Na  Bashir  Yakub.

Kisheria yapo  mazingira  ambapo  mtu  aliyeuza  ardhi  anaweza  kuidai tena  ardhi  ileile  aliyouza kutoka kwa mnunuzi na  akaipata. Na  hapa  haijalishi  kama  mnunuzi  ameiendeleza  ardhi  kwa  kiasi  gani au  amebadilisha hati na kuingia  jina  lake  na  vitu  vingine  kama  hivyo.  

Sheria  imetoa  haki  hii  kwa  muuzaji  hasa  iwapo  masharti  katika   mkataba  wa  mauziano  yamevunjwa. Kwa  kawaida  kila  mkataba  wa  mauziano  ya  ardhi  huwa  na  masharti  ambayo  hupaswa  kutekelezwa na  kila  upande. Masharti  haya  huwa  ni  ya  msingi  na  hupaswa  kutekelezwa  vilevile  kama  ilivyokubaliwa. 

Kuvunjwa/kukiukwa  kwake  hutoa  haki  kwa  muuzaji  kuchukua  tena  kilicho  chake yaani  kujirejeshea  umiliki  wa  ardhi. Na  hii  mara nyingi  husababishwa  na  kuingia  mikataba  kiholela  bila  kupata  ushauri  au  kusimamiwa  na  wanasheria ambao hupanga masharti  haya  kwa ufundi  usio na madhara. Hapa  chini tutaona  jambo  hilio hufanyikaje  kisheria.

1.MUUZAJI  KUJIMILIKISHA  TENA  ARDHI  BAADA  YA  KUUZA.

Sehemu  ndogo  ya  tatu,  kifungu  cha 73 – 76 cha  Sheria  ya Ardhi   ndivyo  vifungu  katika sheria  ya  ardhi  vinavyoeleza  kwa  urefu  namna  ya  kujimilikisha  tena  ardhi  baada  ya  kuiuza. 

 Kifungu  cha  73  kinaanza  kwa  kusema  kuwa.   mkataba  wa  mauziano  ya  ardhi  unapokuwa  umekamilika   na  mnunuzi  ameshakuwa  mmiliki  wa  ardhi  aliyonunua,  muuzaji  anaweza  kujitoa  katika  mkataba  huo   pale  ambapo  mnunuzi  atakiuka  au  kwenda  kinyume  na  masharti  au  makubaliano  katika  mkataba  huo. Maana  iliyo katika  kifungu hiki  ni  kuwa  tayari mkataba  umekamilika,  na mnunuzi  amemiliki  lile  eneo iwe  nyumba, shamba  au  kiwanja . 

Na  amemiliki  kwa  kiwango  kuwa  mpaka hati/leseni  ya  makazi/ofa n.k   tayari  ina  jina  lake,  lakini  kuna  mambo  aliahidiana  na yule  aliyemuuzia  na  bado  hajayatekeleza  mpaka  sasa. Basi  huyu  aliyemuuzia  ana  haki ya  kudai  umiliki  au  kuchukua  tena  ile  ardhi. Anachukuaje  ile  ardhi  tutaona  hapa  chini.

2.  SABABU  ZA  KUJIREJESHEA  UMILIKI  BAADA  YA  KUUZA.

Sababu  kubwa za  kisheria  za  muuzaji  kujitoa  katika  mkataba  na  kujirejeshea  umiliki  ni  kutokufuatwa  kwa  masharti  au  makubaliano  yaliyo  katika  mkataba  wa  mauzo( sale  agreement).  

Kwa  mfano  kutomaliziwa  kwa hela . Unakuta  mnunuzi  ameahidi  kuwa  atamalizia  kiwango  cha  hela  kilichobaki  ndani  ya  miezi  mitatu  tangu  siku  ya  kusainiwa  kwa  mkataba. Muda  huo  unafika  mpaka  unapita mnunuzi  hataki  kulipa  hela  na  tayari  anamiliki  eneo. Au  ni  ardhi  ya kijiji  na  ameahidi  kuiendeleza  ndani  ya muda  fulani  lakini  bado  hajafanya  hivyo na  muda  umepita sasa.  Haya  ndio  mazingira na kwa  ufupi  hii  huhusisha  kutotekelezwa  kwa yale  aliyoahidi  mnunuzi   katika  mkataba  wa mauzo si  lazima  yawe hayo  tu  niliyotaja.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...