Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Balozi wa Kuwait nchini, Jasem Al Najem wakiwa wamekalia madawati mawili kati ya 50 yaliyotolewa na Kuwait na kukabidhiwa kwake na balozi huyo jijini Dar es salaam Agosti 17, 2016.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea msaada wa sh. milioni 12 kutoka mashirika ya misaada ya Kuwait kwa ajili ya kununulia madawati ili kupunguza tatizo hilo nchini. Pia amepokea madawati 100 kutoka ubalozi wa Kuwait na taasisi ya Direct Aid ya nchi hiyo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo leo (Jumatano, Agosti 17, 2016), Balozi wa Kuwait nchini Tanzania, Bw. Jasem Al Najem amesema msaada huo ni michango kutoka mashirika ya misaada ya nchi yake ambayo yanatoa huduma mbalimbali hapa nchini.

“Tumejipanga kukamilisha ahadi ya madawati 600, tunaendelea kuwasiliana na wenzetu wa Kuwait Fund, na mashirika mengine. Kwa sasa tunachangia madawati, baadaye tutakwenda kwenye ujenzi wa madarasa, hata ikibidi tutaenda kwenye ujenzi wa shule,” alisema.

Balozi Najem amesema wanatoa misaada hiyo ili kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais Dkt. John Magufuli za kutaka wanafunzi wote wakae kwenye madawati.

Akitoa shukrani mara baada ya kupokea msaada huo, Waziri Mkuu alimshukuru Balozi wa Kuwait kwa moyo wao wa kujitolea ikizingatia kuwa ni wiki tatu tu zilizopita alikwishatoa msaada mwingine wa madawati kwenye shule ya msingi Chamazi, wilayani Temeke jijini Dar es Salaam.

Aliyashukuru pia mashirika ya misaada kupitia Ubalozi huo, ambao wametoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa madawati. Ametoa wito kwa mabalozi wengine, sekta binafsi na wadau wa maendeleo watoe michango zaidi ili yapatikane madawati ya kutosha.

Mashirika yaliyotoa michango hiyo ni African Relief Organisation (hundi ya sh. milioni 6), Al Furqaan Islamic Centre (hundi ya sh. milioni 6), Taasisi ya Direct Aid (madawati 50 ya shule za Msingi) na ubalozi wa Kuwait (madawati 50 ya shule za sekondari).

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S.  L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM.

JUMATANO, AGOSTI 17, 2016.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...