TAARIFA YA KAMATI YA UTENDAJI
Kikao cha Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kilichokutana leo kimepitia na kutoa maamuzi yafuatayo:

(i)           Kila mkoa utakua na kituo cha kukuza na kuendeleza vipaji vya watoto (Regional Sports Centre). Mapato ya mchezo wa Ngao ya Hisani msimu huu yatatumika kuagiza kontena la vifaa (mipira size 3, 4, bips na cones) ambavyo vitasambazwa katika vituo vyote vya michezo vya mikoa.

(ii)         Ubovu wa viwanja – Kamati ya Utendaji imeiagiza sekretariat kuwaandikia barua wamiliki wa viwanja vyenye mapungufu, kufanyia kazi marekebisho hayo haraka kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi nchini. Kiwanja ambacho hakitafanyiwa marekebisho hakitatumika kwa michezo ya ligi msimu huu.

(iii)       Twiga Stars – Timu ya Taifa ya Wanawake ya mpira wa miguu nchini Tanzania (Twiga Stars) inatarajiwa kuingia kambini tarehe 04 Agosti kisiwani Zanzibar kwa gharama za TFF kujiandaa na Fainali za Michezo ya Afrika (All Africa Games) zitakazofanyika nchini Congo Brazaville mwezi Septemba mwaka huu. Aidha Kamati ya Utendaji imeiagiza sekretariet kuwasiliana na Kamati ya Olympic nchini (TOC) kuweza kujua mchango wao katika maandilizi hayo ya michezo ya Afrika.

(iv)        Kamati ya Utendaji imeipongeza Kamati ya ndani ya Uendeshaji wa Michuano ya Kombe la Kagame (LOC) kwa kuandaa michuano hiyo vizuri kuanzia mwanzo mpaka sasa inapoelekea mwishoni kesho kwa mchezo wa Fainali.  Aidha Kamati inaipongeza klabu ya Azam FC kwa kufika hatua ya fainali ya michuano hiyo na kuitakia kila la kheri katika mchezo wa kesho ili iweze kulibakisha kombe hilo nyumbani. Kamati hiyo pia imeipongeza klabu ya Yanga kwa kufika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

(v)          Aidha Kamati ya utendaji imeiagiza sekretariat kuandika barua kwenda kwa uongozi wa CECAFA juu ya masikitiko na mapungufu yaliyoenekana katika michuano hiyo. Timu ya Gor Mahia pamoja na washabiki wake wamekuwa wakifanya vitendo vya utovu wa nidhamu huku CECAFA ikiwatazama pasipo kuwapa adhabu yoyote.

(vi)        Kikao hicho cha Kamati ya Utendaji pia kimepitia na kupitisha mapendekezo ya rasimu ya kanuni za uendeshaji wa Bodi ya ligi nchini (TPLB), yaliyowasilishwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za Wachezaji Wakili, Idd Mandi.

 FAINALI KAGAME KIINGILIO  BUKU TATU
Michuano ya Vilabu Bingwa kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup) inatarajiwa kufika tamati kesho jumapili katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kwa mchezo wa Fainali utakaozikutanisha timu ya Azam FC dhidi ya Gor Mahia. 
Viingilio vingine vya mchezo huo wa kesho wa fainali ke ni VIP A ni shilingi elfu kuni na tano (15,000) na VIP B & C, Shilingi elfu kumi (10,000) na sehemu nyingine ya uwanja  iliyobakia ni shilingi elfu tatu (3,000) kwa viti vya rangi ya bluu, kijani na rangi ya chungwa. 
Katika mchezo wa nusu fainali uliofanyika jana, Gor Mahia iliweza kuibuka na ushindi wa mabao 3- 1 dhidi ya Khartoum mabao yaliyofungwa na Michael Olunga, Innocent Wafula na Kagere Meddie na kukata tiketi ya kucheza fainali. 
Gor Mahia chini ya kocha wake Frank Nuttal mpaka kufikia hatua ya fainali, imecheza jumla ya michezo sita, ikiwemo michezo minne katika hatua ya makundi, robo fainali na nusu fainali, ambapo imeweza kushinda michezo mitano na kutoka sare mchezo mmoja. 
Mshambuliaji wa Gor Mahia,Michael Olunga anaongoza kwa ufungaji, akiwa amepachika mabao matano, akifuatiwa na nahodha wa Khartoum Salehdin Osman na msadizi wake Amin Ibrahim wote wenye mabao manne kila mmoja.

