WILAYA ya Igunga,Mkoani Tabora imetenga zaidi ya shilingi milioni 73 kutoka katika mifuko ya jimbo la Igunga mjini na jimbo la Igunga magharibi(Manonga) kwa ajili ya ununuzi wa madawati,ukarabati wa nyumba za walimu,ujenzi wa matundu ya vyoo katika baadhi ya shule na zahanati na kufuatilia matumizi ya shilingi milioni 50 zilizotolewa na mfuko wa jimbo kukamilisha baadhi ya majengo ya maabara za shule za sekondari wilayani hapa.

Akitoa taarifa ya mfuko wa jimbo la Igunga Magharibi,Mbunge wa jimbo hilo, Seif Khamis Gulamali amefafanua kuwa kati ya kiasi hicho cha fedha,zaidi ya shilingi milioni 35 zimetoka katika mfuko wa jimbo la Igunga magharibi na zaidi ya shilingi milioni 38 jimbo la Igunga mjini.

Aidha Mbunge Gulamali hata hivyo amebainisha kwamba lengo la mfuko huo wa jimbo kutoa fedha hizo katika shule za sekondari ni kuzijengea shule hizo mazingira ya kuziwezesha kuwa na sifa ya kupata kidato cha tano na sita katika kipindi cha miaka ijayo.

Kwa mujibu wa mwakilishi huyo wa wananchi wa jimbo la Igunga magharibi shilingi milioni kumi nyingine zimepelekwa katika shule ya sekondari Mwisi na shilingi milioni tano kwa kuchimba matundu ya vyoo na shimo la kutupia sindano katika zahanati.

Hata hivyo Gulamali ameweka bayana kuwa fedha hizo zilizotumika zimetoka katika bajeti ya mwaka unaoishia juni,30,mwaka huu na kuongeza kwamba katika bajeti ijayo ya 2016/2017 fedha itakayopatikana itazidi kuboresha na maeneo mengineyo ili kuhakikisha kwamba malengo yanafikiwa na kwa wakati uliopangwa.

Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Igunga mjini,Dk. Peter Dalali Kafumu ameweka wazi kwamba mfuko wa jimbo umedhamiria kutumia shilingi milioni 38 kwa ajili ya miradi mbali mbali ya maendeleo iliyopo katika jimbo hilo.

Aidha mfuko huo wa jimbo umetoa shilingi milioni 12 kwa ajili ya kupaua nyumba ya mwalimu wa shule ya msingi Mwakipanga iliyokuwa imeezuliwa na upepo na hivyo kuwafanya wanafunzi wa shule hiyo kusomea nje kwa kukaa kwenye miti ambako huko nako wamepeleka shilingi milioni 12.

Akibainisha zaidi Dk.Kafumu ameweka wazi pia kwamba shilingi milioni mbili zilipelekwa kujenga matundu ya vyoo katika shule ya Ntobo na shilingi milioni mbili zilizobakia zitatumiwa na kamati iliyoundwa kwa ajili ya kufuatilia matumizi ya shilingi milioni 50 zilizotolewa na mfuko huo kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya maabara.

Amesisitiza kwamba hatua ya kuundwa kwa kamati hiyo kumetokana na idadi kubwa ya wananchi kutoka katika vijiji mbali mbali kulalamikia matumizi ya fedha hizo pamoja na mifuko ya saruji zilizopelekwa kuwa hazijafika.
Mkuu wa wilaya ya Igunga, Mkoani Tabora, Bi Zippora Pangani akifungua mkutano wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo uliofanyika mjini Igunga.
Mbunge wa jimbo la Igunga magharibi (Manonga), Mkoani Tabora, Seif Khamisi Gulamali (kulia) pamoja na Mbunge wa jimbo la Igunga mjini, Dkt. Dalali Kafumu (shoto) wakiwa kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo wakati wa mkutano wa kawaida wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo uliofanyika mjini Igunga.
Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Igunga,Mkoani Tabora wakiwa kwenye mkutano wa kawaida wa baraza la Halmashauri hiyo uliofanyika mjini Igunga.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...