Na  Bashir  Yakub.
Kisheria  ndoa inapokuwa  imefungwa   kuna  haki  za  msingi  ambazo  huibuka. 

 Hizi  huitwa  haki  za  moja  kwa  moja  ( automatic  right). Huitwa  haki  za  moja  kwa  moja   kwakuwa   hazina  uhiari  katika  kutekelezwa  kwake.  Kuwapo  kwa  ndoa  ndio  kuwapo  kwake  na  hivyo  haihitaji  mtu  kuziomba. Kimsingi  haki  hizi  zipo  nyingi  ambapo  tutaona  baadhi  yake hapa   huku  makala  yakijikita  katika   haki  moja ya  matunzo  kwa  wanandoa.

1.BAADHI  YA  HAKI  ZINAZOIBULIWA  NA  NDOA.
( a ) Haki  ya  tendo  la  ndoa.  Hii  ni  haki  ya  lazima  kwa  wanandoa  na  kutokuwepo  kwake  kunaweza  kubatilisha  ndoa iwapo  mmoja  wa  wanandoa ataamua  kufanya  hivyo. Ni  haki  ambayo  huchukuliwa  kama  ndio ndoa yenyewe  na  hivyo  kuifanya  kuwa  na  umuhimu wa pekee.

( b ) Haki  ya  kutumia  jina la mume. Hii   ni haki  aliyonayo  mwanamke  ambapo  anaruhusiwa kutumia  jina  la  mme  wake  badala  ya  lile  la  baba  yake. Hata  hivyo  sheria  haikueleza  iwapo  mwanaume  naye  anaweza  kutumia  jina  la  mke  wake,  au  la  baba  wa  mke  wake, au la  ukoo  wa  mke  wake.  Pia si  tu  mwanamke  ameruhusiwa  kutumia  jina  la  mme  wake  isipokuwa  hata  lile  la  ukoo  wa  mme  wake.

( c ) Haki  ya  kutumia  mali  za  familia  kwa  pamoja. Haijalishi  mali  hizo  ni  mwanamke  mwanaume  ataruhusiwa  kutumia na  haijalishi  mali  hizo ni  za  mwanaume  mwanamke  ataruhusiwa  kutumia. Isipokuwa  yawe  matumizi  ambayo  hayako  kinyume  cha  sheria.

( d ) Haki  ya  kutunza  watoto/mtoto kama  yupo. Ikiwa  familia  imebarikiwa  na  mtoto/watoto basi  wanadoa  kwa  pamoja  wanawajibika  kuwatunza  watoto  hao  kila  mtu kwa  nafasi  yake. Hii  ina  maana mwanamke  anawajibika  zaidi  kuwa  mwangalizi  mkuu wa  kila  siku  wa  watoto  huku  mwanaume  akilazimika  kutoa  matumizi   hasa  yale ya  kifedha.

( e ) Haki  ya  kugawana  mali  pindi  ndoa  inapovunjika. Hii  huhusisha  mali    zote  ambazo  huitwa  mali  za  machumo  ya  pamoja  baina  ya  mwanamke na  mwanaume.

( f ) Pia  ipo  haki  ya  kurithi  na  kurithiana  iwapo  kuna  kifo  cha  mmoja  wa  wanandoa. Mwanamke  aweza  kurithi  mali  za  mme  wake  halikadhalika  mwanaume. Hii  huenda  mpaka  kwa  watoto  waliopatikana  katika  ndoa  ambapo   huweza  kurithi  mali  za  baba, mama  au  wote  wawili.

( g ) Haki  ya  matunzo  baina  ya  wanandoa.  Hii  ndiyo  itakayojadiliwa  japo  kwa  ufupi .

2.  MWANAUME  KUMTUNZA  MWANAMKE.
Sura  ya  29  ya  Sheria  ya  ndoa  kifungu  cha  63 ( a )  kinasema  kuwa  ni  wajibu  wa  kila  mwanaume  kumtumza  mke/wake zake  kutokana  na  njia  za  kipato  chake.  Neno  njia  za kipato  chake  maana  yake  ni  namna  anavyopata   kipato  ndivyo  atavyotakiwa  kutoa  matunzo  kwa  mwanamke.  Haiwi  kuwa  mwanaume  anapata  kipato  kidogo  halafu  alazimishwe  kutoa   matunzo  makubwa.  Ushahidi  wa  namna  anavyopata  kipato  chake  ndio  utakaoainisha  kiasi  cha  matunzo  kwa  mke  wake.

Aidha kwa  mujibu  wa  kifungu  hicho  matunzo  yanayoongelewa  hapa  yanahusisha   makazi,  mavazi, chakula  na  huduma  nyingine  kama  za afya  n.k. Kitu  cha  msingi  hapa  ni  kuwa  ni  lazima  kwa  mwanaume  kutoa  vitu  hivi  kwa mke  wake.

3.  MWANAMKE  KUMTUNZA  MWANAUME.
Kifungu  hichohicho  cha  63 ( b ) kinasema  kuwa  utakuwa  ni  wajibu  wa  kila  mwanamke  lakini  mwenye  uwezo  kutoa  matunzo  kwa   mume  wake  iwapo  mume  huyo  ana  ulemavu/hajiwezi  jumla  au  sehemu  ya  mwili  wake, kiakili  au  kimwili  na  hivyo  kutokuwa  na  uwezo  wa  kuingiza  kipato  kutokana  na  hali  hiyo.

Kwa  kifungu  hiki  tunaona  kuwa mwanamke  anao  wajibu  wa  kumtunza  mume  wake   lakini  iwapo  tu kwanza  ana  uwezo, pili mwanaume  awe  na  tatizo  ambalo  kwalo  hawezi  kuingiza  kipato  na  tatizo  hilo  liwe la  kimwili  au  kiakili. Kumbe  basi  tunaona  kuwa mwanaume  kumhudumia  mwanamke ni  lazima  hata  mwanamke  awe  mzima  wa  afya  huku   hafanyi  kazi  wakati  mwanamke  kumhudumia  mwanaume  ni  pale  tu  atapokuwa  ana  tatizo  ambalo  linamfanya  asiweze  kufanya  kazi. Lakini  pia  sheria  imesema  mwanamke  atatoa  huduma  iwapo  ana  uwezo wakati  neno  iwapo  ana  uwezo  haikuliwekwa  kwa  mwanaume.Kwa mwanaume  kutoa  ni  kutoa  tu.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.    0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...