Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto, Dkt. Godwin Mollel akizungumza katika mkutano wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Ugonjwa wa Himofilia ambayo hufanyika Aprili 17 kila mwaka. Siku hiyo imeadhimishwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)
Baadhi ya wagonjwa wa Himofilia na Selimundu wakiwa kwenye maadhimisho ya siku ya Ugonjwa wa Himofilia duniani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru akieleza umuhimu wa huduma ya afya kwa wagonjwa wa Himofilia.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Stella Rwezaura akiwasilisha mada kwa wagonjwa wa himofilia wakiwamo watoto.
Edson mwenye Himofilia akimlisha keki Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Mollel. Leo ni siku ya kuzaliwa kwa Edson ambaye amesherekea siku hiyo na watoto wenzake pamoja na wazazi.

SERIKALI imewataka wataalamu wa afya katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kutoa elimu ya magonjwa ya damu nchini ikiwemo Himofilia ili wenye ugonjwa huo waweze kugunduliwa na kupelekwa mapema hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Wototo, Dkt. Godwin Mollel wakati wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Ugonjwa wa Himofilia ambayo hufanyika Aprili 17 kila mwaka lengo ikiwa ni kuwaleta pamoja watu wenye matatizo ya Himofilia duniani.

Dkt. Mollel amesema wananchi wakipatiwa elimu ya ugonjwa huo itawasaidia kupunguza madhara na vifo vitokanavyo na magonjwa yasioambukiza ikiwemo Himofilia na Selimundu.

Naibu Waziri alimuagiza Mratibu wa Mradi wa ‘Kuongeza Kasi ya Upatikanaji wa Huduma kwa Watu Wenye Magonjwa ya Damu,’ kwenda katika hospitali za rufaa, kanda na wilaya ili kutoa elimu ya ugonjwa huo ambayo itawasaidia watu wenye Himofilia kufika hospitali mapema.

“Dkt. Stella hakikisha unakwenda katika hospitali za kanda kutoa elimu hii, nafikiri itakuwa njia rahisi kuwafikia wataalamu wengi wa afya nchini,” amesema Dkt. Mollel

Amesema maisha ya watu wenye tatizo la Himofilia yanahitaji uangalizi mkubwa ili kuzuia uvujaji damu, ulemavu na vifo, hivyo hulazimika kupimwa ili kubaini aina ya Himofilia inayo msumbua mgonjwa na kupata matibabu ya kuchomwa factor (chembechembe za protini zilizokosekana mwilini) ili kusaidia kugandisha damu.

“Kama tunavyofahamu, Himofilia ni ugonjwa wa damu kukosa uwezo wa kuganda ambao unasababishwa na   ukosefu wa kiwango cha kutosha cha chembechembe za protini zinazotakiwa kugandisha damu, hivyo husababisha damu kuvuja muda mrefu baada ya mgonjwa kupata jeraha na kuhatarisha maisha,’’ amesema Dkt. Mollel.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Mollel alishiriki kwenye maandamo ya kuadhimisha siku ya ugonjwa wa Himofilia duniani na alizindua dawa mpya ya Emicizumab ambapo Waziri alishuhudia mmoja wa wagonjwa wenye Himofilia akichomwa sindano Emicizumab.

Pia, Waziri alizindua gari la mradi wa ‘Kuongeza Kasi ya Upatikanaji wa Huduma kwa Watu wenye Magonjwa ya Damu.’

Naye Mkurugezi Mtendaji wa Hospitalli ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru amesema mwaka jana Tanzania ilikuwa ni miongoni mwa nchi 10 barani Afrika zilizochaguliwa kupewa msaada wa dawa mpya ya Emicizumab kwa ajili ya wagonjwa wa Himofilia

“Mhe. Waziri, ninafurahi kukwambia kuwa Tanzania tumekuwa nchi ya nne barani Afrika kupokea msaada wa dawa hizi na kuanza kuitumia rasmi ambapo kwa Afrika Mashariki, Tanzania inakuwa nchi ya pili baada ya Kenya na nyingine zilizopokea dawa hizi barani Afrika ni pamoja na Zambia na Cameroon”.

“Dawa hizi ni ghali sana hivyo kwa kuwa mradi huu ni wa miaka mitatu tunaomba Serikali ione namna ambavyo itaendeleza huduma hii iweze kuwa endelevu baada ya mradi kuisha muda wake,” amesema Prof. Museru.

Mmoja wa wanachama wa chama cha watu wenye magonjwa ya Himofilia, Bi. Regina Shirima aliitaka jamii hasa kinababa kushirikiana na kinamama katika kuwapeleka hospitali watoto wenye himofilia kwani baadhi ya kina baba wamekuwa wakiwakimbia wake zao baada ya kubaini mmoja ya watoto ana tatizo la Himofilia.

“Tunawashukuru wataalamu wa MNH akiwamo Dkt. Stella, tunawapigia simu usiku mara mtoto anapovuja damu,” amesema Bi. Shirima.

