Baada ya kufanikisha kwa Tamasha la siku ya Kandanda hapo
Oktoba 17 mwaka jana, Tamasha lililobeba Ujumbe wa "#OneBallOnTxt
Book" ikiwa ni Dhima kamili ya kunyanyua Mchezo wa mpira wa miguu kuanzia
ngazi ya shule ya msingi na kuwasisitizia watoto wetu umuhimu wa kusoma pia,
Timu nzima ya Wanakandanda imeonelea Kuufungua Mwaka 2016 kwa kwenda kutembelea
Kituo cha kulelea watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu na kukabidhi Mchango
wao ambao ulitokana na mauzo ya fulana za Tamasha la Siku ya Kandanda mwaka
jana.
Ikumbukwe tulieleza kwamba kwa kila Fulana moja
itakayonunuliwa, asilimia kumi itaenda katika kampeni ya
#MpiraMmojaKitabuKimoja (#OneBallOneTxtBook). Kamati ilifanikiwa kuuza Fulana
100 ambazo tumefanikiwa kutumia asilimia iliyotakiwa katika kununulia vifaa
ambavyo tunakabidhi katika kituo cha House of Blue Hope Leo hii.
Vitabu vilivyonunuliwa ni vya Hisabati, Kiingereza,
Kiswahili, Sayansi, Jiografia na Teknohama. Mipira imekabidhiwa miwili, ambayo
tulipewa na mdhamini, hivyo pesa iliyotakiwa kununulia mipira tuliongezea
katika vitabu.
“Tunashukuru Kandanda Day kwa mchango huu katika kituo
chetu, utasaidia kuwajenga watoto kimasomo na kimichezo” Amesema Msimamizi wa
kituo hicho, Daudi Mboma.
Pia Tunachukua nafasi hii kutoa shukrani zetu za dhati kwa
wadhamini wetu wote( BinSlum , BayPort
TZ, SDS, Michuzi Media Group, MacAuto Accessories, SalehJembe Blog, Pepsi,
GALACHA na Kandanda.co.tz) tuliokuwa nao toka Tunaanza Tamasha hili la Siku
ya Kandanda kwa Mwaka wa Tatu mfululizo kwa kujitolea kwao kwetu katika
kufanikisha Siku yetu pia kuwapa Mrejesho wa kile ambacho tumekifikia kwa Mwaka
wa Tatu!. Pia bila kuwasahau Chama cha Madaktari, TASMA, kwa kushiriki nasi katika
Tamasha la mwaka jana.
Hakika mafanikio ni mengi sana si rahisi ya kuyaorodhesha
yote lakini kwa Uchache ni kukua kwa Muamko kwa Familia ya watu wa Kandanda
katika ushiriki wa Siku hii, pia Kujua umuhimu wa kushiriki katika michezo kwa
Jamii katika kudumisha Afya za miili yetu pamoja na kushiriki katika upimaji wa
Afya zetu siku ya Tamasha.
Malengo ya Siku hii ya Kandanda ni kuinua Ari na Muamko kwa
wananchi wote katika kushiriki katika matamasha na kurudisha kile ambacho jamii
ya wasionacho wangekihitaji kukipata kupitia matamasha haya.
Kama Taifa mchezo upendwao zaidi ni Kandanda lakini bila
Maarifa na Vifaa hatuwezi kuja kuwa na Kina Mbwana Samatta ama Thomas Ulimwengu
wengi zaidi hivyo basi tunapenda tutoe Rai kwa Watanzania wote waliopo ndani na
nje ya Nchi kushirikiana nasi katika kufikia malengo yetu makuu ya kupeleka
Kitabu Kimoja na Mpira Mmoja katika kila Kaya ya Mtanzania mmoja ili kuinua
Elimu, Michezo pamoja na kujenga Afya ya miili yetu.
Tungependa watu wengi zaidi, kutoka katika jamii tofauti,
mashirika tofauti na hata makampuni tofauti tukaungana kwa pamoja Mwaka huu
2016 na kuifanya siku hii iwe kubwa zaidi na Tupeleke na kuwafikia watoto wengi
Zaidi. Tunatarajia kuwa na siku ya kandanda mwaka huu Katika siku ya Jumamosi
ya Tatu ya Oktoba (#Oktoba15), ikitanguliwa na matamasha madogo madogo ambayo
tutatoa utaratibu hapo baadae ili kuwapa wadau wa kandanda kote kushiriki.
Lengo letu ni kuhusisha Tamasha hili kufanyika siku moja katika sehemu
mbalimbali Tanzania, tukiwa na lengo moja.
Kwa kuwapelekea Kitabu Kimoja na Mpira Mmoja
Pamoja Tutaweza
Kamati ya Maandalizi Kandanda Day 2015
Picha ya Pamoja na baadhi ya watoto wa Kituo cha House of Blue Hope wakiwa na vitabu na mpira.
Bi Fatma (Team DizoMoja) akiwa na Msimamizi wa Kituo, Daudi Mbnoma.
Mwenyekiti wa Kamati, Patrick 'Patoo' Dumulinyi, akimkabidhi vitabu na mpira Mlezi wa kituo cha House of Blue Hope, Daudi Mboma. Kulia kwa Patoo ni Bi Fatma Hassan mwakilishi wa TeamDizoMoja na Kushoto kwa Mboma ni Meneja wa TeamIsmail (Mabingwa 2015/16), Ismail Mohammed.
Watoto wa kituo cha House of Blue Hope wakifurahia mpira
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...