Watumishi Wizara ya Fedha na Mipango wameaswa kufanya kazi kwa weledi na kuwekeza nguvu zaidi katika ukusanyaji mapato ili kukuza uchumi wa nchi na kuifanya nchi iwe kitovu cha uchumi Barani Afrika.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango alipokuwa akiongea na watendaji wa Wizara hiyo alipowasili Wizarani hapo mara baada ya kuapishwa jana Ikulu jijini Dar es salaam.
Katika mazungumzo yake na watendaji hao, Mhe. Dkt. Mpango, aliuagiza uongozi wa Wizara yake kuunda na kisimamia sera za mfumo wa ukusanyaji kodi ambao utabaki kuwa rafiki kwa wafanyabiashara ili kukuza biashara na uwekezaji nchini.
“Ili kutekeleza kutekeleza ukusanyaji wa kodi kwa kutumia mfumo rafiki kwa wafanyabiashara na Serikali, Wizara inawajibu wa kusimamia na kukuza uchumi ambao utawanufaisha wananchi walio wengi, kwa kuhakikisha kodi zote ndogondogo ambazo ziko chini na nje ya Wizara, ambazo ni kero kwa wanachi wa hali ya chini zinapatiwa ufumbuzi kwani wananchi hao nao wanastahili maisha mazuri” Alisema Mhe. Dkt. Mpango.
Waziri Dkt. Mpango aliwasisitiza watendaji kufanya kazi kwa bidii, maarifa na weledi ili nchi iweze kupiga hatua kwa kuzingatia nidhamu katika kufanya kazi ambayo ni dhamana walizokabidhiwa.
Naye Naibu Waziri Wizara ya Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji aliwahimiza watendaji wa wizara hiyo kufanyakazi kwa umoja na mshikamano waliokuwa nao katika utendaji kazi ili kuleta maendeleo yenye tija huku akisisitiza kuwa wizara hiyo ndiyo msingi katika kukuza uchumi wa nchi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Servacius Likwelile aliwapongeza Viongozi hao wapya wa Wizara kwa kuteuliwa kwao kuiongoza Wizara ambayo ndiyo muhimili wa Serikali.
Aidha, Dkt. Likwelile alitoa wito kwa watendaji wa wizara hiyo kuzingatia maagizo ya Mhe. Waziri kwa maendeleo ya nchi ili kulinda hadhi na heshima ya wizara.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip
Mpango akisoma kadi ya pongezi aliyoipokea kutoka kwa viongozi kwa niaba ya watumishi wa
Wizara hiyo yenye lengo la kumpongeza kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo. Wa
kwanza kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Servacius Likwelile
na Mkurugenzi Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu Bi. Deodatha Makani (katikati).
Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Sera Prof.
Adolph Mkenda akifafanua jambo ofisini kwa Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt.
Philip Mpango mara baada ya kuwasili Wizarani hapo jana jijini Dar es salaam.
Watendaji wa Wizara ya
Fedha na Mipango wakielezea majukumu ya Idara na Vitengo katika mkutano na Waziri
wa Fedha na Mipango Mhe.Dkt. Philip mara baada ya kuwasili Wizarani hapo jana jijini Dar es salaam.
Habari na picha na Kitengo cha Mawasiliano
Wizara ya Fedha
na Mipango
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...