Na Teresia Mhagama

Imeelezwa kuwa wilaya za Chato na Biharamulo zitapata umeme wa uhakika ifikapo mwanzoni mwa mwezi Juni mwaka huu mara baada ya kukamilika kwa ufungaji wa mtambo wa pili wa umeme wilayani Biharamulo mkoani Kagera.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Kagera na kujionea maendeleo ya ufungaji wa mtambo huo utakozalisha umeme wa kiasi cha kilowati 650. Mwijage amesema kuwa mtambo huo utakaoanza kazi mwanzoni mwa mwezi Juni utaongeza kiasi cha umeme unaopatikana katika wilaya hizo mbili hivyo kuwepo kwa uhakika wa upatikanaji wa umeme wa kutosha tofauti na ilivyo hivi sasa.

"Tumeamua kuongeza mtambo wa pili kwa kuwa huu uliopo  haukidhi mahitaji ya wakazi wa wilaya hizi mbili na hii ni kwa sababu mtambo uliopo unazalisha umeme wa kiasi cha kilowati 800 wakati mahitaji ya umeme katika wilaya hizi ni kilowati 1300," alisema Mwijage.

Alieleza kuwa kukamilika kwa mtambo  huo wa kilowati 650 utafanya wilaya hizo kuwa na umeme wa kiasi cha kilowati 1450 na hivyo kuwa na ziada ya umeme wa kiasi cha kilowati 150.

Alieleza kuwa awali mtambo huo unaofungwa katika wilaya ya Biharamulo, ulikuwa ukitumika mkoani Kigoma na uamuzi wa kuupelekea mtambo husika wilayani Biharamulo ulifanyika baada ya mkoa wa Kigoma kupata mitambo mipya ya uzalishaji umeme.

“Baada ya kuuleta mtambo huu wilayani Biharamulo, Serikali ilinunua baadhi ya vipuri vipya kwani vile vya awali vilichakaa na kusababisha mtambo huu kutokufanya kazi kwa ufanisi. Kazi inayofanyika hivi sasa ni wataalam wetu wa TANESCO kubadilisha vifaa chakavu na kufunga vifaa vipya ili mtambo huu uanze kuhudumia wilaya hizi mbili,” alisema Mwijage.

Alisema kuwa wataalam wa TANESCO watafanya majaribio ya mtambo huo ifikapo Mei 30 mwaka huu na majaribio hayo yatafanyika kwa muda wa siku tatu mfululizo hadi hapo mtambo utakapozinduliwa rasmi Juni 4, 2015.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage (kushoto) akikagua mtambo wa umeme utakaozalisha kiasi cha kilowati 650, unaofungwa katika wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage (wa pili kulia) akiangalia vipuri vitakavyofungwa katika mtambo wa umeme utakaozalisha kiasi cha kilowati 650 wilayani Biharamulo. Mtambo huo uliokuwa ukitumika mkoani Kigoma umehamishiwa wilayani Biharamulo baada ya mkoa wa Kigoma kupata mitambo mipya.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage (wa kwanza kushoto) akikagua baadhi ya mitambo ya umeme, katika wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, wakati alipokuwa katika ziara yake ya kikazi mkoani humo kwa lengo la kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...