Na Rhoda James.

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amekutana na Waziri wa Migodi na Nishati wa Namibia, Obeth Kandjoze na kuzungumza masuala mbalimbali kuhusu sekta wanazozisimamia.

Kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Wizara ya Nishati na Madini kilihudhuriwa na Viongozi Waandamizi Kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Maurel et Prom Tanzania na Namibia, Christophe Maitre pamoja na Ujumbe kutoka Wizara ya Migodi na Nishati.

Profesa Muhongo alielezea kuhusu, ugunduzi wa gesi asilia ambao umefikia futi za ujazo wa trilioni 57.25T. Ujenzi wa mabomba ya kusafirishia gesi asilia kama vile Mradi wa Songo Songo, Mnazi Bay na ule wa kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.

Aliongeza kuwa, Serikali ya Tanzania inatekeleza miradi mikubwa ikiwa ni pamoja na Mradi wa Gesi Asilia kimiminika (Liquefied Natural Gesi) unaotarajiwa kujengwa mkoani Lindi, Kiwanda cha kutengeneza mbolea na ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima Uganda hadi Bandari ya Tanga Tanzania.

Pia, alizungumzia kuhusu madini, akisema kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na Madini mengi ikiwa ni pamoja na Uranium ambapo alimuomba Waziri Kandjoze wa Namibia kuangalia uwezekano wa wataalam wa Tanzania kwenda kujifunza zaidi kuhusu madini hayo nchini Namibia kwani nchi hiyo imepiga hatua katika masuala ya uchimbaji wa madini husika.

Kwa upande wake, Waziri Kandjoze aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa mapokezi mazuri na kusema kuwa, Namibia ina uzoefu mkubwa katika masula ya uchimbaji madini ya Uranium. Namibia ni nchi ya tano duniani katika uzalishaji wa Uranium ambapo madini hayo yanauzwa nje ya nchi na kuzalishia umeme.

Waziri Kandjoze alisema kuwa, atatembelea Taasisi zilizopo chini ya Wizara ikiwa ni pamoja na TPDC, TANESCO na EWURA ili kupata elimu zaidi kuhusu sekta za Nishati na Madini.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akielezea uzoefu wa Tanzania katika masuala ya Sekta za Nishati na Madini. Kulia kwake ni Waziri wa Migodi na Nishati wa Namibia, Obeth Kandjoze. Wengine katika picha ni viongozi waandamizi kutoka Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zake pamoja na Ujumbe kutoka Wizara ya Migodi na Nishati ya Namibia.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akimsikiliza mtaalam kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) (hayupo pichani) akielezea kuhusu tozo mbalimbali ikiwemo ile ya tariff. Kulia kwake ni Waziri wa Migodi na Nishati wa Namibia, Obeth Kandjoze. Wengine katika picha ni Ujumbe kutoka Namibia.
Waziri wa Migodi na Nishati wa Namibia, Obeth Kandjoze (akisaini kitabu cha wageni) ofisini kwake. Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo(anayeshuhudia).
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Migodi na Nishati wa Namibia, Obeth Kandjoze pamoja na Ujumbe kutoka Namibia.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...