Leo jijini Dar-es-Salaam, Thamini Uhai imetoa mrejesho wa shughuli zake tokea kuanzishwa kwake na kuwasilisha mipango yake kwa mwaka 2017 kwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Thamini Uhai (iliyoitwa World Lung Foundation hapo awali), imefanya kazi kwa karibu na wahisani pamoja na serikali za mikoa, kujenga mfumo ambao umepelekea ugatuzi wa huduma za dharura za kuokoa maisha ya mama na watoto wachanga kutoka hospitali kwenda kwenye vituo vya afya. 
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto - Mh Ummy Mwalimu (katikati) na Dr Hussein Kidanto - kaimu mkurugenzi wa idara ya huduma za kinga Wizara ya Afya (kushoto) wakishauriana na Mkurugenzi mtendaji wa Thamini Uhai, Dr Nguke Mwakatundu (Kulia) wakati wa mkutano wa mrejesho wa shirika la Thamini Uhai, leo jijini Dar-es-Salaam.

Mfumo huu wa kipekee wa huduma ya afya umehusisha pia kuboresha vituo vya huduma za afya ili viweze kutoa huduma hizi za dharura, kuendeleza mafunzo ya jamii kupitia vyombo vya habari na waelimishaji jamii ili kuhamasisha jamii itumie vituo vya huduma za afya, kuboresha mifumo ya rufaa, kuhakikisha upatikanaji wa ushauri wa afya kila wakati. Pia shirika imetoa mafunzo, usimamizi na elimu endelevu kwa wahudumu wa afya, waganga wasaidizi (AMO) na manesi ambapo elimu hiyo inatolewa na madaktari bingwa ili kugatua huduma na ujuzi na hivyo kuongeza uwezo katika jamii zilizopo pemebezoni.

Akizungumzia mafanikio yao, Dr. Nguke Mwakatundu, Mkurugenzi Mtendaji wa Thamini Uhai, amesema:
Wadau kutoka shirika la Thamini Uhai, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Ofisi ya Rais - Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa wakimsikiliza kwa makini Waziri Ummy Mwalimu wakati wa mkutano wa mrejesho wa shirika la Thamini Uhai, leo jijini Dar-es-Salaam.

“Moja ya mafanikio yetu muhimu ni jinsi shughuli zetu zimeweza kuleta mabadiliko katika maisha ya wagonjwa katika nyanja zinayotuhusu. Tumeona vifo vya uzazi na rufaa zikipungua kwa kiasi kikubwa na kwa njia endelevu katika maeneo haya, pamoja na kuona ongezeko la maana katika idadi ya wanawake wanaoamua kujifungua katika vituo vya huduma za afya.”

Akitilia mkazo baadhi ya changamoto, Dr. Mwakatundu ameeleza kuwa ili mafanikio haya yawe endelevu kuna haja ya kupanga rasilimali za kutosha kwa ajili ya wafanyakazi wa afya na kuboresha mfumo wa usamabazaji wa vifaa na madawa.

Waziri wa Afya, Mh, Ummy Mwalimu akitoa mchango wake kuhusu kazi za Thamini Uhai, amesema: “Ningependa kutambua mchango wenu katika kuhakikisha akina mama wanajifungua kwa usalama katika mikoa husika. Naelewa kuwa mmefanya kazi kubwa kuboresha mifumo ya huduma za dharura katika vituo vya afya na hospitali, mmeanzisha kampeni za mawasiliano na kuimarisha mifumo ya rufaa kutoka vituo vya afya kwenda hospitali.”

Thamini Uhai imekwisha kabidhi serikalini shughuli zake za mradi wa afya ya uzazi katika mikoa miwili – Morogoro na Pwani, na imepanga mwaka 2017 kuanza utaratibu wa kukabidhi shughuli zake katika mkoa wa Kigoma.
Wadau kutoka shirika la Thamini Uhai, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Ofisi ya Rais - Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa wakishauriana wakati wa mkutano wa mrejesho wa shirika la Thamini Uhai, leo jijini Dar-es-Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...