A; KIKAO KAMATI YA UTENDAJI
KAMATI ya Utendaji ya Chama cha
Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), inatarajiwa kukutana Ijumaa
Agosti 7, 2015, Dar es Salaam kujadili masuala mbalimbali yahusiyo michezo na
waandishi wa habari za michezo hapa nchini.
Pamoja na mambo mengine, kikao hicho
kitajadili namna bora ambayo chama kinaweza kushiriki kwa kuangalia jinsi ya
kuwaunganisha wanamichezo kwa namna mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu wa Rais,
Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu kwa maslahi ya michezo
nchini.
Moja ya madhumuni ya TASWA wakati inaanzishwa ni kuwaunganisha waandishi wa habari za michezo nchini, kushirikiana katika kukuza na kupromoti michezo na wanamichezo kwa njia ya kalamu na njia nyingine za kupashana habari.
Kwa msingi huo tunaamini kikao
kitatoa muongozo mzuri, ambao unaweza ukasaidia wanamichezo hapa nchini
kufahamu sera za michezo kwa wagombea mbalimbali na hivyo kufanya uamuzi sahihi
wakati ukifika.
Pia kikao kinatarajiwa kufanya
uteuzi wa washiriki wa semina mbili zinazotarajiwa kufanyika hivi karibuni, zikihusisha
waandishi wa habari za michezo wa kada ya kati na wale wazoefu.
Tunaamini tumetoka mbali na tunajua
safari yetu ya kuchangia kukuza michezo nchini bado ni ndefu na ina mabonde,
mabwawa na utelezi. Sisi hatujiulizi ,
Jee tutafika? Bali hujiambia juhudi zetu zitatufikisha tunapotaka
kufika.
B; PONGEZI AZAM
Tunatoa pongezi kwa timu ya soka ya
Azam FC kwa kuibuka bingwa wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati
‘Kombe la Kagame’ mwaka 2015.
Tunaungana na Watanzania wengine
katika kufurahia ubingwa huu, baada ya Jumapili Azam kuifunga Gor Mahia ya
Kenya mabao 2-0 katika mchezo wa fainali Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, hivyo
tunawaomba wachezaji watumie ubingwa wa Kagame kama changamoto ya kufanya
vizuri katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF) mwakani.
Azam wasibweteke na kuona tayari
wamemaliza kazi, bali waendelee na jitihada za kutafuta mafanikio makubwa
zaidi.
C: UTOAJI WA VITAMBULISHO
TASWA ilisitisha kutoa vitambulisho
vipya kwa wanachama wake kwa muda kwa sababu ilikuwa ikifanya utaratibu wa
kubadili vile vya awali na kuwa na vitambulisho vya kisasa zaidi, ambapo suala
hilo lipo hatua za mwisho kukamilika na hivi karibuni wanachama wote wapya
watapatiwa vitambulisho vyao.
Nawasilisha,
Amir Mhando,
Katibu Mkuu TASWA
05/08/2015
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...