WATU sita, akiwemo Mwalimu wa Shule ya Msingi Katunguru iliyoko Kata ya Wendele, Tarafa ya Msalala wilayani Kahama, wamekamatwa mjini hapa wakiwa na vipande sita vya mifupa inayodhaniwa kuwa ya albino. 

 Taarifa zilizopatikana mjini Kahama zimeeleza kwamba, mwalimu huyo Bahati Kilungu Maziku (56), Msukuma na mkazi wa Mtaa wa Mbulu katika Halmashauri ya Mji wa Kahama, amekamatwa akiwa na watu watano, wakiwemo waganga wa jadi watatu, katika harakati za kuuziana mifupa hiyo.
Wengine waliokamatwa ni mganga wa jadi Bi. Elizabeth au Shija Makandi Sweya (42), mkazi wa Busongwahala, Wilaya ya Nzega mkoani Tabora, Bilia Masanja Mhalala (39), Msukuma, mkulima na mkazi wa Mogwa wilayani Nzega, mke wa Biria ambaye ni mganga wa jadi Regina au Tatu Kashinje Nhende (40), Msukuma na mkazi wa Mogwa. 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, SACP Justus Kamugisha, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo Mei 21, 2015 na kwamba watu hao walikamatwa saa 7:00 mchana katika nyumba moja ya kulala wageni inayofahamika kwa jina la Maji Hoteli iliyopo Phantom, Kata ya Nyasubi mjini Kahama baada ya Polisi kuweka mtego kufuatia taarifa za wasamaria wema. 
Taarifa ya Kamanda Kamugisha imesema kwamba, mnamo Mei 19, asubuhi, mkuu wa upelelezi wa Wilaya ya Nzega alipata taarifa kuwa kuna mtu anauza viungo vya albino, ndipo walipoweka mtego. Hata hivyo, alisema kuwa walishindwa kuwakamata na baadaye mtu huyo alihamishia biashara hiyo wilayani Kahama. 
 Aidha, watuhumiwa wengine waliokamatwa ni Muhoja John Shija (24), Mnyamwezi na mkazi wa Isagenhe wilayani Nzega pamoja na mganga wa jadi na mfanyabiashara Abubakar Ally Magazi (25), Mrundi na mkazi wa Nzega. Taarifa za uchunguzi wa awali zinaeleza kwamba, Mwalimu Bahati ndiye aliyesuka mpango mzima akishirikiana na waganga wa jadi Bi. Shija Makandi ambaye ndiye aliyeitafuta mifupa hiyo na Abubakar Magazi ambaye alikuwa apelekewe ili ‘kuibetua’ (kuitengeneza) na kuzalisha fedha. 
 Watuhumiwa watano wanadaiwa kwamba walifunga safari kutoka Nzega hadi Kahama kwa Mwalimu Bahati, ambaye kwa mujibu wa maelezo ya awali, ndiye aliyejua ni wapi ambako mifupa hiyo ingeuzwa, hivyo walikuwa wanakutana hapo kwa ajili ya kugawana fedha. 
 Mifupa hiyo inadawa kuhusishwa na tukio la kukatwa mkono wa kulia Bi. Muungu Masaga Gedi (35) mwenye albinism, mkazi wa Kitongoji cha Mkuyuni, Kijiji cha Buhekela, Kata ya Igoweko wilayani Igunga, ambalo lilitokea Mei 16, 2014 na kufunguliwa Jalada Namba IGU/IR/1070/2014. 
 Katika tukio hilo, mume wa majeruhi huyo, Mapambo Mashili, aliuawa kwa kukatwa mapanga na watu wasiofahamika wakati akipambana na watu hao wasimdhuru mkewe.  
 Hata hivyo, amesema, jeshi la polisi bado linaendelea na msako dhidi ya watu wengine wanaotajwa kwamba ndio walioitafuta mifupa hiyo, na kwa mujibu wa taarifa za awali, ndio waliohusika na mauaji pamoja na kumjeruhi mama huyo. Picha zote za watuhumiwa hao 
zimepigwa na Daniel Mbega, Kahama

Bilia Masanja Mhalala.


Mwalimu wa Shule ya Msingi Katunguru wilayani Kahama, Bahati Kilungu Maziku.


Abubakar Ally Magazi.


Elizabeth au Shija Makandi Sweya na Regina au Tatu Kashinje Nhende.

Muhoja John Shija

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 24, 2015

    Very sad, very sad indeed
    Kwangu mimi the guilty party here is ignorance. How can you blame or punish these people if their only sin is just stupid ignorance.Lazima iwe kampeni ya kuwaelimisha wananchi kama hawa na wengine.I am not offering ignorance as an excuse, but ignorance is the culprit who commited the offence.

    ReplyDelete
  2. AnonymousMay 24, 2015

    hamna cha ignorance hapo! Kila mtu anajua kuua ni au kujerui ni kosa la jinai na kinachowasukuma kwenye upuuzi huu ni imani za kishirikina! na kama wakinyongwa hawa nina uhakika tatizo litapungua

    ReplyDelete
  3. AnonymousMay 25, 2015

    Labda nakubaliana nawe ,wanyonge wote,wachome moto. Ewe bwana mkali, utanyonga wangapi uondoe ujinga na ushirikina wetu

    ReplyDelete
  4. AnonymousMay 25, 2015

    Sura zao hazionyeshi chembe ya ukatili. Sijui nini kinawatokea watu hawa pengine ni simulizi za kijinga tu zimewapelekea kufanya hayo!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...