Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe, amesema upatikanaji wa gesi ni nyenzo muhimu ya uendelezaji wa viwanda vya kati ili kutengeneza ajira na kuharakisha maendeleo ya nchi.
Mhe. Membe alipongeza uamuzi wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kuichagua Tanzania kuwa miongoni mwa nchi tatu za Afrika itakapohamishia baadhi ya viwanda vyake, akazitaka taasisi za uwekezaji na uendelezaji wa viwanda kuweka mikakati madhubuti ya kutumia fursa hiyo kikamilifu.
Mhe. Waziri alisema hayo leo wakati wa mhadhara wa aliyekuwa Mchumi Mkuu na Makamu wa Rais Mwandamizi wa Benki ya Dunia, Prof. Justin Yifu Lin, kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, jijini Dar Es Salaam, uliohudhuriwa na wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na wadau wengine.
Alisema uendelezaji wa viwanda lazima utiliwe mkazo katika mpango wa Tanzania kuingia uchumi wa kati 2025. "Tuache kukimbilia viwanda vikubwa vinavyohitaji mitaji mikubwa, ambayo hatuna.Tuchague viwanda vya kati vitakavyoajiri watu wengi kwa uwekezaji wa wastani."
Mhe. Membe alisema uendelezaji wa viwanda usambae nchi nzima ili kuvutia vijana kuishi vijijini badala ya kukimbilia mijini. "Sasa hivi nchi yetu ina viwanda takriban 3,000 lakini zaidi ya theluthi mbili viko Dar Es Salaam. Lazima umeme upelekwe vijijini kuleta uwiano wa maendeleo ya viwanda," alisisitiza.
Katika mhadhara wake, Prof. Lin alisema nchi nyingi zinazoendelea zilifanya maamuzi yasiyo sahihi kuhusu viwanda. "Nchi nyingi zilifuata kile kinachoitwa Muafaka wa Washington na kuanzisha viwanda vikubwa kwa maelekezo ya nchi tajiri, ambavyo viliwashinda kuendesha kwa kuwa vilihitaji uwekezaji mkubwa sana."
Alisema nchi za Asia zilizoendelea kwa haraka ni zile zilizoamua kuzingatia mazingira halisi na kwenda hatua kwa hatua katika kuanzisha viwanda. "Hii iliimarisha uchumi wao na kuukuza."
Prof. Lin alisema serikali zina wajibu wa kusimamia uendelezaji wa viwanda kwa kuweka sera sahihi, kuhimiza uwekezaji kwenye uzalishaji wa bidhaa zenye masoko ya uhakika na kusaidia sekta binafsi ishiriki kikamilifu.
Akiongelea Tanzania, Mchumi huyo wa Kichina alisema ingawa gharama za ajira ziko chini, gharama za uendeshaji ziko juu, hivyo hazivutii uwekezaji. Alisema moja ya sababu kubwa za Shilingi ya Tanzania kushuka thamani ni uuzaji mdogo wa bidhaa nchi za nje.
Makamu wa Rais wa zamani wa Benki ya Dunia, Prof. Justin Yifu Lin akitoa mada yake juu ya uwanzishaji wa viwanda nchini Tanzania katika muadhara ulioandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje. BOFYA HAPA KWA PICHA ZAIDI |
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...