Mfuko wa Maendeleo ya jamii –TASAF-umeanza mkakati maalumu utakaowezesha jamii ya Wahadzabe walioko katika mikoa ya Arusha,Manyara na Singida kuandikishwa katika Mpango wa Kunusuru Kaya maskini unaotekelezwa na mfuko huo nchini kote.

Wakizungumza wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya maskini unavyotekelezwa katika wilaya ya Karatu mkoani Arusha,viongozi wa TASAF walioambatana na wadau wa maendeleo walioongozwa na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia nchi za Tanzania Bi.Bella Bird,na baadhi ya maafisa wa benki hiyo kutoka Marekani ,baadhi ya wahadzabe waliomba kuorodheshwa katika Mpango huo ili waweze kunufaika na huduma zitolewazo kupitia utaratibu wa kuhawilisha fedha.

“ baadhi ya wananchi wenzetu wameandikishwa kwenye mpango huku wengi wetu hatujapata fursa hiyo na tumeanza kuona namna wanavyonufaika na huduma za mpango huo’’ alisisitiza mmoja wa wahadzabe katika kijiji cha Endamaghan umbali wa kilometa 70 kutoka makao makuu ya wilaya ya Karatu mkoani Arusha.

Akizungumza baada ya kutembelea makazi ya wahadzabe Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bi. Bella Bird amepongeza jitihada zinazochukuliwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF- kwa kuweza kuwafikia wananchi ambao wanakabiliwa na umaskini nchini kote.

‘’Benki ya Dunia inatambua na kuunga mkono jitihada za serikali ya Tanzania katika kukabili tatizo la umaskini miongoni mwa wananchi wake,umuhimu mkubwa pia unapaswa kuwekwa katika kunusuru jamii za watu walioko katika mazingira magumu wakiwemo wahadzabe” alisisitiza Bi. Bird.

Kwa upande wake,Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF-Bwana Ladsilaus Mwamanga alisema zoezi la kutambua na kuziandikisha kaya maskini katika jamii ya Wahadzabe lilifanyika. Hata hivyo alisema zoezi hilo liliathiriwa kwa kiwango kikubwa na mfumo wa maisha ya jamii hiyo wa kuhamahama kutafuta chakula kwa kuwinda wanyama na kuokota matunda na asali.

“Hatukuweza kuwaandikisha wote ingawa kimsingi wanastahili kuingizwa kwenye Mpango,hii ilitokana na kuhamahama kwa wananchi hao kujitafutia chakula hususani matunda, asali na mizizi” alisisitiza Bwana mwamanga.

Hata Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TASAF ameahidi kuwa kazi ya kuziandikisha kaya za walengwa katika jamii hiyo ya wahadzabe na nyingine zenye maisha ya kuhamahama itafanyika upya na kwa haraka ili waweze kuziingiza kwenye Mpango wa Kunusuru na Kaya Maskini unaotia mkazo katika kuboresha maisha ya walengwa hususani kupitia sekta za elimu, afya,lishe na kukuza kipato kwa kaya za walengwa.

Zifuatazo ni picha za ziara ya viongozi wa TASAF na Wadau wa Maendeleo katika maeneo ya wahadzabe,wilayani Karatu Mkoani Arusha.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Bw. Ladislaus Mwamanga (aliyevaa Kaunda suti) akiwasikiliza baadhi ya wananwake wa jamii ya Wahadzabe katika kijiji cha Endaghan wilayani Karatu mkoani Arusha wakati wa ziara ya wadau wa maendeleo na TASAF kuona utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini .
Baadhi ya Wananchi kutoka jamii ya Wahadzabe wakisikiliza hotuba ya Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bi. Bella Bird ( hayupo pichani) alipotembelea kijiji cha Endamaghan kuona utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia TASAF.
Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bi. Bella Bird akiwahutubia wakazi wa Endamaghan katika wilaya ya Karatu mkoani Arusha juu ya utekelezaji wa Mpango 
Mmoja wa Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika kijiji cha Endamaghan kutoka jamii ya Wahadzabe akipokea fedha za ruzuku kupitia mpango huo.
Baadhi ya walengwa wa Mpango wa kunusuru kaya maskini katika kijiji cha Endamaghan wakiwemo jamii ya Wahadzabe wakisikiliza hotuba ya Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bi. Bella Bird (hayupo pichani) juu ya utekelezaji wa Mpango huo.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...