Mkazi wa kijiji cha Masanga wilayani Same, Magreth William akiwaangalia mbuzi wake aliowapata kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia mradi wa Kupunguza Athari za Ukame unaofadhiliwa na UNICEF, tarehe 2, Juni 2015.
Mkaguzi Hesabu za Serikali, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu Hesabu za Serikali nchini, (kushoto), Jacob Ndaki akimsikiliza Mkulima wa mtama, kijijini Masanga wilayani Kishapu, Magreth William (kulia ) wakati wa ufuatiliaji wa utekelezaji mradi wa Kupunguza Athari za Ukame unaoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, (katikati) ni Mratibu maafa wilayani Kishapu, Posian Kuhabwa, tarehe 2 Juni, 2015.
Halmashauri ya wilaya ya Kishapu imefanikiwa kupunguza athari za maafa yanayotokana na ukame kwa kutekeleza vyema mradi wa kujengea jamii uwezo wa kukabili maafa ya ukame unaoratibiwa na Ofisi ya waziri mkuu, idara ya uratibu maafa.
Mradi huo wenye kauli mbiu “Athari za Ukame zinapunguzika jamii husika ikijengewa uwezo”, umetekelezwa wilayani humo kwa mafanikio katika kata ya Mwamalasa, Masanga na Langana kutokana na vikundi vya maendeleo kumi (10) kufanikisha ufugaji wa Mbuzi na kuku, kilimo cha viazi, mtama, mboga mboga pamoja na upandaji wa miti kwa uhifadhi wa mazingira.
Akiongea wilayani humo mara baada ya kuiongoza timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya waziri Mkuu inayofuatilia utekelezaji wa mradi huo tarehe 2 Juni, 2015, Mratibu maafa Wilayani Kishapu, Ponsian Kuhabwa amefafanua kuwa kwa kutumia vikundi vya maendeleo katika kata husika kwa utekelezaji, kata hizo zimefanikiwa kupata uhakika wa chakula na kipato, hali ambayo huzifanya kata hizo kutoathiriwa na ukame.
Kuhabwa; “Kikundi cha Mazingira kata ya Masanga chenye watu 10, kupitia mradi huu kinao mbuzi 200, kuku 200 ikiwa awali walipatiwa mbuzi 50 na kuku 50 kwa ajili ya kuanza ufugaji, lakini pia kikundi hiki kinayo mashamba ya mtama, viazi lishe na bustani za mboga mboga hali inayo ifanya jamii inayotekeleza mradi huu kufanikiwa kupunguza athari zitokanazo na ukame ”.
Akiongea na timu ya wataalamu hao, mkazi wa kijiji cha Masanga, kata ya Masanga, wilayani Kishapu, Magreth William, amefafanua kuwa ukame uliokuwa ukiikumba kata hiyo mara kwa mara, walikuwa wanapata athari za upungufu wa chakula pamoja na kutokuwa na kipato kutokana na mazao yao ya biashara kuharibikia mashambani.
William; “Tumeweza kupunguza athari za maafa ya ukame kupitia mradi huu kwa kuwa tunaouhakika wa chakula kwa kuwa tunalima mazao yanayo himili ukame kama mtama na viazi lishe lakini pia tunao uhakika wa kipato kwa kuwa tunafuga mbuzi na kuku hivyo pamoja na ukame unaendelea kujitokeza lakini kwa sasa hatuathiriki kama awali”.
Mradi wa Kuijengea Jamii Uwezo wa Kupunguza Athari za Maafa kwa Mikoa iliyoathirika zaidi na ukame unafadhiliwa na Benki ya Dunia na kusimamiwa na UNICEF chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Halmashauri husika wakiwa Watendaji wakuu wa mradi huo. Mradi huo unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 18, ulizinduliwa wilayani Same, mkoani Kilimanjaro tarehe 11 Desemba, 2013.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...