Mwakilishi wa  Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, akizungumza  siku ya Alhamis Usiku, muda mfupi  kabla ya  kuonyeshwa kwa filamu ya "the Boy from Geita" ambayo inaelezea uovu wanaotendewa watu wenye ulemavu hususani watoto Nchi Tanzania. Katibu Mkuu  Msaidizi wa ofisi ya Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa,  Bw.  Ivan Simonvic wapili kutoka kushoto alitambua mchango wa serikali katika kuukabili uovu dhidi ya  watu wenye ulemavu wa ngozi   na akahidi  Taasisi hiyo na  nyingine za Umoja wa Mataifa  ushurikiano na  Serikali. wa Kwanza ni  Bw. Peter Ash mwanzilishi na Mkurugenzi wa  Asasi ya  Unter the Same Sun na  karibu na Balozi  ni  mwakilishi kutoka Uwakilishi wa Kudumu wa Canada katika  Umoja wa Mataifa
Sehemu wa wageni  waalikwa  waliofika kuangalia filamu ya "the Boy from Geita" iliyonyeshwa Alhamisi usiku hapa  Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa. 

Na  Mwandishi Maalum, New York
SIKU moja  baada ya  Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kuelezea kwa waandishi wa habari juhudi zinazofanywa na serikali dhidi  uovu wanaofanyiwa  watu wenye  ulemavu wa ngozi.

Kamisheni  ya   Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (UNHR ) imesema itashirikiana na  Serikali ya Tanzania katika  juhudi hizo   za kuukabili  ouovu  unaofanywa dhidi ya  jamii  hiyo ya watanzania.

Kauli hiyo  imetolewa Alhamisi  usiku   na   Katibu Mkuu Msaidizi wa Ofisi ya Kamisheni ya Haki za  Binadamu, Bw.  Ivan Simonovic   muda mfupi kabla ya kuonyeshwa kwa filamu ya “ the Boy from Geita”.

Bw. Ivan Simonovic  amesema,  ushirikiano huo ni katika kutambua juhudi zinazofanywa na  serikali katika siyo  tu  kwa kuhakikisha tatizo hilo linatoweka lakini pia kwa kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaohusika  na ukatili huo.

“Tofauti na  nchi nyingine,  Serikali ya Tanzania imeonyesha ujasiri na uthubutu  wa kukabiliana na uovu unaofanywa dhidi ya watu wenye ualibino. Ni  kwa kutambua juhudi hizo  tutashirikiana  na serikali katika kukomesha  uovu huu” akasema Bw. Simonovic.

Kauli ya  Bw. Ivan Simonovic ya kutambua juhudi hizo za serikali,  kumetokana na  shuttle diplomacy iliyofanywa na  Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania, Balozi Tuvako  Manongi ya kuonana na  wakuu wa Idara ambazo zimefadhili  kuonyeshwa kwa filamu hiyo hapa Umoja wa Mataifa,   pasipo kuushirikisha  wala  kuujulisha  Uwakilishi  wa Tanzania.

Aidha  maelezo ya awali kuhusu  filamu hiyo  yanaupotoshaji wa baadhi ya mambo  hali iliyomfanya Mwakilishi huyo wa Tanzania katika  Umoj wa Mataifa kuchukua  fursa ya  kuyatolea ufafanuzi.

“Usiku huu   ninapenda kutambua juhudi zinazofanywa na  Moja ya nchi Mwanachama  wa Umoja wa Mataifa, Tanzania, ambayo Mwakilishi wake  Wakudumu Balozi Tuvako  Manongi  yupo  pamoja  nasi.  Siyo tu kwamba  Tanzania imeonyesha  ujasiri na uthubutu wa kutambua ukubwa wa  tatizo linalowakumba watu wenye  ualibino   lakini  pia  imefanya juhudi za kuwaelimisha wananchi wake huku ikuchukua hatua muhimu” akasema Bw. Ivan Simonovic.

Akaeleza zaidi kwamba  kama watakavyoona kwenye   filamu hiyo. Waziri Mkuu  wa Tanzania  Mhe. Mizengo  Pinda amekuwa msemaji  na  mtetezi wa haki za watu wenye ualibino  kwa kufanya  ziara za kutembelea maeneo mbalimbali ya nchi kuhimiza   na  kuelimisha wananchi kuachana na  ukatili huo.

“Kujituma kwake  na namna anavyolichukulia tatizo hili kwa uzito wa aina yake,  ni ushahidi wa namna  gani Tanzania  inavyokabiliana na changatomo hii.  juhudi hizi zimeleta matokeo chanya ambapo    hakuta taarifa za matukio ya kuvamiwa watu wenye ualibino  katika miezi ya hivi karibuni.

