Na. Tamimu Adam – Jeshi la Polisi.
Jeshi la polisi nchini, limeanzisha mpango wa kuboresha usalama wa jamii nchi nzima ambao unalenga kuboresha utoaji wa huduma bora kwa wananchi, kuboresha mawasiliano ya ndani na nje ya Jeshi la polisi kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wa usalama ambapo mpango huo utaanza kutekelezwa katika mkoa wa kipolisi kinondoni ambapo lengo lake ni kupunguza uhalifu kwa asilimia kumi ifikapo mwaka 2019.
Akihitimisha maabara ya mpango huo iliyofanya kazi kwa wiki sita, Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Abdulrahmani Kaniki aliwahakikishia washiriki wa maabara ya kuboresha usalama wa jamii, kuwa Jeshi la polisi litatekeleza kwa vitendo mapendekezo yote yaliyotokana na maabara hiyo, kwani baadhi ya mapendekezo hayahitaji bajeti hivyo utekelezaji wake utaanza mara moja.
“Kazi iliyofanywa na maabara hiyo ni kubwa na umuhimu katika kuboresha usalama wa jamii katika nchi yetu hivyo mapendekezo yote ni lazima yafanyiwe kazi ili kuleta mafanikio chanya”. Alisema Kaniki.
Aliongeza kuwa mpango huo umeanzia katika mkoa wa kipolisi kinondoni na baadaye utaenea nchi nzima, ambapo alizitaja sababu zilizopelekea kuanza na kinondoni kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa makosa, kupanuka mji, idadi kubwa ya watu na uwepo na shughuli nyingi za kiuchumi ukilinganisha na maeneo mengine.
Naye, Mtendaji mkuu wa ofisi ya Rais ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi (PDB), Omari Issa alisema mpango huo wa uboreshaji wa usalama wa jamii ambao unaanza na mkoa wa Kinondoni uliandaliwa kwa kuwashirikisha wadau kutoka taasisi mbalimbali za serikali na kijamii ambao kwa pamoja walishirikiana kwa pamoja katika kuangalia namna ya kuboresha usalama wa jamii ili kuwezesha jamii kuwa salama.
Aliongeza kuwa mpango wa matokeo makubwa sasa unahitaji kuzingatia vitu vikuu vitatu katika utekelezaji wake ambavyo ni kujiwekea vipaumbele, nidhamu ya utekelezaji na uwajibikaji hivyo alisema hana wasiwasi na Jeshi la Polisi katika utekelezaji wa mpango huo hapa nchini.
Mpango wa uboreshaji wa usalama wa jamii unalenga kuboresha na kurahisisha huduma mbalimbali zinazotolewa na Jeshi la polisi ikiwemo kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa askari, usimamizi wa rasirimali watu na vifaa na kuweka mikakati ya kuwashirikisha wadau wa kada mbalimbali ndani ya jamii katika kuboresha usalama wa jamii.
Maabara hiyo ya kuboresha usalama wa jamii ripoti yake inatarajiwa kukabidhiwa kwa Inspekta Jenerali wa Polisi hivi karibuni ili kuanza utekelezaji wake kwa kuanza na mkoa wa kipolisi wa Kinondoni.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...