Kwa uapnde wa Azam chini ya kocha wake Stewart Hall, imefanikiwa kufika hatua ya fainali bila ya kuruhusu nyavu zake kutikisika, huku safu yake ya ushambuliaji ikiwa imepachika mabao tisa (9) katika michezo mitano iliyocheza kuanzia hatua ya makundi. 
Kuelekea mchezo wa Fainali, Azam FC iliziondosha Yanga SC kwa mikwaju ya penati (5-4) hatua ya robo fainali, na kasha kuindoa KCCA hatua ya nusu fainali kwa kuifunga kwa bao 1- 0, bao lililofungwa na mshambuliaji chipukizi Farid Musa.
Mshambuliaji Kipre Tchetche ana mabao matatu kwa upande wa washambuliaji wa Azam FC, akifuatiwa na nahodha John Bocco na Farid Musa wenye mabao mawili kila mmoja.

Katika fainali hiyo ya kesho, inatarajiwa kuwa ya vuta ni kuvute kutokana na makocha wa timu hizo, Frank Nuttal wa Gor Mahia kutaka kushinda taji hilo kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 tangu Gor Mahia kushinda kombe hilo mara ya mwisho mwaka 1985 walipotwaa kwa mara ya tano (5). 
Huku Stewart Hall akiwania kuweka historia ya kwanza kwa klabu ya Azam FC kuweza kutwaa kombe hilo kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo miaka tisa iliyopita, baada ya kusindwa kutwaa taji hilo ilipotinga fainali mwaka 2012 kwa kufungwa na Yanga SC mabao 2-0.

Mchezo huo wa fainali unatarajiwa kuanza saa 9:45  alasiri kwa saa za Afrika Mashariki, huku mchezo wa kusaka mshindi wa tatu ukitarajiwa kuanza saa 7:30 mchana ukizikutanisha timu za Khartoum ya Sudan dhidi ya KCCA kutoka nchini Uganda. 
Bingwa wa michuano hiyo atazawadiwa kitita cha Dola za Kimarekani Elfu Thelathini (U$ 30,000), mshindi wa pili Dola za Kimarekani Elfu Ishirini (U$ 20,000) huku mshindi wa tatu akizawadiwa Dola za Kimarekani Elfu Kumi (U$ 10,000).

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi nchini Mkoa wa Temeke, linawashikilia watu watatu kutoka nchini Kenya kufuatia kufanya kosa la shambulio katika mchezo wa nusu wa fainali kati ya Gor Mahia dhidi ya Khartoum katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam. 
Raia hao wa Kenya walifanya shambulio kwa mlinzi wa TFF uwanja wa Taifa, Omary Mayai wakiwa katika jukwaa la VIP A ambapo askari polisi walijaribu kuwaonya na kuwaomba kuwa wastaarabu, lakini walishidwa kutii amri ya polisi na kuendelea kufanya vurugu kabla ya mmoja wao kukimbilia ndani ya uwanja na kuketi katika benchi la ufundi la Gor Mahia. 
Namba ya jarada la kesi iliyofunguliwa kituo cha Polisi cha Chang’ombe ni CHA/RB6265/2015, na wanaoshikiliwa kituoni hapo ni mshabiki wa Gor Mahia Jackson Mjidie (Jaro Soja), pamoja na waandishi wa habari wawili kutoka kituo cha Citizen, Okinyi Mike na Jariri Otieno.
  
DIRISHA LA USAJILI KUFUNGWA AGOSTI 6
Dirisha la Usajili kwa Vilabu vya Ligi Kuu (VPL), Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na Ligi Daraja la Pili (RCL) linatarajiwa kufungwa tarehe 06 Agosti, 2015. 
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) linavikumbusha vilabu vyote kufanya usajili wa wachezaji wao mapema kabla ya kufungwa kwa dirisha hilo, ili kuondokana na usumbufu wa kufanya usajili dakika za mwisho. 
Pindi dirisha hilo litakapofungwa Agosti 06, hakuna klabu au timu yoyote itakayoweza kufanya tena usajili wake, hivyo ni vyema vilabu vitahakikisha vinamaliza mausala ya usajili mapema kabla ya siku ya mwisho.
  
U15 KUJIPIMA LEO ZANZIBAR
Kikosi cha timu ya Taifa cha vijana wenye umri chini ya miaka 15 (U-15) leo kinatarajiwa kushuka dimbani kisiwani Zanzibar kucheza michezo wa kirafiki na kombani ya kisiwani humo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika mwaka 2017. 
Timu ya vijana ya Taifa wenye umri chini ya miaka 15 (U15) imekua ikiingia kambini kila mwisho wa mwezi kwa ajili ya kucheza michezo ya kirafiki ya kujipima nguvu, na kocha kupata nafasi ya kuona maendeleo ya vijana na kuongeza wachezaji wengine wanaonekana katika kuboresha kikosi hicho. 
Kikosi hicho cha Vijana cha U-15 kilichopo chini ya kocha mzawa Bakari Shime, kinajumuisha wachezaji 22 waliopo kambini, na kinatarajiwa kucheza michezo miwili kisiwani Zanzibari leo jumamosi na jumapili, kabla ya kurejea jijini Dar es salaam.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA 
MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...