Na Benny Mwaipaja,MoFP

SERIKALI za Tanzania na Korea Kusini, zimetiliana saini Hati ya Makubaliano (Aide Memoire) kwa ajili ya Ushirikiano wa utekelezaji wa Miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwemo wa Maji, Nishati, Kilimo, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano-TEHAMA na Viwanda itakayogharimu Dola za Marekani Milioni 300, sawa na TSh.Bilioni 650, katika kipindi cha miaka mitano ijayo kuanzia mwaka 2016 hadi 2020.

Fedha hizo ni sawa na ongezeko la Dola Milioni 100 ikilinganishwa na kiasi cha Dola Milioni 200 ambazo nchi hiyo ya Korea iliipatia Tanzania kama mkopo wenye masharti nafuu katika kipindi cha miaka miwili iliyopita (2014 hadi 2016).

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Shaaban, ametia saini makubaliano hayo kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, huku upande wa Korea Kusini ukiwakilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Fedha ya Korea Bw. Weon-Kyoung Jo.

Kusainiwa kwa makubaliano hayo ni mwanzo wa matayarisho ya kuandaa Mpango kazi wa namna ya kutekeleza miradi hiyo ili iende sambamba na Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa miaka 5 uliozinduliwa hivi karibuni mjini Dodoma na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa na Mkakati Mbadala wa Kupunguza Umaskini Zanzibar (MKUZA Successor Strategy).

Akizungumza mara baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Shaaban, amesema kuwa miradi hiyo ya maendeleo iliyochaguliwa kutekelezwa katika sekta zilizotajwa zitachochea ukuaji wa uchumi wa Taifa na kupunguza umasikini kwa wananchi.

Bi. Amina Shaaban alisema kwamba Hati hiyo ya Makubaliano ya ushirikiano kati ya Tanzania na Korea Kusini, yamejikita zaidi katika uboreshaji wa mifumo ya Tehama, kuimarisha sekta ya kilimo pamoja na kuboresha miundombinu inayosaidia ukuaji wa viwanda hususan ya nishati ya umeme katika kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2016/17 hadi 2020/21.

“Ushirikiano wa Tanzania na Korea Kusini umeanza tangu mwaka 2000, kwa kuhusisha taasisi zake mbili ambazo ni Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA) ambalo limeipatia Tanzania kiasi cha zaidi ya dola za Marekani 30.9 na Benki ya Exim-Korea ambayo imetoa Dola za Marekani zaidi ya Milioni 455 sawa na zaidi ya Tsh 900 bilioni kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii katika kipindi cha miaka 10 iliyopita” alisema Bi. Amina Shaaban 
Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa Kimataifa (Uchumi) wa Wizara ya Fedha ya Korea Weon-Kyoung Jo (kushoto) akizungumza wakati wa mjadala wa Ushirikiano katika misaada ya maendeleo ya kiuchumi kabla ya kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Korea, yenye thamani ya dola Milioni 300, katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dar es salaam.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Hamis Shaban na Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa Kimataifa (Uchumi) wa Korea Weon-Kyoung Jo wakibadilishana Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Miradi mbalimbali ya Maendeleo baada ya kusainiwa. Hati hiyo ina thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 650.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Hamis Shaban na Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa Kimataifa (Uchumi) wa Korea Weon-Kyoung Jo wakisaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Miradi mbalimbali ya Maendeleo, yenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 650.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Hamis Shaban na Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa Kimataifa (Uchumi) wa Korea Weon-Kyoung Jo wakipeana mikono baada ya kusaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Miradi mbalimbali ya Maendeleo, yenye thmani ya zaidi ya dola za Marekani milioni 300, katika ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...