 2015, kulia kwake ni Katibu Tawala Msaidizi (Uchumi na Uzalishaji) Mkoani Mtwara, Bw. Johansen Bukwari.
Baadhi ya washiriki wa warsha ya uwasilishaji wa Mkakati wa Mawasiliano wa kukabiliana na maafa kwa mkoa wa Mtwara wakifuatilia uwasilishwaji wa mkakati huo, uliofanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu wa Shughuli za Maafa mkoani Mtwara tarehe 23 Aprili, 2015.
Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu shughuli za Maafa ofisi ya Waziri Mkuu, Brig.Jen. Mubazi Msuya (Walio kaa wa pili kushoto) akiwa na washiriki wa warsha ya Kuwasilisha Mkakati wa Mawasiliano wa kukabiliana na maafa kwa mkoa wa Mtwara mara baada ya kuwasilisha mkakati huo tarehe 23 Aprili, 2015, wa kwanza kulia kwake ni Katibu Tawala Msaidizi (Uchumi na Uzalishaji) Mkoani Mtwara, Bw. Johansen Bukwari.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...