MAONYESHO ya biashara na Utalii yaliyoandaliwa nchini Saud
Arabia katika Mji wake Mkuu wa Riyadh, yamefanyika wiki iliyopita huku Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ikionekana kung’ara baada ya wageni wengi kupendezwa na
bidhaa zilizokuwa zinaonyeshwa katika banda la Tanzania.
Katika maonyesho hayo ambayo bidhaa mbalimbali zilionyeshwa
ukiwamo eneo maalum la mlima Kilimanjaro, nguo za Kitanzania na viatu pamoja na
bidhaa nyingine muhimu zilizoonekana kuwapendeza wengi waliohudhuria maonyesho
hayo.
Akizungumza katika maonyesho hayo, Balozi wa Tanzania nchini Saud Arabia, Mheshimiwa Hemed Mgaza, alisema kwamba wananchi wengi waliohudhuria maonyesho hayo walionekana kuvutiwa zaidi na nchi ya Tanzania kutokana na vivutio vyake.
Alisema hali hiyo imekuja kutokana na aina ya bidhaa zilizoonyeshwa pamoja na ubunifu wa kutangaza bidhaa zao na nchi kwa ujumla, wakiamini kuwa utachochea wageni wengi wa kutoka nchini hapa kwenda kutembelea nchini Tanzania kwa mambo mbalimbali.
“Tumewahakikishia kwamba mbali na nchi yetu kujawa na
vivutio vingi kutoka Tanzania Bara na Visiwani, lakini bado tumejawa na amani
kiasi kwamba unapokuwa kwenye ardhi ya Tanzania huna sababu ya kuwa na wasiwasi
wowote kwa sababu wananchi wake wanaishi kwa upendo,” alisema Balozi Mgaza.
Kwa mujibu wa Balozi Mgaza, maonyesho hayo kwenye ofisi yao
waliyapa jina la Visit Tanzania the land Kilimanjaro, Serengeti and Zanzibar,
ambapo pia walitangaza bidhaa za chai, kahawa, viatu vya kimasai, vinyago vya
wanyama na nguo za utamaduni.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...