 “ Ofisi ya Haki za Binadamu inakaribisha na kutambua juhudi hizo za serikali ya Tanzania katika kukabiliana na Ubaguzi. Mfumo mzima wa Umoja wa  mataifa upo tayari kuwaunga mkono” akasema  katibu Mkuu  Msaidizi.

Alipopewa  nafasi ya kuzumgumza mbele ya  hadhara hiyo. Balozi Tuvako Manongi   kwanza,  alimshukuru Katibu Mkuu  Msaidizi kwa kutambua mchango wa serikali,  na pia kumpatia fursa ya kuja kuzungumza na kutoa fafanuzi kwa niaba ya serikali yake.

Balozi Manongi, alirejea kauli  aliyoitoa mbele ya  waandishi siku ya jumatano, kwamba, Tanzania  haikatai na wala haipingi kwamba kuna tatizo kwa  watu wenye ualibino.

Akasema  pamoja na kukiri kuwapo  kwa matukio  ya uovu dhidi ya watanzania hao, lakini  angependa pia kuweka rekodi sawa  na hasa kufuatia  maelezo  ya upotoshaji ambayo yametolewa kwenye vipeperushi vinavyoitangaza filamu hiyo.

Baadhi ya mambo ambayo Balozi  ameyatolea ufafanuzi  ni lile linaloelezwa  na waandaji wa filamu  hiyo  kuwa  eti  ualibino  ualianzia Tanzania  miaka 2000 iliyopita  jambo analosema    halijathibitishwa kisayansi.

 Akafafanua pia kwamba,  Watanzania ni waumini wa dini ya kiislamu au wakristo , kwa hiyo kusema   kuwa sehemu kubwa ya watanzania wanaamini katika uchawi halina mashiko. 

Akasema kwamba si  sahihi pia kueleza kwamba wazazi ni washirika katika kutenda  maovu dhidi ya watoto wao wenye ualibino.  Amefafanua pia kuwa neno zeruzeru ni tafsri ya  Kiswahili ya neno alibino na kwamba tafsri inayotolewa na waandaji hao ni  upotoshaji.
Balozi Manongi  pia amekanusha  taarifa zilizoelezwa na waandaji hao kwamba Asasi ya Under the Same Sun, ilipokuja Tanzania mwaka 2007  haikukuta  chama chochote cha kuwasema watu wenye ualibino si  kweli. Kwani  chama cha Tanzania Albinism Society ( TAS) kimekuwapo tangu mwaka 1978 na kimekuwa kikiendesha shuguli zake kwa kushirikiana na serikali.

“ Mashambulizi dhidi ya watu wenye ualibino nchini Tanzania,  ni  makosa ya jinai, yanayofanywa na watu  binafsi ambao wamejawa na mawazo  uovu ambayo yanaweza tu kuthibitishwa na vyombo yha sheria” akasisitiza Balozi.

Na kuongea kwamba  Tanzania inaheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria na kwa kuheshimu  huko  haiwezi kutoa hukumu kiholela  bila ya kufuata mkondo wa sheria.

Akifafanua Zaidi kwa takwimu Balozi Manongi amesema  watu bilioni moja au Zaidi wenye aina mbalimbali za ulemavu, asilimia 80 wanatoka  nchi zinazoendelea. Na kwamba kwa mujibu wa sensa ya watu iliyofanyika  nchini, watu  2.6  milioni sawa na asilimia 5.8 ya idadi yote ya watu wana aina moja ama nyingine ya ulemavu. Kati yao 16,477 au 0.04 asilimia wana ualibino.

Wakati wa kipindi cha majibu na maswali baadhi ya  watizamaji walihoji sababu ya waandaji wa filamu hiyo kuionyesha  Marekani ili hali kwamba katika  Marekani yenyewe  pia  kuna vitendo  vya  ubaguzi   wa hali ya juu yakiwamo matukio ya watu  kuuwa.

Wengine walitaka kujua ni watu gani wanaonunua viungo vya watu wenye ualibino  swali lililojibiwa na waandaji wa filamu hiyo kuwa ni   ni matajiri  wakiwamo wanasiasa  kiuhalifu. Wakasema pia kwamba  ni watanzania wachache ambao bado wanaimani potofu dhidi ya watu wenye ualibino, huku wakibainisha  uhuru wa vyombo vya habari nchi Tanzania imechangia kwa kiasi kikubwa  kufahamika kwa madhila wanayofanyiwa watu wenye  ualubino.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...