
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewaagiza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri
zote nchini kuhakikisha kuwa wanaongeza udhibiti na usimamizi wa
migogoro ya ardhi kwenye maeneo yao husika.
Ametoa agizo hilo leo mchana (Jumatano, Desemba 23, 2015) wakati
akizungumza na viongozi wa mkoa wa Lindi kwenye Ikulu ndogo mara baada
ya kuwasili akitokea jimboni kwake Ruangwa.
“Ardhi ni mali ya Serikali lakini
maeneo yanayotwaliwa kwa sababu mbalimbali za maendeleo yasiwe chanzo
cha migogoro na wananchi tunaowaongoza,” alisema.
Akitoa mfano, Waziri Mkuu alisema
anatambua kuna mgogoro wa eneo la mgodi katika wilaya ya Ruangwa baina
ya wananchi na wawekezaji wa kampuni ya Uranex. Na hii ni kwa sababu wao
ndiyo waliamua kufanya tathmini (evaluation) ya eneo hilo. Yale ni
makosa kwa sababu aliyepaswa kufanya tathmini ni Halmashauri na siyo
mwekezaji,” alisema.
Alisema wawekezaji wanaruhusiwa
kisheria kufanya tathmini lakini sheria waliyoitumia ni sheria namba 8
peke yake. “Kama Halmashauri ingefanya kazi hiyo ni lazima wangetumia
sheria ya ardhi ya vijiji pamoja na sheria ya madini na wananchi
wangepata thamani halisi ya ardhi yao,” alisema.
“Ninaagiza Halmashauri ya Wilaya
ya Ruangwa ikahakiki lile eneo na kubaini kama ni la kilimo au la madini
na kama ni la kilimo, wananchi wamelima mazao gani na kwa muda gani
kisha wafanye tathmini upya. Yuko valuer wa Halmashauri mwenye dhamana
hiyo na siyo wao,” alisema.
“Nasisitiza tena ni vema
Wakurugenzi wote, Wakuu wa Wilaya chini ya uongozi wa Wakuu wa Mikoa
mjiridhishe kuwa hakuna migogoro kwenye maeneo yenu. Kama ipo, imalizeni
kwa kukaa mezani na kuzungumza na pande husika, inawezekana kabisa,”
alisisitiza.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...