JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA

Simu: 255-22-2114615, 211906-12
Barua pepe: nje@nje.go.tz
Barua pepe: gcu@nje.go.tz

Nukushi: 255-22-2116600

              

 


                20 KIVUKONI FRONT,
                           P.O. BOX 9000,
                  11466 DAR ES SALAAM, 
                                    Tanzania.

 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
  
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kufariki kwa Mahujaji zaidi ya 700 na wengine zaidi ya 800 kujeruhiwa wakati wakishiriki ibada ya Hijja iliyofanyika Makkah, Saudi Arabia tarehe 24 Septemba, 2015.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ubalozi wa Tanzania, Saudi Arabia
Mahujaji hao walifariki na kujeruhiwa kutokana na msongamano mkubwa wa watu uliotokea kwenye eneo la Mina.

Aidha, taarifa hizo zinaeleza kuwa hadi sasa Mahujaji wapatao watano (5) kutoka Tanzania wamefariki dunia na wengine kujeruhiwa. Majina ya Watanzania waliofariki na kutambuliwa ni Bi. Mwanaisha Hassan Juma, Mkungwe Suleiman Hemedi na Sefu Saidi Kitimla. Mtu mwingine aliyefariki ni Raia wa Kenya anayeishi nchini ambaye ametambulika kwa jina la Bi. Fatuma Mohammed Jama.

Ubalozi unaendelea na jitihada za kupata jina la Mtanzania mwingine aliyefariki kwenye tukio hilo. Aidha, Serikali ya Saudia imetangaza kuwa itatoa taarifa kamili ikiwemo idadi ya watu waliofariki na majeruhi na nchi wanazotoka mara itakapokamilika.

Pia Ubalozi wetu kwa kushirikiana na Taasisi zinazoshughulikia masuala ya Hijja za Tanzania ikiwemo BAKWATA pamoja na Mamlaka za Serikali ya Saudi Arabia unaendelea kufuatilia kwa karibu ili kujua endapo kuna vifo na majeruhi wengine kutoka Tanzania.

Hivyo basi, Wananchi wanaombwa kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu wakati Serikali ikiendelea kufuatilia.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es Salaam
25 Septemba, 2015

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Ankal

    Kwetu wanadamu, huu ni msiba mkubwa sana. Lakini Mungu ndiye anafahamu njia zake. Tumtegemee wakati huu wa majonzi.

    Nilifundishwa katika dini yangu ya Katoliki kwamba tukifa katika mazingira kama haya, ambapo tunakuwa tumejitakasa kiroho, ni kifo chema. Kwa msingi wa imani hii, na kwa kuzingatia kuwa hao mahujaji walikuwa katika hali safi kiroho, wameenda kwenye mapumziko ya milele mbinguni. Hii ni faraja. Iwe faraja kwa wafiwa na wengine.

    Papo hapo, wakati huu wa majonzi, zimejitokeza taarifa kuwa kiongozi mmoja huko Saudia amewalaumu wa-Afrika kwa tukio hili la kusikitisha. Kama taarifa hizo ni kweli, sioni busara yake, hasa kwa kipindi hiki kigumu:

    http://howafrica.com/saudi-prince-blames-black-africans-for-hajj-stampede-717-dead-so-far/

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...