Na Mwandishi wetu, Muheza
Ushirikishwaji wa wananchi na uongozi mzuri ni nyenzo muhimu za kuleta maendeleo katika wilaya ya Muheza, mkoani Tanga.
Akihutubia wananchi waliojitokeza kumuunga mkono mwishoni mwa wiki wilayani Muheza, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Adadi Rajabu alisema maendeleo duni katika wilaya hiyo yametokana na uongozi mbaya.
Alikua akichukua fomu za kugombea ubunge jimbo la Muheza kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Muda wa mabadiliko umefika,” alisema balozi huyo na kuongeza: “ili wilaya hii iendelee tunahitaji uongozi mzuri na ushirikishwaji wananchi.”
Aliwaambia mashabiki wake kuwa anagombea ubunge kwa kuwa anaamini kuwa uongozi wa sasa haujachukua hatua zinazostahili katika kusaidia wananchi kupata maendeleo wanayohitaji.
Alisema upatikanaji wa maji safi na salama ya uhakika, barabara na elimu bora vitakuwa vipaumbele atakavyoshughulikia haraka.
Alisema haikubaliki kwa kina mama kutembea umbali mrefu kutafuta maji na kuahidi kumaliza tatizo hilo.
“Nikiwa mbunge wenu, tatizo hili litakwisha,” aliahidi.
Alisema atahakikisha anaishawishi serikali kuleta walimu wa kutosha katika wilaya hiyo kwa kuwa madarasa pekee haina maana ya elimu bora kwa watoto.
Bw. Rajabu alisema barabara mbovu ni kikwazo kwa maendeleo ya wakulima wa wilaya hiyo ambao wanashindwa kusafirisha mazao yao sokoni na kujiongezea kipato.
“Changamoto zote hizi zinahitaji muwakilishi mzalendo atakayekuwa tayari kufanya kazi na wana Muheza kumaliza tatizo la umaskini,” alisema mwana usalama huyo mzoefu mstaafu, ambaye kabla ya kuwa balozi aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) katika Jeshi la Polisi Tanzania.
Aliyekua
Balozi wa Tanzania Nchini Zimbabwe, Mh. Adadi Rajabu (kulia) akipokea fomu
kutoka kwa katibu wa CCM Wilaya ya Muheza, Tija Magoma kuomba ridhaa ya
kugombea ubunge katika jimbo la Muheza kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM)
hivi karibuni wilayani Muheza.
Aliyekua
Balozi wa Tanzania Nchini Zimbabwe ,
Mh. Adadi Rajabu (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)
muda mfupi baada ya kuchukua fomu na kuelezea nia yake ya kugombea ubunge
katika jimbo la Muheza kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivi karibuni. Kulia ni Mwenyekiti wa CCM kata ya Majengo,
Bw. Ali Kanyika.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...