Afisa
Uhusiano Mwandamizi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw.
Salim Shao (kulia) akimkabidhi hundi ya shilingi milioni 15 Meneja Mkuu
wa Kampuni ya Capital Plus International Limited, ambao ni waandaaji wa
mbio za Rock City Marathon, Bw. Erasto Kilawe, jijini Dar es Salaam
jana ikiwa ni udhamini wa mbio hizo zitakazofanyika katika viwanja vya
CCM Kirumba jijini Mwanza tarehe 15 Novemba mwaka huu.
Afisa
Uhusiano Mwandamizi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw.
Salim Shao (kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)
kwenye hafla fupi ya kukabidhi hundi ya shilingi milioni 15 kwa Kampuni
ya Capital Plus International Limited, ambao ni waandaaji wa mbio za
Rock City Marathon, jijini Dar es Salaam jana ikiwa ni udhamini wa mbio
hizo zitakazofanyika katika viwanja vya CCM Kirumba jijini Mwanza tarehe
15 Novemba. Kushoto ni Meneja Mkuu wa Kampuni ya Capital Plus International Limited, Bw. Erasto Kilawe.
Meneja
Mkuu wa Kampuni ya Capital Plus International Limited, ambao ni
waandaaji wa mbio za Rock City Marathon, Bw. Erasto Kilawe (kushoto)
akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kwenye hafla fupi ya
kupokea hundi ya shilingi milioni 15 kutoka Shirika la Taifa la Hifadhi
ya Jamii (NSSF), ikiwa ni udhamini wa mbio hizo zitakazofanyika katika
viwanja vya CCM Kirumba jijini Mwanzana tarehe 15 Novemba mwaka huu.
Kulia ni Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Salim Shao.
NSSF yapiga jeki Rock City Marathon kwa Sh 15M/-
Shirika
la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limetoa shilingi milioni 15
kudhamini mbio za Rock City Marathon mwaka huu, huku waandaaji wa mbio
hizo wakitangaza zawadi za washindi.
Jumla
ya shilingi milioni kumi zimetengwa kushindaniwa katika makundi
mbalimbali ya mbio za mwaka huu zilizopangwa kufanyika Novemba 15
(jumapili hii) katika viwanja vya CCM Kirumba jijini Mwanza.
Akizungumza
wakati wa makabidhiano ya hundi ya shilingi milioni 15 kwa waratibu wa
mbio hizo, Capital Plus International Limited, Afisa uhusiano mwandamizi
wa NSSF, Bw. Salim Shao alisema kuwa NSSF imeendelea kudhamini mbio
hizo kwa mwaka wa saba mfululizo baada ya kuona maboresho yanayofanyika
kila mwaka katika mbio hizo zinazowakutanisha wanariadha kutoka ndani na
nje ya nchi.
“Kwa
upande wetu tunaona ushiriki wetu katika mbio hizi kama fursa ya
kukutana moja kwa moja na wateja wetu lakini pia tutatumia fursa hii
kuwaelezea washiriki juu ya umuhimu wa kujiunga na mfuko wetu ili waweze
kunufaika na huduma za kipekee zinazotolewa na NSSF,” Alisema Bw. Shao.
Mbio
za Rock City Marathon, zinazoandaliwa na Kampuni ya Capital Plus
International (CPI), kwa ushirikiano na Chama cha Riadha Tanzania (RT),
pamoja na Chama cha Riadha Mkoa wa Mwanza (MRAA) zinalenga kutambua na
kuinua vipaji vya wanariadha nchini na pia kukuza utalii wa ndani
kupitia sekta ya michezo.
Meneja
mkuu kutoka kampuni ya Capital Plus International, Bw. Erasto Kilawe,
alisema kuwa udhamini huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kufanikisha hatua
za mwisho za maandalizi ya mbio hizo na baadhi ya fedha hizo zitatumika
kama zawadi kwa washindi wa mbio za mwaka huu.
“Baada
ya kupata udhamini huu, tunafaraja kubwa kutangaza zawadi
watakazopatiwa washindi. Kwa mbio za Kilomita 21, jumla ya shilingi
milioni saba na laki moja zimetengwa kwa ajili ya washindi. Washindi wa
kwanza watazawadiwa Tsh 1.5m/- huku washindi wa pili wakijipatia laki
tisa na washindi wa tatu watapata laki saba kila mmoja.
Kwa
mbio za kilomita tano, zaidi ya shilingi laki nne zimetengwa kwa ajili
ya washindi. Jumla ya shilingi laki tatu na arobaini zimetengwa kwa
ajili ya washindi wa mbio za kilomita 3 na shilingi laki mbili imetengwa
kama zawadi kwa ajili ya mbio za watoto za kilomita mbili.”
Alisema
kuwa kamati ya maandalizi ya mbio za mwaka huu imefanya kazi kubwa ili
kuhakikisha kuwa kiwango cha mbio hizo kinaongezeka ili kuzifanya ziwe
na msisimko zaidi.
“Kwa
namna ya kipekee sana nipende kuwashukuru wadhamini wa mbio za mwaka
huu ambao ni Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Precision Air,
Bodi ya Utalii Tanzania, New Mwanza Hotel na Bank M,” alisema.
Bw. Kilawe alitoa wito kwa wakazi wa jiji la Mwanza na miji jirani kujisajili kwa kuchukua fomu katika uwanja wa Nyamagana.
“Fomu
za ushiriki pia zinapatikana katika ofisi za Kampuni ya Capital Plus
International zilizopo ghorofa ya tatu jengo la ATC, mtaa wa Ohio jijini
Dar es salaam na Uwanja wa Amri Abeid mjini Arusha,” alihitimisha.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...