Mkuu wa Hazina wa Benki ya Exim, Bw. George Shumbusho (wapili kushoto) akimkabidhi hundi yenye thamani ya shilingi milioni kumi Makamu Mkuu wa Chuo cha Dodoma (UDOM), Profesa Idris Kikula (Kulia) ikiwa ni sehemu ya mchango wa benki hiyo katika mfuko maalum wa chuo hicho maarufu kama Endowment Fund, wakati wa hafla fupi jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Akishuhudia ni Meneja Msaidizi wa Masoko wa Benki hiyo, Bi Anita Goshashy
BENKI ya Exim Tanzania imechangia fedha kiasi cha shilingi mil. 10/- kwenye mfuko maalumu wa Chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) maarufu kama “UDOM Endowment Fund” ikiwa ni sehemu ya mpango wa benki hiyo kusaidia sekta ya elimu nchini.
Mfuko huo ulianzishwa na chuo hicho hivi karibuni kikilenga kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia baadhi ya mahitaji muhimu ya chuo sambamba na uwekezeaji katika fursa za kitaaluma hususani kwenye masuala ya tafiti za kisayansi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki mara tu baada ya kupokea hundi ya kiasi hicho cha pesa,Makamu Mkuu wa chuo hicho, Prof Idris Kikula alisema kwa sasa pesa yote inayopatikana inahifadhiwa kwenye akaunti maalumu ya uanzishwaji wa mfuko huo.
“Hadi kufikia sasa tumefanikiwa kupokea takribani milioni 500/-ikiwa ni pesa taslimu pamoja na ahadi kutoka kwa wachangiaji mbalimbali.Tukishakamilisha mipango yote kuhusu aina za uwekezaji ndipo tutajua kila uwekezaji utatengewa kiasi gani japo kwa kiasi kikubwa pesa nyingi itaelekezwa kwenye miradi ya tafiti,’’ alisema.
Katika kuthibitisha kuwa uwekezaji kwenye tafiti za kisayansi unaweza kuwa na tija zaidi Prof Kikula alitolea mfano mafanikio ya hivi karibuni waliyoyapata baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho ambao wameweza kubuni program maalumu inayoweza kuendesha zoezi za chaguzi mbalimbali.
“Kwa sasa programu hiyo bado inaendelea kufanyiwa majaribio na zaidi tunarajia kuitumia kwenye chaguzi zetu za wanafunzi pale pale chuo,’’ alisema Prof. Kikula huku akitoa wito kwa taasisi nyingine za fedha kuiga mfano wa benki ya Exim kwa kuchangia kwenye mfuko huo na maendeleo ya elimu kwa ujumla.
Aidha, Prof. Kikula alibainisha kuwa chuo hicho kitakuwa na wajibu wa kuhakikisha kuwa kitaendelea kuwajulisha wachangiaji wote wa mfuko huo kuhusiana na mwenendo mzima wa mfuko huo yakiwemo mafanikio yake.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkuu wa Hazina wa benki ya Exim Bw. George Shumbusho alisema benki yake iliamua kuunga mkono jitihada za chuo hicho ikiwa ni namna ya kuthibitisha umakini wake kwenye masuala yote yanayohusu sekta ya elimu na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
“Exim kamwe tusingeweza kuvumulia kuona kwamba kuna programu muhimu kama hii inaendelea ndani ya taifa letu bila kutuhusisha kwa namna yoyote ile,’’ alisema Bw. Shumbusho huku akiahidi kwa niaba ya benki hiyo kuendelea kuwezesha mfuko katika siku zijazo kulingana na matokeo na ufanisi wa mfuko.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...