SERIKALI leo imetoa
ufafanuzi kuhusu upatikanaji wa vibali vya kusafirisha mazao kwenda nje ya nchi
ambapo imesisitiza kuwa vibali hivyo vinapatikana bila gharama na hakuna urasimu wowote.
Akitoa ufafanuzi huo,
Mwanasheria wa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Bwana George Mandepo (Pichani) alisema
kuwa vibali vya kusafirisha mazao ya kilimo nje ya nchi, hutolewa bila gharama
na kuongeza kuwa biashara hiyo inaweza kufanywa na mtu yeyote, kinachotakiwa ni
mhusika kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.
Bwana Mandepo aliongeza
kuwa, uuzaji wa mazao nje ya nchi, unasimamiwa na Sheria ya Usalama wa Chakula iliyofanyiwa
marekebisho mwaka 2009, inayojulikana kama Sheria ya Nafaka na Mazao
Mchanganyiko (Serial and Other Produce Act, 2009) inayompa mamlaka Waziri wa
Kilimo Chakula na Ushirika kutoa kibali cha kuuza mazao nje ya nchi kwa mtu
mwenye vigezo.
Sheria hiyo pia, inampa
mamlaka Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, kukasimu madaraka ya kutoa vibali
kwa Makatibu Tawala wa Mikoa wakati wa dharura kama ilivyokuwa katika msimu wa
kilimo wa 2013/2014 ambapo Taifa lilikuwa na ziada ya kutosha.
Bwana Mandepo aliongeza
kuwa, katika Sheria hiyo inamtaka mfanyabiashara kuainisha aina ya mazao na kiwango ambacho anataka kusafirisha, lengo ni kuhakikisha
kuwa, Serikali inakuwa na takwimu kamili za mazao yanayosafirishwa nje ya nchi.
Baadhi ya masharti
nafuu ambayo mfanyabiashara anatakiwa, kuyafuata ni pamoja na kuwasilisha
taarifa zake binafsi kama Jina lake kamili au Jina la Kampuni, anuani ya makazi,
au eneo analotoka na uthibitisho wa mazao anayotaka kusafirisha nje ya nchi.
Aidha, Bwana Mandepo
aliongeza kuwa Mfanyabiashara wa mazao kwenda nje ya nchi atapaswa kuwa na
Cheti cha ubora wa mazao husika anayosafirisha, kinachojulikana kama ‘phytosanitary
certificate’ kwa mujibu wa Sheria inayosimamia
ubora wa mazao (The Plant Protection Act 1997). Sheria hiyo inataka mazao yanayosafirishwa
nje au kuingizwa nchini, yawe na ubora unaokubalika Kimataifa.
Bwana Mandepo
alimalizia kwa kutoa wito kuwa nafasi ipo wazi kwa kila Mtanzania kuchangamkia
fursa ya kusafirisha mazao nje ya nchi kwa kuwasilisha maombi ya kibali kwa Wizara ya Kilimo Chakula
na Ushirika kwa ajili ya kupata kibali hicho na kwamba Mfanyabiashara
anayewasilisha maombi yake, anapaswa kuambatanisha leseni yake ya biashara,
cheti cha mlipakodi na awe na idhini ya maandishi kutoka Wilaya au Mkoa ambako
mazao husika yanatoka.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...