Tunapoelekea kipindi hiki cha sikukuu ya Pasaka ambayo inaanza kesho
Ijumaa Kuu, Jeshi la Polisi nchini, linatoa tahadhari kwa wananchi,
kuwa makini katika suala zima la ulinzi na usalama wa maisha na mali
zao.
Uzoefu unaonyesha kwamba, katika kipindi kama hiki cha sikukuu
kuna baadhi ya watu hupenda kutumia fursa hiyo kufanya vitendo vya
uhalifu. Hata hivyo, Jeshi la Polisi katika mikoa yote limejipanga vizuri
kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha
kwamba hakuna vitendo vyovyote vya uhalifu vitakavyojitokeza na pale
vitakapoonyesha dalili ya kujitokeza viweze kudhibitiwa kwa haraka.
Aidha, ulinzi umeimarishwa kwenye maeneo yote, yakiwemo maeneo ya
kuabudia, fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo mengine ambayo
yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu.
Vilevile, Jeshi la Polisi linawataka madereva na watu wote watakaokuwa
wakitumia barabara, kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama
barabarani, kuepuka kwenda mwendo kasi, kujaza abiria kupita kiasi na
kutumia vilevi wawapo kazini. Wamiliki wa kumbi za starehe wazingatie
uhalali na matumizi ya kumbi zao hususani katika uingizaji wa watu
kulingana na uwezo wa kumbi hizo, badala ya kuendekeza tamaa ya fedha
kwa kujaza watu kupita kiasi.
Aidha, wazazi wawe makini na watoto wao, kutokuwaacha watembee peke
yao ama kwenda disko toto bila kuwa chini ya uangalizi wa watu wazima ili
kuepusha ajali na matukio mengine yanayoweza kusababisha madhara juu
yao.
Wananchi wakumbuke kutokuacha makazi yao bila uangalizi na
endapo italazimu kufanya hivyo watoe taarifa kwa majirani zao, na pale
wanapowatilia mashaka watu wasiowafahamu watoe taarifa haraka kwenye
vituo vya polisi vilivyo karibu yao, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa
haraka.
Mwisho, Jeshi la Polisi linapenda kuwashukuru wale wote ambao tayari
wamefunga kamera za CCTV katika maeneo yao ya biashara hususani
yale yanayokuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu, yakiwemo maduka,
mahoteli na maeneo ya benki. Jeshi la Polisi linaendelea kuwasisitiza ambao
bado hawajaweka kamera hizo, kuweka ili ziweze kusaidia kubaini wahalifu
na hata kurahisisha ukamataji wa wahalifu hao endapo uhalifu unatokea.
Tunawatakia watanzania wote Pasaka njema.
Imetolewa na:-
Advera Bulimba -SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...