TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za rambirambi kuombeleza kifo cha mwanasiasa mkongwe na aliyekuwa mbunge wa muda mrefu wa Jimbo la Mafia, Mkoa wa Pwani, Kanali (mst) Ayubu Shomari  Mohamed Kimbau, ambaye aliaga dunia asubuhi ya leo,  Jumapili, Agosti 30, 2015 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam. 
Katika salamu za rambirambi alizomtumia Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Eng. Evarist Ndikilo, Rais Kikwete ameeleza kusikitishwa kwake na taarifa za kifo cha Mzee Kimbau ambaye kwa miaka mingi alikuwa Mbunge wa Jimbo la Mafia kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM). 
Amesema Rais Kikwete katika salamu zake: “Nimesikitishwa na taarifa za kuaga dunia kwa Mzee Ayubu Kimbau ambaye nimejulishwa kuwa amefariki asubuhi ya leo katika Hospitali ya Muhimbili. Mzee Kimbau atakumbukwa sana kwa utumishi wake wa umma na uzalendo wake kwa taifa lake kuanzia alipokuwa katika Jeshi  la  Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambako alipanda nafasi hadi kufikia cheo cha Kanali na baadaye katika uwakilishi wa wananchi wa Mafia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.” 
“Kupitia kwako, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, naungana na wananchi wote wa Mafia na wa mkoa wa Pwani kuomboleza kifo cha mmoja wa magwiji wa siasa na wauwakilishi wa wananchi katika nchi yetu. Nawaombeni mpokee salamu zangu za dhati ya moyo wangu katika kuomboleza kifo hiki,” amesema Rais Kikwete na kuongeza: 
“Aidha, kupitia kwako naitumia familia ya Kanali Kimbau salamu zangu nyingi za pole. Wajulishe kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa na kuwa msiba wao ni msiba wangu. Naelewa machungu yao katika kipindi hiki kigumu na nawaombea kwa Mwenyezi Mungu aweze kuwapa nguvu, uvumilivu na subira. Naungana nao pia kumwomba Mungu aiweke peponi roho ya Marehemu Kanali Ayubu Shomari  Mohamed Kimbau. Amen.”

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

30 Agosti, 2015

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...