Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako  Manongi na  Mwakilishi wa Kudumu wa Malta katika Umoja wa Mataifa,  Balozi Christopher  Grima wakipongezana  mara  baada ya  kutia sahihi  hati  walizoshika za kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia katika ngazi ya Mabalozi. Hati hizo baadaye ya zitawasilishwa  rasmi  kwa  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. 

Na Mwandishi Maalum, New York

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya  Malta zimekubaliana kuanzisha uhusiano  wa kidiplomasia baina  yao. Wawakilishi wa Kudumu wa  mataifa hayo mawili katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi wa Tanzania na Christopher Grima  wa  Malta ndio waliotia sahihi hati za kuridhia kuanzishwa kwa  uhusiano huo na ambao utakuwa katika ngazi ya  Mabalozi.

Wakizungumza mara baada ya  utiaji sahihi hati hizo, wawakilishi  hao wameelezea kuwa kuanzishwa kwa uhusiano  huo ni hatua muhimu  sana katika kukuza na kuendeleza ushirikiano na uhusiano  kati ya mataifa hayo mawili na  watu wake. Tanzania  imekuwa ikinufaika kwa ufadhili wa nafasi za masomo  kutoka  Malta kwa watumishi mbalimbali  wakiwamo wa Wizara ya Mambo ya Nje na  Ushirikiano wa Kimataifa na    Wizara nyingine.  
Wawakilishi wa Kudumu wa Tanzania,  Balozi Tuvako  Manongi na  Christopher  Grima Malta wakitia sahihi hati za kuanzisha uhusiano wa  kidiplomasia katika ngazi ya Mabalozi. Wanaoangalia utiaji sahihi  ni   Tully Mwaipopo Afisa Mwandamizi  wa Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania na Bw. Alan Cordina, Afisa wa Uwakilishi wa  Kudumu wa Malta.
 Mhe. Jaji Mkuu Mohamed Othman Chande katika picha hii ya maktaba, mwishoni mwa wiki aliwasilisha ripoti ya  Jopo lake lililoundwa  na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  kupitia na  kuchambua taarifa mpya  kuhusu kifo cha Bw. Dag Hammarkjold,  kilichotokea mwaka 1961.  Jopo hilo  ambalo  liliongozwa na Mhe. Jaji Mkuu  lilikuwa na washirika wengine kutoka Denmark na Australia  na liliundwa Mwezi March 2015, kwa mujibu wa Azimio namba 69/246 la Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa    walitakiwa kuwasilisha taarifa yake si Zaidi  ya  tarehe 20 mwezi huu wa June

Katika hatua nyingine,  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon amepokea  ripoti ya Jopo huru la wataalamu  alilounda kupitia na kuchambua taarifa mpya kuhusu  kifo cha   Bw. Dag Hammarskjold aliyewahi kuwa  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Kiongozi wa  Jopo hilo alikuwa  Mhe. Jaji Mkuu wa Tanzania Othman Chande akishirikiana na wanajopo wengine ambao ni  Bw. Kerry Macaulay kutoka Australia na Bw. Henrik  Larsen  wa Denmark.

Kwa  mujibu wa taarifa iliyotolewa na   Msemaji wa Katibu Mkuu,  inaeleza kwamba, Katibu Mkuu  ameipokea taarifa hiyo  na kuwashukuru wanajopo  hao kwa kazi nzuri na kubwa na kwa  mchango wao muhimu katika kutafuta ukweli kuhusu mazingira yaliyosababisha kifo cha  Katibu Mkuu wa zamani  Dag Hammarskjold pamoja na  wajumbe wengine aliokuwa  amefuatana nao usiku wa  tarehe 17-18 September  1961.

Taarifa hiyo inaeleza zaidi kwamba,  Katibu Mkuu, ameridhishwa kwamba jopo  hilo liliweza kwenda  Zambia na kuzungumza na  mashahidi na kwamba  jopo limeweza kukusanya nyongeza  ya taarifa mpya kutoka kwa nchi  wanachama na vyanzo vingine zikiwamo   maktaba  binfasi   huko Belgium, Sweden na  Uingereza.

Taarifa ya msemaji wa Katibu Mkuu  inaeleza kuwa  Katibu Mkuu ataipitia   taarifa hiyo  kwa umakini mkubwa na kwa  haraka  na  kisha kwa ataiweka ripori hiyo  pamoja na uchambuzi wake(Katibu Mkuu)  na  mwelekeo wa baadaye kwa Nchi Wanachama mapema iwezekanavyo.

TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO WA SHERIA YA  BAHARI

Bi. Monica Otavu,  Wakili wa Serikali Mkuu,  akizungumza wakati wa Mkutano wa  25 wa  Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Sheria ya Bahari. Katika   Mkutano huo wa wiki  moja   pamoja na  masuala  mengine, wajumbe walitambua na kupongeza mchango  mkubwa unaofanywa na vyombo vinavyoundwa na   Mkataba huo .  Vyombo hivyo ni  Mahakama ya Migogoro ya  Bahari ,   Kamisheni ya mwambao wa  Bahari ( Commission on Limits of Continental Shelf),  na  Mamlaka ya Kimataifa chini ya Bahari ( International Seabed Authority

WANAFUNZI WA FEZA WATEMBELEA UWAKILISHI
Pichani ni Baadhi ya  Wanafuzi wa  Shule ya Feza Tanzania na viongozi wao  ambao wapo  hapa  Marekani kwa ziara ya  mafunzo walipata nafasi ya kufika katika uwakilishi wa kudumu wa Tanzania  na  walibadilishana  mawazo na Naibu Mwakilishi wa  Kudumu,  Balozi Ramadhan Mwinyi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...