*Ni la MSD litahudumia mikoa mitatu ya kanda ya Tabora.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefungua duka la dawa la Bohari Kuu ya Dawa (MSD) katika hospitali ya Manispaa ya Mpanda lilogharimu sh. milioni 55 litakalohudumia mikoa mitatu ya Kigoma, Katavi na Tabora.
Pia duka hilo itatoa huduma kwa vituo vya kutolea huduma za afya 580 ikiwa ni pamoja na hospitali za rufaa za mikoa miwili ya Kigoma na Tabora, Hospitali za wilaya sita za Nzega, Igunga, Urambo, Kobondo, Kasulu na Mpanda Mji.

Waziri Mkuu amefungua duka hilo la dawa la MSD, lililoko  katika hospitali ya Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi leo (Jumanne, Januari 17, 2017) ikiwa ni utekelezaji wa agizo alilolitoa kwa MSD Agosti 20, 2016 alipokuwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Katavi. Aliuagiuza  uongozi MSD kujenga duka hilo ili kurahisisha upatikanaji wa dawa katika mkoa huo pamoja na mikoa jirani.

Aidha, Waziri Mkuu amesema baada ya kufunguliwa kwa duka hilo Serikali haitarajii kusikia tena katika vituo vya afya na Zahanati zilizoko mkoani Katavi na mikoa jirani  zinakosa dawa. Amewaagiza Wakurugenzi kusimamia suala hilo na kuhakikisha vituo vyote vya afya vinakuwa na dawa za kutosha.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameziagiza Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto kukutana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kutafuta namna bora ya kutumia fedha za huduma za afya zinazipatikana katika halmashauri nchini.
Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali imetoa sh. bilioni 1.5 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa hospitali ya mkoa wa Katavi ili kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali ya Manispaa ya Mpanda.

Amesema lengo la Serikali ni kuwa na Hospitali ya Rufaa kwa kila mkoa, hivyo, Mkoa wa Katavi ni miongoni mwa mikoa mipya itakayojengwa Hospitali ya Mkoa ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Bw. Laurean Bwanakunu amesema ujenzi waduka hilo la Mpanda hadi kukamilika umegharimu sh. milioni 55, huku benki ya CRDB ikitoa sh. milioni 50 na MSD imeweka dawa na vifaa tiba vya sh. milioni 104.45 na vifaa vya TEHAMA vya sh. milioni tano.

Amesema kuanzishwa kwa duka hilo kutaongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa wagonjwa hasa dawa ambazo hazimo katika orodha zilizoidhinishwa na Serikali kutumika katika vituo vyake vya kutolea huduma za afya ila zimeidhinishwa kutumika nchini na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Amesema dawa na vifaa tiba vilivyomo katika orodha ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) zinapatikana katika duka hilo kwa bei nafuu, hivyo kuondoa usumbufu kwa wagonjwa kwenda kuzitafuta katika maduka ya mbali na kwa bei ghali.

“Nitoe mfano mdogo wa tofauti ya dawa katika ya maduka ya MSD na maduka ya mitaani, hapa dawa ya sindano ya kutibu fungus aina ya Fluconazole inauzwa sh. 2,300 na mitaani sh. 4,500 na dawa ya sindano kwa ajili ya kushusha kisukari (Insulin) chupa moja MSD ni sh. 8,500 na mitaani sh. 20,000,” amesema.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, JANUARI 17, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua duka la dawa la MSD katika hospitali ya Mpanda Januari 17, 2017.    Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali Mstaafu, Rafael  Muhuga na kulia kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu. Kulia ni Waziri wa Nishati na Madini , Profesa Sospeter Muhongo, Wapili kulia ni Mbunge wa mapanda Mjini, Sebastian Kapufi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipiga makofi  baada ya kufungua duka la dawa  la MSD katika hospitali ya Mpanda  Januari 17, 2017. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu na kulia ni Mbunge wa Mapanda Mjini Sebastian Kapufi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kakitazama dawa za bibadamu baada ya kufungua duka la dawa la MSD katika hospitali ya Mpanda Januari 17, 2017.  Watatu kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu na wapili kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Katavi, Muselem Said Abdallah.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kakitazama dawa za binadamu baada ya kufungua duka la dawa la MSD katika hospitali ya Mpanda Januari 17, 2017.  Kushoto  ni Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu .
Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akizungumza na Elizabeth Zephania , mmoja wa wazazi waliojifungua katika hospitali ya Mpanda  wakati alipotembelea wodi ya wazazi ya hospitali hiyo Januari 17, 2017.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)7.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...