Na Teresia Mhagama
Imeelezwa kuwa Wilaya za Chato na Biharamulo zitaanza tena kupata umeme wa uhakika ifikapo Jumapili ya tarehe 19 Julai, 2015 baada ya kukamilika kwa ukarabati wa mtambo wa umeme wa kilowati 650 unaohudumia wilaya hizo.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Kagera na kujionea maendeleo ya ufungaji wa mtambo huo wa pili uliofungwa wilayani Biharamulo ambao ulianza kufanya kazi mwanzoni mwa mwezi Juni mwaka huu.
Mwijage amesema kuwa mtambo huo ulipata hitilafu ambapo kifaa kijulikanacho kama crankshaft kilikatika hivyo wataalam kutoka Shirika la Umeme nchini (TANESCO) wanaendelea kufunga crankshaft nyingine ambayo imetolewa katika mtambo wa umeme ulioko mkoani Kigoma ambao hautumiki kwa sasa.
Alisema kuwa mtambo huo wa kilowati 650 umeongeza kiasi cha umeme uliokuwa ukipatikana katika wilaya hizo mbili hivyo hivi sasa upo uhakika wa upatikanaji wa umeme wa kutosha tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
"Tuliamua kuongeza mtambo wa pili kwa kuwa ule wa kwanza ulikuwa haukidhi mahitaji ya wakazi wa wilaya hizi mbili na hii ni kwa sababu mtambo huo ulikuwa ukizalisha umeme wa kiasi cha kilowati 800 wakati mahitaji ya umeme katika wilaya hizi ni kilowati 1300," alisema Mwijage.
Alieleza kuwa kukamilika kwa mtambo huo wa kilowati 650 kumezifanya wilaya hizo kuwa na umeme wa kiasi cha kilowati 1450 na hivyo kuwa na ziada ya umeme wa kiasi cha kilowati 150.
Alisema kuwa awali mtambo huo wa kilowati 650 uliofungwa katika wilaya ya Biharamulo, ulikuwa ukitumika mkoani Kigoma na uamuzi wa kuupeleka mtambo husika wilayani Biharamulo ulifanyika baada ya mkoa wa Kigoma kupata mitambo mipya ya uzalishaji umeme.
“Baada ya kuuleta mtambo huu wilayani Biharamulo, Serikali ilinunua baadhi ya vipuri vipya kwani vile vya awali vilichakaa na kusababisha mtambo huu kutokufanya kazi kwa ufanisi. Wataalam wetu wa TANESCO walibadilisha vifaa chakavu na kufunga vifaa vipya ili mtambo huu uanze kuhudumia wilaya hizi mbili,” alisema Mwijage.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage (wa
kwanza kushoto) akizungumza na na
wataalam kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ambao wanakarabati kifaa kilichopata hitilafu (crankshaft) katika mtambo wa kuzalisha
umeme wa kilowati 650 uliofungwa
wilayani Bharamulo ambao unatarajia kuanza tena kuzalisha umeme siku ya
Jumapili.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage (wa
kwanza kushoto) akiangalia housing ya kifaa kilichopata hitilafu (crankshaft) katika mtambo wa kuzalisha
umeme wa kilowati 650 uliofungwa wilayani Bharamulo ambao unatarajia kuanza
tena kuzalisha umeme siku ya Jumapili. Anayetoa maelezo ni mtaalam kutoka Shirika la Umeme nchini
(Tanesco), Mhandisi John Magembe.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage
(katikati) akiweka saini katika Kitabu
cha Wageni mara baada ya kufika katika Ofisi za
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wilayani Biharamulo kukagua
maendeleo ya ukarabati wa kifaa
kilichopata hitilafu (crankshaft)
katika mtambo wa kuzalisha umeme wa kilowati 650 uliofungwa wilayani Bharamulo ambao
unatarajia kuanza tena kuzalisha umeme siku ya Jumapili.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...