Na Aron Msigwa 
 Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kuwatumia wahandisi wazalendo waliosajiliwa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kutekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu katika maeneo mbalimbali nchini. 
 Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya Wahandisi kwa mwaka 2015 jana  jijini Dar es salaam, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema kuwa Wahandisi wanao mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi kwa kuifanya mipango iliyo kwenye karatasi kuwa katika uhalisia unaoonekana kwa macho. 
 Amesema fani ya uhandisi inagusa maisha ya watu moja kwa moja hasa sekta ya ujenzi wa miundombinu ya maji, umeme, majengo,miundombinu ya migodi, hospitali, barabara, viwanda na shughuli nyingine za kihandisi. 
 "Ni jambo lililowazi kuwa tuna kila sababu ya kujivunia maendeleo na mafanikio tuliyofikia, tuna kila sababu ya kuwatumia na kutoa kipaumbele kwa wahandisi wazalendo ,wahandisi wetu wanaweza" Amesisitiza Balozi Sefue. 
 Amewataka wahandisi hao kuendelea kuzingatia weledi pindi wanaposimamia utekelezaji wa miradi ya Serikali ili miradi hiyo iendane na thamani halisi ya fedha za wananchi kwa kuwa Serikali inatumia fedha nyingi kugharamia miradi hiyo. 
 "Nawataka muendelee kuzingatia weledi,muwe waadilifu na mfanye kazi kwa bidii ili tufikie malengo ya Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025,mkumbuke kuwa kazi mnazofanya zinaonekana na watu wote, zikiwa mbaya au kuwa chini ya viwango watasema tu na mtaonekana hamzingatii taaluma wala viapo vyenu" Amesisitiza. 
 Amesema toka mwaka 2005 hadi 2015 Sekta ya Uhandisi nchini Tanzania imeweza kuwanufaisha watanzania kwa kuzalisha ajira 256,480 na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira mzauri kwa kuboresha shule , vyuo na taasisi mbalimbali ili ziweze kuzalisha wahitimu bora wenye kuhimili ushindani soko. 
 Aidha, ameziagiza Halmashauri kote nchini kuhakikisha kuwa zinakuwa na wahandisi waliosajiliwa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi kabla ya Juni 30, 2016 na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kuweka msisitizo katika ubora wa wahandisi wa ndani na nje ya nchi pamoja na kuimarisha ushirikiano uliopo katika sekta ya ujenzi baina Tanzania na nchi za jirani. 
 Awali akiongea kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kuongea na washiriki wa maadhimisho hayo Naibu Katibu Mkuu,Wizara ya Ujenzi, Muhandisi Joseph Nyamhanga, amesema kuwa siku hiyo inatoa fursa kwa wahandisi kote nchini kukutana na kubadilishana uzoefu wa kitaalam katika kuleta maendeleo nchini. 
 Amesema Bodi ya Usajili wa Wahandisi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imewezesha kufanyika kwa maadhimisho hayo nchini Tanzania lengo kubwa likiwa ni kuweka msukumo na msisitizo wa kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa 2015, kuangalia changamoto na mikakati ya kukabiliana nzao. 
 Ameongeza kuwa mkutano huo wa mwaka unafanyika nchini Tanzania kwa mara ya 13 ukizishirikisha baadhi ya nchi za Afrika zikiwemo Nigeria,Afrika kusini,Malawi, Kenya na wawakilishi kutoka Norway.
 Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akizungumza na Wahandisi kutoka maeneo mbalimbali nchini wakati wa ufunguzi wa Siku ya Wahandisi nchini mwaka 2015 jijini Dar es salaam.
 Baadhi ya Wahandisi wahitimu kutoka katika vyuo na taasisi mbalimbali wakiapa kiapo cha utii kwa Taaluma yao mbele ya Kamishna wa Viapo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wahandisi yanayoendelea jijini Dar es salaam.
 Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akikabidhi vyeti na miongozo mbalimbali ya utendaji wa kazi kwa Wahandisi baada ya kuapishwa   jijini Dar es salaam
 Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akikabidhi vyeti na miongozo mbalimbali ya utendaji wa kazi kwa Wahandisi baada ya kuapishwa  jijini Dar es salaam
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi nchini Tanzania (ERB) Mara baada ya ufunguzi wa Siku ya Wahandisi 2015 leo  jijini Dar es salaam. 
Picha na Lorietha Laurence Maelezo)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Waandisi wazalendo watumike vizuri kuendeleza nchi hii mijini na katika wilaya zote azi zao wasipewe wababaishaji.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...