Na Tiganya Vincent, RS-Tabora

SERIKALI ya Mkoa wa Tabora imetoa wito kwa viongozi wa dini mbalimbali mkoani hapa kutumia nafasi zao katika kusaidia mapambano dhidi ya kilimo na matumizi dawa za kulevya aina ya bangi katika jamii. Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati akifungua mkutano wa siku tatu wa Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi Watendaji, Wakuu wa Idara na viongozi wa dini mkoani hapa.

Alisema kuwa vitendo vingine vya uhalifu katika jamii vinasababishwa na matumizi ya dawa za kulevya kama vile bangi ambazo zinawapelekea baadhi ya vijana kuchukua maamuzi mwngine ya kujichukulia sheria mikononi. Mwanri alisema kuwa pamoja na kuwa Serikali ya Mkoa wa Tabora kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi imekuwa ikiendesha zoezi la kufyeka mashamba ya bangi katika mapori mbalimbali bado viongozi wa kiroho wanayo nafasi ya kuwaelimisha Waumini wao kuepuka matumizi na kilimo cha zao hilo haramu ili kuhakikisha vijana wanakuwa katika maadili mazuri na sio yale ya kuelekezwa na bangi.

Alisema kuwa matumzi ya bangi yamesababisha baadhi ya vijana kukosa hata heshima hata kuwa tayari kupambana na wazee au watu wanaowazidi umri bila kuzingatia kuwa kufanya hivi ni kinyume na utamaduni mwa Mtanzania ambao unawataka vijana kuwa heshimu watu wazima. Mwanri aliongeza kuwa vitendo vya matumizi ya bangi viachwa vikaendelea na hatimaye vikajipenyeza hadi mashuleni upo uwezekano wa kuharibu na wanafunzi na kusababisha vurugu.

“Tunawaomba sana viongozi wetu wa kiroho mtusaidie kuhusu suala la bangi…utamkuta kijana ameshavuta na kuanza kusema bangi ni bangue …bangi nipe nguvu nikapigane na fulani…jambo linaonyesha kuwa bangi umsababisha kijana kupenda kutafura shari” alisisitiza Mkuu huyo Mkoa.

Akitoa mada kuhusu hali ya ulinzi na usalama kwa kipindi cha Januari hadi Septemba mwaka huu , Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora Wilbroad Mtafungwa alisema kuwa katika kipindi hicho kumekuwepo na matukio 167 ya watu kupatikana na dawa za kulevya aina ya bangi.

Alisema kuwa jeshi la Polisi mwaka huu limefanikiwa kukamata dawa nyingi za kulevya ikiwemo bangi kutokana na misako kuongezeka na kufanikiwa kuwakata watuhumiwa na kugundua maeneo ambao wamekuwa wakilimia bangi katika mapori mbalimbali. Aidha Kamando hiyo wa Mkuu wa Tabora alitoa wito kwa viongozi wa kiroho kusaidia kutoa elimu juu ya kuepuka imani ya kishirikina ambazo ndizo zimekuwa zikisababisha mauaji wa wazee na walemavu.

Kwa upande wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Askofu Mkuu Mihayo Tabora (AMUCTA) Padre Dkt. Juvenalis Asantemungu alisema anakusudia kutunga kitabu kitakachohusu maadili kwa ajili ya kuelimisha jamii ya wakazi wa Tabora na maeneo mengine ili kuzingatia maadili na kuepukana na vitendo vya kuwachoma wazee kwa imani za kishirikina. Alisema kuwa mtu anayezingatia maadili hawezi kutenda uovu huo wa kukatisha maisha ya wazee kwa sababu ya kuona kuwa wamekuwa na macho mekundu kutokana na mazingira wanayoishi.

Mkutano huo wa siku tatu ambao mada mbalimbali zinajadiliwa na ulioandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora umewahusisha Wakuu wa Wilaya zote, Wakurugenzi Wote , Wakuu wa Idara zote , Taasisi za Umma zote na viongozi wa dini kwa lengo la kumbushana majukumu ya kila mmoja ili kuboresha huduma kwa wananchi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...