WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa mikoa 11 inayolima pamba nchini wahakikishe wanasimamia vizuri  wakulima wa zao hilo ili kuongeza uzalishaji na kuwaletea tija wananchi. Agizo hilo limetolewa leo (Jumanne, Septemba 26, 2017) na  Waziri Mkuu wakati akizungumza na wakuu hao wa mikoa kwenye kikao alichokitiisha mjini Dar es Salaam kujadili maendeleo ya zao hilo.

Kikao hicho ni muendelezo wa kikao alichokitiisha mjini Dodoma  (Ijumaa, Septemba 8, 2017) kujadili mbinu za kufufua zao hilo.

Wakuu wa mikoa walioitwa kwenye kikao hicho ni kutoka mikoa ya Shinyanga, Singida, Kagera, Tabora, Morogoro, Mara, Mwanza, Simiyu, Katavi, Kigoma na Geita. Waziri Mkuu amesema katika kipindi hiki ambacho msimu wa maandalizi ya kilimo cha pamba umeanza ni vema kwa Maofisa Kilimo na Wagani wakawasimamia wakulima kwa ukaribu ili wahakikishe wanafuata mbinu bora za kilimo.

Amesema iwapo wakulima watapata usimamizi mzuri kutoka kwa Maofisa Ugani waliopo kwenye maeneo yao kuanzia hatua za awali za utayarishaji wa mashamba yao itawasaidia katika kuongeza  tija, kwenye uzalishaji wao.

“Serikali inawataka Maofisa Kilimo na Wagani wawasimamie wakulima kuanzia maandalizi ya shamba, kupanda, matumizi ya pembejeo na dawa, kuvuna na kutafuta masoko ili kilimo cha zao hilo kiweze kuwaongezea tija.”

Amesema Maafisa Kilimo wote walioko kwenye kila Halmashauri ni lazima wahusike kikamilifu katika kuwaelekeza wakulima namna ya kutumia mbinu bora za kilimo ili waweze kupata mazao mengi , hivyo kujikwamua kiuchumi. Pia Waziri Mkuu amewaagiza Wakuu wa Vyuo vya Kilimo nchini wahakikisha wanakuwa na mashamba darasa yatakayotumika na wakulima na wanafunzi wao kujifunza mbinu bora za kilimo kwa vitendo.

 Kikao hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba; Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI; Bw. Suleiman Jafo, Makatibu Wakuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Kilimo, Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Dkt. Tito Haule na Mkurugenzi Uhamasishaji Mazao, Bw. Twahir Nzallawahe.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Wakuu wa Mikoa inayolima zao Pamba kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu jijini Dar es salaam Septemba 26, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...