Balozi Seif Ali Iddi akizindua Mradi wa Maji safi na salama katika kisiwa cha Tumbatu ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
 Balozi Seif akimtwisha ndoo ya Maji Bibi Miza Ali Haji mara baada ya kuuzindua mradi wa maji safi na salama katika kisiwa cha Tumbatu kiliopo Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na Wananchi wa Kisiwa cha Tumbatu waliohudhuria uzinduzi wa maji safi na salama hapo katika eneo la Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya hiyo pembezoni mwa Bandari ya Tumbatu.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwasili katika Bandari ya Kisiwa cha Tumbatu na kupokewa na Katibu Tawala wa Wilaya Ndogo ya Tumbatu Nd. Khatib Habib Ali kwa ajili ya uzinduzi wa Mradi wa Maji Safi na salama Kisiwani humo.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar daima itaendelea kutekeleza kazi zote zilizoahidiwa na chama cha zamani cha Afro Shirazy Party { ASP } katika kuwajengea  ustawi bora Wananchi wake.

Amesema  huduma za maji safi na salama ilikuwa ni miongoni mwa ahadi kubwa Nne zilizotolewa na ASP wakati ikiomba ridhaa ya kutaka kuviongoza Visiwa vya Zanzibar wakati ikipigania  kuwakomboa Wananchi wake.

Akizindua mradi wa maji safi na salama uliopo Wilaya ndogo ya Tumbatu Mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya kutimia miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 Balozi Seif Ali Iddi alisema SMZ inatambua  umuhimu wa maji kwa uhai na maendeleo ya Wananchi na ndio maana ikaamua kwa makusudi kutekeleza ahadi hizo.

Alisema hali ya upatikanaji wa huduma za maji safi na salama ndani ya Zanzibar hasa Vijijini inatia moyo kutokana na jitihada kubwa zilizochukuliwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } Wadau wa Maendeleo ndani na nje ya Nchi kwa kushirikiana katika kukabiliana na upungufu wa maji.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwakumbusha Wananchi  lazima wajenge tabia ya kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa vianzio vya maji kwa lengo la kulinda mazingira.

Akitoa Taarifa ya Kitaalamu ya mradi wa maji safi na salama katika Kisiwa cha Tumbatu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Mkaazi, Maji na Nishati Zanzibar Nd. Ali Khalil Mirza alisema ujenzi wa mradi huo ulioanzia kwa hatua ya uchimbaji  wa visima viwili vyenye uwezo wa kuzalisha Maji Lita Laki 250,000  katika Vijiji vya Tingatinga na Pale ulienda sambamba  na ulazaji wa Mabomba  yenye  urefu wa Kilomita 8.25.

Katibu Mkuu huyo wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati alifahamisha kwamba awamu ya kwanza ya mradi huo tayari imeshatumia zaidi ya shilingi Mia 636.7 Milioni wakati ile iliyobakia inatarajiwa kutumia shilingi Milioni 400.Mapema  akisoma  Risala ya Wananchi wa Kisiwa hicho Katibu Tawala wa Wilaya ndogo ya Tumbatu Ndugu Khatib Habib Ali alisema kukamilika kwa mradi huo wa maji safi na salama kutawapunguzia usumbufu wa kupata huduma hiyo hasa akina Mama.

Nd. Khatib alisema Wananchi wa Shehia zote nne zilizomo ndani ya Kisiwa cha Tumbatu wanathamini juhudi kubwa za Viongozi wao ambazo ni kichocheo cha kasi katika kuelekea kwenye  Maendeleo.Aliuomba Uongozi pamoja na wahandisi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } kuhakikisha kwamba awamu ya Pili iliyobakia ya mradi huo inakamilika kwa wakati uliopangwa.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...