Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es salaam
Waziri
Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, ameiagiza Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu
nchini (NBAA) kuwachukulia hatua wale wote wanaoitia doa taaluma hiyo kwa
kufanya ubadhilifu wa fedha za umma.
Maagizo
hayo yametolewa kwa niaba yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mpango,
wakati wa Uzinduzi wa Kituo cha Taaluma ya Uhasibu (APC) uliokwenda sambamba na
ufunguzi wa Mkutano wa mwaka wa wahasibu unaojumuisha wadau kutoka nchi za Afrika
Mashariki, katika eneo la Bunju, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Amesema
kuwa Idadi ya Wahasibu wenye sifa inazidi kuongezeka na hivyo kuisaidia Serikali,
japo kuwa Serikali hairidhiki kuona wanataaluma wa Uhasibu na Ukaguzi wa hesabu
(CPA) wanaongezeka huku vitendo vya ubadhilifu wa fedha za Umma na ufisadi vikiendelea
kuripotiwa.
“Wapo
hata wahasibu wanaotumia taaluma yao vibaya, wanaowawezesha wafanyabiashara
kukwepa kodi, wanachakachua vitabu vya taarifa za fedha na kufanya ufisadi kwa
njia ya kalamu na kompyuta jambo ambalo halikubaliki hata kidogo” Aliongeza
Dkt. Mpango
Amesema
kuwa machozi ya masikini wa Tanzania yatawafuata mafisadi hadi kaburini lakini
serikali ya Awamu ya Tano haitasubiri hao mafisadi wafe, itawatumbua na wala
hakuna mzaha na kwamba tayari mahakama ya mafisadi imeanza kazi na
itawashughulikia.
Aidha,
Waziri huyo wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amewaasa wanataaluma wa
uhasibu na ukaguzi wa hesabu kuitumia taaluma yao kuisaidia Serikali katika
hatua yake ya kuelekea katika uchumi wa kati unaotegemea viwanda kwa kuwa
taaluma hiyo ina umuhimu mkubwa.
Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango (kulia), akikata utepe kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuashiria kuzindua rasmi Kituo cha Taaluma ya Uhasibu (APC), kilichopo Bunju jijini Dar es Salaam leo. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), Profesa Isaya Jairo na Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa GEPF, Joyce Shaidi.
Mwonekano wa baadhi ya majengo ya kituo hicho.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...