Wahasibu nchini wametakiwa kuzingatia viwango vya uhasibu vinavyotakiwa na kukubalika kitaifa na kimataifa wakati wa kuandaa taarifa za fedha kwa kuzingatia maslahi ya Taifa.

Wito huo umetolewa na Kamishna Msaidizi Sera, kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Shogholo Msangi, wakati akikabidhi tuzo za Taarifa Bora za Fedha kwa mwaka 2015/2016, kwaniaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dotto James tukio lililofanyika katika Kituo cha Taaluma ya Uhasibu (APC), kilichoko Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es salaam

Katika tukio hilo ambalo liliambatana na kufungwa  kwa Mkutano wa mwaka wa Wahasibu unaojumuisha nchi za Afrika Mashariki, Wizara ya Fedha na Mipango, kupitia Fungu 50, imepata tuzo ya kuandaa vitabu bora vya mahesabu vinavyokidhi viwango vilivyowekwa na Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi (NBAA).

Bw. Msangi amesema kuwa taarifa za fedha hutumika katika matumizi mbalimbali katika Sekta ya umma na binafsi, hivyo iwapo taarifa hizo zitakuwa katika viwango vyenye ubora zitaongeza imani ya wananchi kwa Serikali yao.

Amesema kuwa taarifa hizo pia hutegemewa na wawekezaji katika kupanga maamuzi yao ya uwekezaji hapa nchini hatua itakayosaidia nchi kufikia malengo yake ya kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), Bw. Pius Maneno, amesema kuwa, kumekuwa na mafanikio makubwa katika utoaji wa taarifa za fedha kwa upande wa Taasisi za Umma na Binafsi mwaka huo ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

“Mwaka uliopita Taasisi nyingi za umma zilishindwa kufikia asilimia 75 ambacho ndicho kiwango cha chini kabisa cha Taasisi kuingia katika ushindani wa Tuzo ya taarifa bora ya Fedha ya mwaka, lakini kwa mwaka huo, Taasisi za Serikali zilizokidhi kiwango hicho ni zaidi ya Asilimia 50.” AliongezaBw. Maneno.

Aidha, amesema kuwa katika kutafuta mshindi wa Tuzo hiyo taasisi mbalimbali zimehusishwa ikiwemo Mamlaka ya Bima Tanzania, Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Taasisi ya Utawala wa Fedha na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kabla ya matokeo kuthibitishwa na Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA).

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya NBAA Prof. Isaya Jairo amebainisha faida za tuzo ya taarifa bora ya fedha kuwa ni pamoja na kujenga uwazi, uwajibikaji, uadilifu na kuwa na taarifa ya fedha yenye viwango.Amezitaka Taasisi nyingi kushiriki katika ushindani ili kuboresha taarifa za fedha za Mashirika yakiwemo ya umma na binafsi, huku akitoa wito kwa Serikali kuziagiza Taasisi zake kushiriki kikamilifu.

Miongoni mwa wizara zilizoibuka na ushindi wa Tuzo hiyo ni Wizara ya Fedha na Mipango Fungu 50 ambapo iliwakilishwa na Mhasibu wake Mkuu Bw. Christopher Lupama kupokea Tuzo hiyo, ambaye amebainisha kuwa Tuzo hiyo imewapa nguvu ya kuendelea kufanya vizuri katika utoaji wa Taarifa ya Fedha yenye viwango.

Taasisi 56 zimeshiriki kuwania tuzo hiyo inayoandaliwa kila mwaka na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA).
 Mhasibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Fungu 50 Bw. Christopher Lupama, (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa alioambatana nao wakati wa kupokea tuzo ya Taarifa Bora ya Fedha kwa mwaka 2015, katika Kituo cha Taaluma ya Uhasibu (NBAA) kilichopo Bunju nje kidogo ya jiji la Dar es salaam.
Kamishna Msaidizi wa Sera wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Shogholo Msangi (kulia) na Mwenyekiti wa Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), Prof. Isaya Jairo wakibadilishana mawazo wakati wa zoezi la kuwakabidhi washindi wa Tuzo ya Taarifa bora ya Fedha kwa mwaka 2015, tukio lililofanyika katika Kituo cha Taaluma ya Uhasibu (APC) kilichopo Bunju nje kidogo ya jiji la Dar es salaam.
  Kamishna Msaidizi wa Sera wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Shogholo Msangi akiwa katika picha ya pamoja na na washindi wa tuzo ya Taarifa Bora za Fedha kwa mwaka 2015, katika Kituo cha Taaluma ya Uhasibu (NBAA) kilichopo Bunju nje kidogo ya jiji la Dar es salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...