Asilimia 73 ya maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) yanayotokea  miongoni mwa vijana Barani Afrika huwapata wasichana  huku asilimia 15 ya vijana wote  ndiyo wanaotambua hadhi yao ya VVU na hivyo kusababisha  tatizo hilo kuendelea kuwa  kubwa.
Hayo yamesemwa leo na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea kwenye mkutano wa 15 wa Umoja wa wake wa Marais wa Afrika wa Kupambana na Ugonjwa wa Ukimwi (OAFLA) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo Sandton Convention Centre mjini Johannesburg Afrika ya Kusini.
Mama Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema tatizo la VVU na Ukimwi bado ni kubwa miongoni mwa vijana wa kike na kama wataendelea kuambukizwa kwa kiwango hicho kutakuwa na muda mrefu wa kupambana na maambukizi kwa wenzao ambao hawajaambukizwa na kutahitajika muda mrefu wa matumizi ya dawa za kufubaza VVU ambazo ni ghali.
“Ushauri wangu kwenu ni kuongea juhudi zaidi ili kupaza sauti za watoto wetu wa kike ambao wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa VVU, kufanya mapambano dhidi ya Ukimwi kuwa  ni agenda ya kudumu ya OAFLA kila tutakapotayarisha mipango yetu ya taarifa mapambano dhidi ya VVU ni muhimu kujumuishwa”, alisisitiza Mama Kikwete.
Kwa upande wa elimu Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema upatikanaji wa elimu bora kwa mtoto wa kike kutafungua fursa za kuweza kuboresha afya, kipato chake na hatimaye kujiongezea uwezo wake binafsi na familia kwa ujumla.
Alisema, “Tunatambua kwamba kwa kadri mtoto wa kike anavyokaa muda mwingi shuleni ndivyo anavyoweza kuepuka uzazi katika umri mdogo, vifo vinavyotokana na matatizo ya uzazi na umaskini”.
Mama Kikwete alisema ili kukabiliana na changamoto hizo Taasisi ya  WAMA  imeendesha kampeni ya mtoto wa mwenzio ni mwanao;Mkinge na Ukimwi kwa njia za upashanaji habari, mafunzo na uraghibishi kwa kutoa mafunzo ya stadi za maisha na ujinsia kwa vijana wa rika mbalimbali ili kuwawezesha kuepuka ujauzito na maambukizi ya VVU.
“Tumetekeleza afua mbalimbali za kusaidia kutokomeza maambukizi mapya ya VVU kutoka kwa Mama Kwenda kwa mtoto (EMTCT), kushirikiana na jamii za wafugaji ili kuepuka desturi zinazochochea vifo vya kina mama vitokanavyo na uzazi katika umri mdogo, tohara kwa wasichana na unyanyasaji wa kijinsia na kutekeleza kampeni ya kupima na kutibu mabadiliko ya awali ya saratani ya shingo ya kizazi”, alisema Mama Kikwete.
Akiwakaribisha wake hao wa Marais, Mke wa Rais wa Afrika ya Kusini Mama Thobeka Madiba Zuma alisema muda umefika kwa wao  kuonyesha majukumu yao katika Bara la Afrika kwa kuungana  kwa pamoja na viongozi wa jamii zao ili waweze  kuondoa unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake zikiwemo mila kandamizi, kusimamia ili wanawake wapate haki za uchumi, afya ya uzazi na kulinda haki za  wazee, walemavu na watoto.
“Vijana wapate elimu ya afya ya uzazi huduma ya kuzuia  maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ipatikane kwa urahisi kwa wanawake walio na maambukizi hii itasaidia  wanawake kujifungua watoto  wasio na maambukizi na hivyo kutokuwa na maambukizi katika vizazi vijavyo”, alihimiza Mama Thobeka.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Ukimwi (UNAIDS) kutoka Umoja wa Afrika (AU) na Tume ya kushughulikia Uchumi ya Afrika (ECA) Rosemary Museminali alisema kama jamii itaamua kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja ikiwa ni pamoja na kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali pamoja na mashirika binafsi ya kupambana na ugonjwa wa Ukimwi inawezekana kwa kiasi kikubwa kumaliza maambukizi ya VVU.
Rosemary alisema,  “Katika nchi za Afrika msichana mmoja kati ya wasichana 10 wenye umri wa chini ya miaka 15  ana mtoto, wasichana hawa wanatakiwa kuwa  shule na kubeba vitabu na siyo kubeba watoto pia wako katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya VVU
Mkutano huo wa wake wa marais wa Afrika ulienda sambamba na mkutano wa 25 wa wakuu wa nchi na viongozi wa Serikali wa Afrika uliomalizika  leo mjiniJohannesburg.
Wake wa Marais na Wakuu wa Nchi za Afrika wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya ufunguzi wa mkutano wao wa mwaka unaozungumzia uwezeshaji kwa wanawake na Maendeleo katika Bara hili. 
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akitoa hotuba yake ya mwisho kwenye kikao cha Wake wa Marais na Wakuu wa Nchi za Afrika kinachofanyika kwenye Ukumbi wa Sandton jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini.
Kwa picha zaidi BOFYA HAPA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...