Mkurugenzi wa TradeMark Tawi la Tanzania, Bw. John Ulanga akifungua Mkutano wa Chama cha Wafanya Biashara Wanawake wa Tanzania (TWCC) jijini Dar es salaam mwishoni mwa wiki. |
Tanzania itafaidika na msaada wa Dola za Marekani Milioni
5,300,000 ambazo ni zaidi ya Shilingi Bilioni 12 za Kitanzania, zitakazotolewa
na Taasisi ya TradMark, East Afrika, kuwajengea uwezo wafanyabiashara wanawake
wa Tanzania, kuyafikia masoko ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, hata nje ya
Afrika na kwa kuanzia, TradeMark,
itaanzisha madawati ya jinsia kwenye mipaka mitatu ya Holili, Kabanga na
Mutukula.
Ahadi ya fedha hizo, imetolewa na Mkurugenzi wa
TradeMark Tawi la Tanzania, Bw. John
Ulanga (pichani), wakati akifungua Mkutano wa Chama cha Wafanya Biashara Wanawake wa Tanzania,
TWCC, kujadili vikwazo kwa
wafanyabiashara wanawake mipakani, uliofanyika jijini Dar es Salaam, mwishoni
mwa wiki.
Ulanga amesema fedha
hizo zitatolewa na TradeMark East Africa, kupitia mradi wake wa “Women in
Trade” uliolenga kuwajengea uwezo
kuhimili ushindani wa kibiashara na kukabiliana na vikwazo vya kibiashara kwa wafanyabiasha
wanawake Tanzania kuwawezesha kufanya biashara ya kimataifa ikiwemo kuwezesha
bidhaa zao kuyafikia masoko ya nchi za Afrika Mashariki na soko la kimataifa.
Bwana Ulanga amesema, TradeMark East Africa ni taasisi
inayoongoza katika kuleta usawa wa kijinsia katika biashara, kwa sababu utafiti
umeonyesha kuwa asilimia 70% ya wanaofanya biashara za mipakani ni wanawake na
wanakabiliwa na vikwazo vingi vya kibiashara vikiwemo vikwazo vya kijiografia,
vikwazo vya kijinsia, vikwazo vya kisheria, vikwazo vya kimtazamo, hivyo
TradeMark imeandaa mpango kamambe wa miaka sita wa kuwajengea uwezo,
atakaogharimu shilingi bilioni 12, kati ya hizo, Chama cha Wafanyabiashara
Wanawake Tanzania, TWCC, kitapatiwa shilingi milioni 500.
Akishukuru kwa msaada huo, Mwenyekiti wa Chama cha
Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC), Bibi Jaquiline Mneney Maleko,
ameishukuru TradeMark kwa msaada huo, na kuahidi utatumika vizuri kwa malengo
yaliyokusudiwa.
TradeMark East Africa (TMEA) ni shirika lisilo la kiserikali, la maendeleo
kwa lengo la kuongezeka ustawi wa kiuchumi katika nchi za Jumuiya ya Afrika
Mashariki kwa njia ya biashara. TMEA inafanya kazi kwa karibu na taasisi za
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), serikali za kitaifa, sekta binafsi na asasi
za kiraia.
TMEA inachangia ukuaji wa biashara Afrika Mashariki kwa kufungua fursa za
kiuchumi kupitia:
• Kuongezeka kwa fursa za upatikanaji
wa masoko;
• Kuboresha mazingira ya biashara; na
• Kuboresha biashara ya ushindani.
Kuongezeka kwa kiwango cha biashara kuchangia
ukuaji wa uchumi, na kupunguza umaskini na hatimaye kuongezeka ustawi.
TMEA ina makao
yake makuu mjini Nairobi nchini Kenya, na ina
matawi katika miji ya Arusha, Bujumbura, Dar es Salaam, Juba, Kampala na
Kigali.
Ili kujua zaidi kuhusu TMEA, tafadhali tembelea tovuti TMEA katika www. www.trademarkea.com
Mwisho
Mkurugenzi wa TradeMark Tawi la Tanzania, Bw. John Ulanga akifafanua jambo wakati akifungua Mkutano wa Chama cha Wafanya Biashara Wanawake wa Tanzania (TWCC)
Mkurugenzi wa TradeMark Tawi la Tanzania, Bw. John Ulanga wakati akifungua Mkutano wa Chama cha Wafanya Biashara Wanawake wa Tanzania (TWCC)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...