Hospitali ya Taifa Muhimbili ikishirikiana na wadau wa afya Novo Nordisk Foundation (NNF) na Novo Nordisk Hemophilia Foundation (NNHF), ilianzisha mradi huu ili kuongeza kasi ya upatikanaji huduma kwa watu wenye magonjwa ya damu unaotekelezwa kwa pamoja kati ya Tanzania na Kenya.

Takwimu za kidunia zinaonyesha mtu mmoja kati ya watu 10,000 ana tatizo la Himofilia. Mpaka sasa Tanzania inakadiriwa kuwa na watu takribani milioni 56 mpaka 60 hivyo inaweza kuwa na wagonjwa wapatao 6,000 hadi 12,000.  Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 97 ya watu wenye ugonjwa huu duniani bado hawajagundulika ambapo kwa upande wa Tanzania waliotambulika na wanaendelea na matibabu ni 167 tu.





 Maelezo ya jumla ya Picha,  Viongozi waandamizi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ, Viongozi waandamizi wa Serikali, na Wananchi mbalimbali waliohudhuria Hafla hiyo.







RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kwamba mwezi mtukufu wa Ramadhani ni mwezi wa kuhurumiana ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wanyonge wakiwemo wajane na yatima.

Alhaj Dk Mwinyi aliyasema hayo jana wakati alipokuwa akiwasalimia Waumini wa dini ya Kiislamu huko katika Masjid Tawba maarufu Jongeyani uliopo Malindi kwa Tausi, Wilaya ya Mjini,  Mkoa wa Mjini Magharibi mara baada ya kumaliza Sala ya Ijumaa.

Katika salamu zake hizo, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kwamba kila mmoja kwa nafasi yake ni vyema akaona haja ya kuyasaidia makundi hayo katika jamii ili na wao waweze kuitekeleza ibada ya funga ya Ramadhani ipasavyo.

Pia, Alhaj Dk. Mwinyi alitoa wito kwa wafanyabiashara wote kwamba mwezi mtukufu wa Ramadhani ni mwezi wa kuhurumiana hivyo, mfanyabiashara anatakiwa kupata faida ya kiasi na sio kupata faida mara mbili kwani hilo si jambo la busara.

Kutokana na hilo, Rais Dk. Mwinyi aliitaka Taasisi za Serikali zenye kushughulika na kuhakikisha kwamba bei elekezi zinafuatwa wafanye wajibu wao kuzuia wimbi la wafanyabiashara kupandisha bei mara kadhaa katika kipindi hichi cha mwezi wa Ramadhani.

Na Abdullatif Yunus Michuzi TV.

Ili kuendelea kuvutia Wawekezaji Mkoani Kagera na kuufanya Mkoa huo kuwa mahala sahihi na Salama kwa wawekezaji, Kituo Cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Kimetembelea Kiwanda cha Kuchakata minofu ya Samaki aina ya Sangara cha Supreme Perch kilichopo Bukoba Manispaa eneo la Nyamkazi, ili kubaini shughuli za uendeshaji wa Kiwanda hicho.

Bi. Pendo Gondwe Mwakilishi wa TIC Kanda ya Ziwa akiambatana na wataalam wengine wamefika Kiwandani hapo mapema Februari 16 Mwaka huu na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Kiwanda Hicho, kinachosimamiwa na Mwekezaji kutoka India, kabla ya kupata nafasi ya Kutembelea  na kukagua kiwanda hicho.

Meneja wa Kiwanda  Bwana Manoj Manohoran katika Mazungumzo hayo hakusita kuwasilisha changamoto zinazowakabili Kama Wawekezaji ikiwa ni pamoja na mifumo ya Kodi na Ushuru amabayo wamedai kutokuwa rafiki, Usumbufu wa Barabarani wakati wa kusafirisha samaki kilio kikubwa ikiwa ni kufunguliwa Mara kwa Mara mzigo wao na kupelekea kupoteza ubora, Ukosefu wa malighafi ya kutosha  ambapo kwa sasa uzalishaji ni kidogo sana kwa kile kinachoelezwa kuwa Samaki  aina ya Sangara wamepungua Ziwani na mengine mengi.

Mara baada ya kutembelea Kiwanda hicho Bi. Pendo amepongeza na kushukuru Uongozi wa Kiwanda hicho kwa namna kilivyojizatiti kwa Miundo mbinu katika kuhakikisha kinazalisha bidhaa bora zinazotokana na samaki, na kuongeza kuwa changamoto zote zilizobainishwa, wao kama Washauri katika masuala ya Uwekezaji wanazibeba na watazifikisha katika mamlaka zinazohusika ili zitatuliwe na kuendelea kutengeneza Mazingira mazuri ya mwekezaji huyo kunufaika na uwekezaji wake.

Licha ya changamoto zilizobainishwa na Mwekezaji huyo, Kiwanda Cha Kuchakata minofu ya Samaki cha Supreme Perch kimekuwa kikitengeneza mpaka Bilioni 30 kwa Mwaka kupitia mauzo yao huku Soko la minofu hiyo likiwa Hispania, Italia na Uholanzi, mbali na kutoa ajira kwa Watanzania pia Kiwanda kimekuwa na mchango mkubwa kwa Jamii inayokizunguka kwa kuchangia Shughuli za kimaendeleo ikiwemo Ujenzi wa Visima vya Maji, Shule na wakati mwingine kuwezesha Kliniki inayombetea kwa Wakazi wa Visiwani.


