Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akimpongeza Askofu Mkuu Wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT) Dkt.Stephen Munga wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 125 ya dayosisi hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Mbuyukenda mjini Tanga leo. Picha na Freddy Maro.
------------------------------------
Kusoma hotuba yote BOFYA HAPA
------------------------------------
Sehemu ya hotuba ya Rais Kikwete juu ya
Dhima ya Viongozi wa Dini na Uchaguzi Mkuu
Huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu ambao pia una umuhimu wa aina yake katika historia ya nchi yetu. Tunaiaga Awamu ya Nne na kuikaribisha Awamu ya Tano ya uongozi wa nchi yetu. Niruhusuni nitumie fursa hii kuwaomba viongozi wa dini muiombee nchi yetu ipite kipindi hiki kwa salama na amani.
Dhima ya Viongozi wa Dini na Uchaguzi Mkuu
Huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu ambao pia una umuhimu wa aina yake katika historia ya nchi yetu. Tunaiaga Awamu ya Nne na kuikaribisha Awamu ya Tano ya uongozi wa nchi yetu. Niruhusuni nitumie fursa hii kuwaomba viongozi wa dini muiombee nchi yetu ipite kipindi hiki kwa salama na amani.
Uzoefu wa nchi nyingi za
Afrika, chaguzi hutoa mwanya kwa uvunjifu wa amani. Haijawa hivyo kwetu, lakini
haina maana kuwa tunayo kinga ya milele. Hata na sisi tunaweza kuwa kama wale
iwapo yale yaliyowafikisha wenzetu hapo hatutayaepuka.
Mafanikio yetu ya kuendesha uchaguzi
kwa amani na usalama yametokana na tahadhari ambazo Serikali na viongozi wa
dini tumekuwa tukizichukua. Tuendelee kufanya hivyo. Tusiwape mwanya
wanasiasa wenye dhamira ovu kuwafarakanisha Watanzania.
Tuendelee kukemea matumizi mabaya ya
fedha, rushwa, hila, ghilba na hujuma katika chaguzi. Tunapaswa
kufanya hivyo tena zaidi sasa, wakati wa michakato ya ndani ya vyama vya siasa
na baadae wakati wa uchaguzi.
Tuwakemee wanasiasa wapenda madaraka
kwa gharama yoyote, ambao watataka kutumia fedha kununua ushindi au
ubaguzi wa rangi, kabila, dini na kadhalika, kuwabagua wapinzani wao na
kujijenga kisiasa.
Nawaomba msiwasikilize wala kuwaendekeza
kwani mchezo wao ni mauti yetu. Wakatalieni kwa macho makavu na kwa
kweli.
Hatupaswi kukaa kimya dhidi ya watu wanaokiuka
maadili na kuchochea mifarakano katika taifa letu. Hawa si watu wema
watatufikisha pabaya. Hawaitakii mema nchi yetu. Kamwe tusiruhusu
wachezee dini zetu ambazo ni mhimili muhimu sana wa amani yetu.
Tofauti na ukabila ambao pamoja na ubaya wake,
lakini unaweza kuhusisha eneo dogo, dini unahusisha nchi nzima. Hakuna
mtu, dini wala eneo litakalonusurika. Tutapoteza ile sifa yetu ya kihistoria ya
kuwa lulu na mfano wa amani katika Afrika.
Tusikubali kumchukiza Mungu akatukasirikia
na kutuadhibu kwa jambo ambalo liko ndani ya uwezo wetu kulizuia
lisitokee. Kwa kweli mambo yakiharibika, hatuwezi kumlaumu mtu
mwingine yeyote bali sisi wenyewe. Katu hatuwezi kusema ni mapenzi
ya Mungu bali itakuwa ni makosa yetu wenyewe.
Nawaomba viongozi wa dini
mlisaidie taifa letu. Limeni mraba wenu vizuri nasi tulime wetu. Msiwape
nafasi viongozi wa siasa na hata wa dini kutumia majukwaa ya dini kuendeleza
maslahi yao ya kisiasa na hasa kupandikiza chuki katika jamii.
Tunawategemea
viongozi wa dini msiwe sehemu ya makundi ya wagombea au vyama vya siasa.
Mnatakiwa msiwe na upande bali muwe juu ya pande zote. Hapo ndipo
mtakapofanya vizuri kazi yenu ya ulezi na kuponya taifa iwapo kutatokea
matatizo.
Hatuwategemei viongozi wa
dini muwapangie waumini wenu vyama au viongozi wa kuwachagua. Tunawategemea
kuwahimiza na kuwakumbusha kuutumia haki na wajibu wao vizuri,
muwahimize na kuwakumbusha kuwa watatakiwa kufanya mambo matatu muhimu.
Kwanza,
kujiandikisha, pili, kujitokeza kwenda kupiga kura
na tatu kuchagua viongozi wazuri, wasiokuwa waovu, wasiofanana na
uovu na kuukaribia uovu, watakaosukuma mbele gurudumu la maendeleo na kujali
maslahi mapana ya jamii husika na nchi yetu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...