WIZARA ya Afya na
Ustawi wa Jamii imeiagiza Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali
kufuatilia matumizi ya sigara ya kiko ya maji (Shisha) katika kumbi za starehe za hapa nchini kwa kuwa sigara hizo zinahusishwa
na matumizi ya madawa ya kulevya.
Akizungumza katika hafla
ya utoaji tuzo kwa wanafunzi na walimu bora wa masomo ya kemia na biolojia kwa
mwaka 2013-2014 iliyofanyika leo Ijumaa (Septemba 18, 2015), Katibu Mkuu wa
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt
Donan Mmbando alisema hatua hiyo ni mkakati wa serikali wa kudhibiti matumizi
ya dawa za kulevya nchini.
Dkt Mmbando alisema Wizara kupitia Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu
wa Serikali inatoa mchango mkubwa wa uchunguzi wa kimaabara kuweza kutambua
dawa za kulevya na pia kuwatambua waathirika wa dawa hizo.
“Serikali inatambua
umuhimu na unyeti wa kazi zinazofanywa na wakala wa maabara na mkemia mkuu wa
serikali katika kulinda afya na usalama wa watu na mazingira pamoja na kuleta
uelewano katika jamii” alisema Dkt Mmbando.
Aidha alisema serikali itaendelea kuitegemea Taasisi hususani katika utaalamu kwa utatuzi wa
masuala yanayohusiana na kulinda afya na usalama wa jamii, hivyo itahakikisha
inaiwezesha taasisi hiyo katika mahitaji ya rasilimalli watu na fedha.
Aidha Dkt Mmbando aliwapongeza
walimu na wanafunzi wote waliofanya vyema katika mitihani yao na kuwakumbusha
juu ya madhara ya matumizi ya dawa za kulevya ambayo yanaweza kufuta ndoto ya
kuwa nguvu kazi ya taifa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...