Bi Pendo Gondwe kutoka Kituo Cha Uwezekezaji Tanzania (TIC) akifanya Mazungumzo na Uongozi wa Kiwanda cha Supreme Perch baada ya kuwasili Kiwandani hapo.
Meneja wa Kiwanda Bwana Manoj Manohoran  akiwasilisha changamoto za Kiwanda cha Supreme Perch kwa wawakilishi wa TIC wakati wa Mazungumzo yaliyofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Kiwanda hicho.
Eneo mojawapo la mitambo ndani ya Kiwanda ambapo Samaki hupitishwa katika hatua mbalimbali wakati wa uchakataji wa minofu.
Muonekano wa Kifungashio cha Minofu ya Samaki aina ya Sangara inayozalishwa na Kiwanda cha Supreme Perch Bukoba Manispaa.

Maboksi Yenye minofu ya Samaki yakiwa yamefungashwa katika chumba maalum cha kuhifadhia bidhaa hiyo,  tayari kusafirishwa kwenda Sokoni.
Bi. Pendo Gondwe akifurahia pamoja na wenzake Muonekano wa kifungashio cha Minofu ya Samaki cha Supreme Perch.
 Muonekano wa Jengo mojawapo la Kiwanda cha Supreme Perch kilichopo Bukoba Manispaa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akitazama fomu za madai ya malimbikizo ya mishahara ya Watumishi wa Umma, mara baada ya kuitembelea Idara ya Usimamizi wa Rasilimali watu Serikalini inayoshughulika na madai hayo. Kushoto ni Katibu Mkuu-UTUMISHI Dkt. Laurean Ndumbaro akishuhudia.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na watumishi wa ofisi yake waliopo UDOM mara baada ya kuwatembelea kwa lengo la kuhimiza Uwajibikaji. Kulia kwake ni Katibu Mkuu-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akisalimiana na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu, Bw. Elisante Mbwilo (wa kwanza kushoto) mara baada ya kuwasili katika Ofisi yake iliyopo UDOM kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji. Kushoto kwake ni Katibu Mkuu-UTUMISHI Dkt. Laurean Ndumbaro.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akielekea Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu ili kuona na kuhimiza utekelezaji wa majukumu ya Idara hiyo. Katikati ni Katibu Mkuu-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro.

 

………………………………………………………………………………………..

Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa ameielekeza Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu ya Ofisi yake kuhakikisha inawatafutia Watumishi wa Umma na Viongozi nafasi za mafunzo ya kuongeza maarifa na utaalamu ndani na nje ya nchi ili kuwajengea uwezo kiutendaji.

Mhe. Mchengerwa ametoa maelekezo hayo, alipoitembelea Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu yenye jukumu la kuandaa sera, miongozo na mifumo ya Usimamizi wa maendeleo ya rasilimaliwatu katika Taasisi za Umma ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mhe. Mchengerwa amesema, Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuwapatia mafunzo ya kutosha Watumishi wa Umma na Viongozi katika Taasisi za Umma ikiwa ni pamoja na Wakuu wa Mikoa na Wilaya ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Ili kuunga mkono azma hiyo ya Mhe. Rais, amesisitiza kuwa Ofisi yake kupitia Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu itahakikisha Watumishi wa Umma nchini wanapata mafunzo yatakayowajengea morali na hali ya kutoa huduma bora kwa wananchi. 

Waziri Mchengerwa ameitaka Idara hiyo kuongeza jitihada za kutafuta Taasisi za Kitaifa na Kimataifa ambazo ziko tayari kutoa ufadhili wa mafunzo kwa Watumishi na Viongozi wa Taasisi za Umma na kuwasilisha fursa zilizopatikana kwa Katibu Mkuu-UTUMISHI ili aone namna bora ya kuzitoa kwa walengwa kwa kuzingatia mahitaji ya Utumishi wa Umma na vipaumbele vya Serikali.

Aidha, amewataka Watumishi na Viongozi watakaopata fursa ya mafunzo kuwajengea uwezo Watumishi na Viongozi wengine ambao hawajabahatika kupata fursa ya mafunzo ili nao waweze kuboresha utendaji kazi wao.

Akipokea maelekezo ya Mhe. Mchengerwa, Kaimu Mkuu wa Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu Bw. Elisante Mbwilo amesema Idara yake itaendelea kutafuta fursa za mafunzo kwa wadau wa ndani na nje ya nchi ili Watumishi na Viongozi wanufaike na fursa zitakazopatikana kwa lengo la kuboresha utendaji kazi.

Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inatekeleza jukumu la kuwajengea uwezo Watumishi wa Umma kwa kuzingatia Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2009 Kifungu G.1 (Kifungu kidogo cha 7, 9, 10 &11), Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya Mwaka 2008 Kifungu cha 4.8 na Sera ya Mafunzo katika Utumishi wa Umma ya Mwaka 2013.