Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto imependa kuwatakia kheri na mafanikio watoto wote wa kidato
cha nne walioanza kufanya mtihani wa Taifa wa kuhitimu elimu ya
Sekondari kuanzia tarehe 01 Novemba, 2016. Wizara yenye dhamana ya
maendeleo ya watoto inawaomba watoto wanaotahiniwa kutambua kuwa, muda
wa kufanya mtihani ni fursa adhimu kwao, hivyo ni lazima kuutumia kwa
umakini mkubwa kwa ajili ya mustakabali wa maisha yao binafsi, familia
na taifa kwa ujumla.
Wizara inawaasa
kuwa waangalifu muda wote wa kutahiniwa, wazingatie kanuni na taratibu
stahiki, na pia kuepuka kuandika mambo ambayo yasiyotakiwa katika
karatasi za mtihani. Kipindi cha kufanya mtihani ni kifupi ukilinganisha
na muda wa miaka minne ambayo watoto hawa wamekaa madarasani wakiwa
katika masomo; hivyo watoto wanahimizwa kujiepusha na vishawishi
vyovyote ikiwemo vitendo vya udanganyifu katika chumba cha mtihani
ambavyo vinaweza kusababisha kubatilishwa kwa matokeo yenu na hivyo
kukatisha ndoto zenu. Ni matarajio ya Wizara kuwa wote mtamaliza
mitihani yenu vizuri na kwa amani na utulivu.
Wakati
watoto wetu wakiendelea kufanya mitihani yao, Wizara inawakumbusha
wazazi na walezi kutambua kuwa mnaowajibu wa kuweka mazingira ya
kuwasaidia kukumbuka yote waliyojifunza kipindi chote cha masomo yao na
kuwa tayari kujibu mitihani yao wakiwa wameandaliwa kisaikolojia ili
kuhitimu vizuri. Aidha Serikali haitarajii kusikia au kuona mzazi au
mlezi yeyote akijaribu kutengeneza mazingira ya kuharibu ndoto ya mtoto
yeyote hasa watoto wa kike kwa kupanga kuwaozesha mara tu wanapomaliza
mitihani ya Taifa ya kidato cha Nne.
Wizara
inaamini kuwa wazazi na walezi watakuwa makini kuandaa mazingira ya
watoto kufikia ndoto zao kielimu, na kuwaepusha watoto wa kike na janga
la ndoa za utotoni, hadi watakapofikia umri stahiki. Wizara inasisitiza
kwamba atakayethubutu kukatisha ndoto ya mtoto wa kike kwa kumwozesha
chini ya umri wa miaka 18, Serikali haitasita kuchukua hatua kali za
kisheria dhidi ya mzazi na mlezi huyo ili kulinda haki na masilahi ya
mtoto kulingana na sheria, taratibu na kanuni zinazomlinda mtoto.
Wizara
inatoa rai kwa wazazi, walezi, makondakta na jamii kwa ujumla, kuwapa
ushirikiano madhubuti watoto wetu katika kipindi hiki cha mitihani yao
ili waweze kuhitimu vizuri mitihani yao. Watahiniwa ni hawa ni vijana
wetu wanaotarajiwa kuendeleza taifa letu, hivyo tuwajengee mazingira
murua ya kupata haki ya elimu ili kuwa na vijana mahiri na wenye weledi
wakiwa na stadi na maarifa ya kubeba majukumu ya Taifa katika harakati
za kuelekea uchumi wa kati,
MARGARET S. MUSSAI
KAIMU MKURUGENZI WA MAENDELEO YA WATOTO
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...