NA RAMADHANI ALI-MAELEZO
CHUO cha Uongozi wa Fedha Zanzibar (ZIFA) kitaanzisha Tawi lake Kisiwani Pemba kuanzia mwaka huu wa masomo na kitaanza kufundisha masomo ya uongozi wa fedha ngazi ya cheti.
Akizungumza na waandishi wa Habari Makao Makauu ya ZIFA Chwaka, Kaimu Mkuu wa Taaluma Dkt. Iddi Salum Haji amesema wameamua kufungua Tawi Pemba ili kuzipunguzia gharama familia zenye kipato cha chini.
Amesema utafiti uliofanywa na Chuo umegundua kuna vijana wengi Kisiwani Pemba waliomaliza kidato cha nne na wanazo sifa za kujiunga na chuo kwa masomo ya cheti lakini wanashindwa kutokana na familia zao kukosa uwezo wa kuwasomesha.
Ameongeza kuwa chuo kimejipanga na kukamilisha taratibu zote za kutoa mafunzo hayo katika Mji wa Wete na wanafikiria kuanzisha Tawi Mjini Dar es salaam hapo baadae.
Dkt. Iddi amesema lengo la Chuo hicho ni kujipanua zaidi hasa kufuatia matokeo mazuri ya mitihani ambapo mwaka huu asilimia 98.3 ya wanafunzi 870 waliofanya mitihani kuanzia ngazi ya cheti mpaka shahada ya kwanza wamefaulu vizuri.
“Wanafunzi waliohitimu fani ya Uhasibu wamepasi asilimia mia, IT asilimia 97 na fani ya Ugavi na Ununuzi wamefaulu kwa asilimia 98,” amesema Kaimu Mkuu wa Taaluma.
Amesema mafanikio hayo yamepatikana kutokana na wanafunzi kujituma zaidi na walimu kujitolea kwa uwezo wao wote na kuwa wabunifu katika kufundisha.
Ameeleza kuwa baadhi ya fani zinzofundishwa na chuo cha Uongozi wa Fedha yanaelekeza zaidi kwa vitendo na yanawasaidia wahitimu kuweza kujiajiri wenyewe.
Dkt. Iddi amewashauri wazazi kuwa waangalifu wakati vijana wao wanapotafuta nafasi za kujiunga na Taasisi za elimu ya juu na kuwataka wahakikishe wanawapeleka kwenye vyuo vyenye sifa na vilivyosajiliwa na kutambuliwa na Bodi za elimu ya juu NACTE na TCU.
“Hivi sasa kumeibuka msururu wa vyuo vinavyojitangaza vinatoa mafunzo ya Elimu ya juu lakini wanafunzi wanapomaliza na kutafuta ajira ama masomo ya juu inakuwa vigumu kupata kutokana na kuwa havitambuliki,” alisema Dkt. Iddi.
Kaimu Mkuu wa Idara ya Masomo ya jumla ZIFA Maalim Said Mohd amesema chuo hivi sasa kimejipanga kuteremka ndani ya jamii kwa kutoa elimu kwa wajasiriamali ili waweze kujiendesha wenyewe.
“Kwa kuanzia chuo tayari kimeendesha mafunzo ya ujasiriamali kwa vikundi vya Wilaya ya Kaskazini A, Wilaya ya Kati na Wilaya Kusini kwa Unguja na Chake chake na Micheweni Pemba na lengo ni kumaliza Wilaya zote za Zanzibar,” alisisitiza Maalim Said.
Mmoja wa wanafunzi waliomaliza masomo mwaka huu Bakar Omar Hamad ameishauri Wizara ya elimu kufanya mapitio ya Taasisi zinazotoa elimu ya juu nchini ili kuhakikisha uhalali wa usajili wao, mitaala inayotumika inalingana na masomo na kuhakikisha walimu wanazo sifa zinazokubalika.
Amesema wazazi wamekuwa wakiwekeza fedha nyingi kuwasomesha watoto wao lakini baadhi ambao mwamko wa kielimu ni mdogo wanawapeleka vijana wao katika vyuo ambavyo pamoja na kupata usajili lakini masomo yanayotolewa yanakosa ithibati ya kufundishwa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...