Makamu wa Pili wa  Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa ufafanuzi juu ya taarifa za vyombo mbalimbali vya habari
Wanahabari  wanapaswa kuwa makini zaidi katika utoaji wa Habari zao hasa kipindi hichi ambacho  Zanzibar  inaendelea kutafuta  njia muwafaka ya hatma yake ya baadaye kufuatia Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar { ZEC } kufuta  Uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba mwaka huu baada ya kubaini hitilafu kadhaa katika zoezi zima la uchaguzi.
Nasaha hizo zimetolewa na Makamu wa Pili wa  Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar  alipotoa ufafanuzi wa kina juu ya taarifa zilizotolewa na  baadhi ya vyombo vya Habari vikieleza kuwa Viongozi wanaokutana kujadili suala hilo wamekubaliana kurudiwa kwa uchaguzi huo.
Alisema Kalamu za waandishi wa Habari kwa sasa ni vyema zikawaelekeza na kuwaongoza Wananchi kujihusisha na harakati zao za kimaisha badala ya kuwaendeleza katika wimbi la mizozano na mifarakano inayoweza kuamsha  hamasa.
Balozi Seif akiongea na Redio ya Kiswahili ya Kimataifa ya Ufaransa { RFI } juzi alichokisema kuwaeleza wanahabari hao ni kwamba Chama cha Mapinduzi            { CCM } pekee ndicho kilichotamka na kuthibitisha kuwa kiko tayari kurejea uchaguzi huo endapo utapangwa upya.
“ Nilichokieleza juzi ni kwamba  CCM peeke ndio Tuliothibitisha  na kukubali kurejea uchaguzi endepo utapangwa tena na hili tunaloendelea nalo la vikao na wenzetu bado tunajadiliana na maamuzi ya pamoja yatatolewa kwa Waandishi hapo baadaye “. Alisema Balozi Seif.
Alisema hadi sasa hakuna chombo chochote cha Habari  ndani na nje ya  Nchi kilichoitwa au kupewa Habari za mazungumzo yanayoendelea kati ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein na Katibu Mkuu wa  CUF ambae pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif  Sharif  Hamadi kwa kuwashirikisha Marais wastaafu wa Zanzibar.
Balozi Seif alisema utaratibu maalum utaandaliwa wa kutolewa taarifa rasmi kwa vyombo vyote vya Habari ili ziwafikie Wananchi wote mara baada ya kukamilika kwa mazungumzo  hayo na makubaliano yatakayofikiwa baina  ya pande hizo mbili.
Aliwathibitishia Wananchi na wageni kwamba hali ya Zanzibar bado iko shwari na salama na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  na ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania  kupitia vyombo vyake vya Dola vitasiamia ipasavyo hali hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba Wananchi wabakie kuwa watulivu, wastahamilivu  na kuendeleza Umoja na mshikamano utakaosaidia kulivua Taifa hili katika shari inayoweza kuepukwa.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
27/11/2015

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Anajifurahisha tu huyu hana jipya hapa lamaana mwaka wenu huu tafuteni pakuishi maana kwa Zanzibar utachekwa na mpaka nzi wa hapa soko la darajani

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...