Baadhi ya watumishi wanaofanya kazi katika Kamisheni ya Umoja wa Afrika AU iliyopo jijini Addis Ababa Ethiopia wakimsikiliza kwa Makini Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Rais Jakaya Mrisho Kikwete alipokuwa anaongea nao leo asubuhi katika Makao makuu ya umoja huo
JIEPUSHENI NA AJIRA ZA UPENDELEO - JK
Na Salva Rweyemamu, Addis Ababa
Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Jakaya Kikwete leo ameuelezea uongozi mpya wa Kamisheni ya AU majukumu yake, ikiwa ni pamoja na kuepukana na kishawishi cha makamishna hao kuajiri ndugu zao katika Umoja huo.
Akizungumza na makamishna wapya ambao walichukua madaraka ya kuongoza Kamisheni hiyo jana, Mwenyekiti huyo wa AU amesema kuwa tatizo la ajira za upendeleo ni la muda mrefu katika AU, na hata kabla ya hapo katika OAU (Organisation of African Unity) uliotangulia AU.
“Afrika ni kubwa na ina watu wengi wenye uwezo. Chukueni bongo kali zaidi kutoka miongoni mwa vijana wa Afrika, na siyo kuajiri watu kwa sababu ni ndugu zenu ama jamaa zenu hata kama hawanazo sifa za kuajiriwa katika taasisi muhimu kama hii,” amesema kiongozi huyo wa AU katika mkutano uliofanyika kwenye Makao Makuu ya AU mjini Addis Ababa, Ethiopia.
AU inatakiwa kuwa na wafanyakazi 939 na mpaka sasa imeajiri 634.
JK pia ameutaka uongozi huo mpya chini ya Jean Ping wa Gabon kusimamia vizuri fedha za AU na kuhakikisha kuwa fedha hizo zinatumika ipasavyo. Amesema kuwa raslimali zenyewe za AU ni kidogo na chache na kama zinatumika vibaya, umoja huo utashindwa kutekeleza mipango yake na kujiimarisha kama inavyotakiwa.
“Tujiepushe na matumizi mabaya ya fedha kidogo ambazo tunazipata. Hili nalo limekuwa linazungumzwa kwa chini chini na kwa muda mrefu katika umoja wetu.”
Na ili kuhakikisha kuwa fedha za AU zinatumika vizuri na ipasavyo, JK ameutaka uongozi huo mpya kuhakikisha kuwa mahesabu ya AU yanakaguliwa kila mwaka mwaka, na hata kila mara inapokuwa lazima kufanya hivyo.
Juu ya majukumu mengine ya makamishna hao, JK ametaka juhudi kubwa kufanywa katika kuendelea kuijenga AU.
“Hii ni taasisi changa mno. Ni kweli kuwa viungo vyake vingi vimeundwa na kukamilika, lakini ukweli ni kwamba bado taasisi yenyewe ni changa na hivyo inahitajika juhudi kubwa zaidi kuweza kuiimarisha.”
AU ilianzishwa rasmi Julai 2002 kuchukua nafasi ya OAU. Amewaambia makamishna hao kuwa wao ndiyo bongo za Afrika na kuwa kwa pamoja wanaunda kundi la watu wanaofikiria kwa niaba ya Afrika (think tank), na hivyo lazima watumie uwezo wao katika kulisaidia Bara la Afrika kupiga hatua.
“Nyie ndiyo think tank wa Bara letu. Mmechaguliwa kwa sababu ya uwezo wetu mkubwa na kwa sababu ya nguvu yenu ya kuweza kupanga na kuleta maendeleo ya Bara letu hili. Lisaidieni,” amesema JK.
Amehimiza ufanisi, uadilifu na ushirikiano katika utendaji kazi na kusisitiza, “kama mnavyojua AU ni taasisi ya kisiasa, na kimsingi, siasa ni kazi ya ushirikiano na hivyo lazima mfanye kazi kwa ushirikiano, miongoni mwenu nyie, kati yenu na mwenyekiti wetu, na kati yenu na wafanyakazi wengine wa AU.”
Amewataka kujenga mahusiano mazuri na pia kujiheshimu katika utendaji kazi, akisema kuwa wao ni viongozi na moja ya wajibu wa kiongozi ni kujiheshimu. “Najua hili mnalijua fika, lakini kwa kuwakumbusha tu ni kwamba baada ya kuingia katika shughuli hii, baadhi ya mambo yenu yalikuwa mambo binafsi, sasa yanaweza wazi, hadharani.”
Baada ya kuwa amemaliza kukutana na makamishna, Mwenyekiti huyo wa AU amekutana na wafanyakazi wote wa AU kwenye Ukumbi wa Congo kwenye makao Makuu ya AU.
JK amewataka wafanyakazi hao kuunga mkono uongozi mpya wa Jean Ping kama walivyounga mkono uongozi uliopita wa Alpha Omar Konare wa Mali ambaye jana alikabidhi uongozi kwa Ping.
Amewashukuru wafanyakazi hao kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya katika kuijenga AU na kusisitiza kuwa mafanikio yote ambayo yamepatikana mpaka sasa yametokana na bidii, juhudi na jasho lao.
“Tusingeweza kuwa tumepata mafaniko tuliyopakata mpaka sasa, yaani tokea Julai 2002 tulipoanza hadi sasa. Mmefanya kazi nzuri kama watumishi wa kimataifa ndani ya Bara lenu wenyewe. Tafadhali endeleeni na moyo huo wa kuijenga Afrika.”
Akiwahimiza kuongeza bidii, JK amemalizia kwa kuwatolea kauli mbinu maarufu ambayo aliianzisha kwenye Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania wakati akiwa waziri wa wizara hiyo ya “Better than yesterday, less than tomorrow.”

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 5 mpaka sasa

  1. HUYU JK KILA AKIONGEA UTADHANI SI YULE TUNAYEMFAHAMU HADA BONGO. YEYE AMEAJIRI KWA KUPENDELEA AKAJAZA WANAMTANDAO RAFIKI ZAKE KIBAO KWENYE NAFASI ZOTE, SASA ANACHOWAAMBIA HUKO "AU" NI NINI?? HIVI HAJUI KUWA WATU WANASOMA NA WANAMFAHAMU VILIVYO?? AACHE KUWADANGANYA WATU AFANYE KAZI KWA VITENDO. ANANNIKERA SANA!!!!!!!!!!!!!!!!!

    ReplyDelete
  2. Yaani kweli siamini kuwa raisi anakemea kupeana madaraka kwa kujuana. Labda anataka kubadilisha hili Tanzania. Akifanya hivyo basi nchi itaendelea!! Kwa vile katoa kauli hiyo, basi wananchi tukiona watu wanamependelewa na hawana ujuzi, basi tukemee kwa nguvu zote hilo. Maana unakuta familia moja ina waziri, PS, balozi etc!! Yaani hakuna watanzania wengine ambao wako competent? Au kama nilivyosoma kwenye vyombo vya habari kuwa watoto wa vigogo ndiyo wamejaa BOT na other important government institutions.

    ReplyDelete
  3. AnonymousMay 01, 2008

    Please JK Practise what you preach and stop blabla blabla.........Is you country do exactly what you said? Please be Honest


    POPO

    ReplyDelete
  4. HII MIJITU/WATU INAYOTAKA ROMA/TANZANIA IJENGWE SIKU MOJA SIJUI INAWAZA NINI

    ReplyDelete
  5. AnonymousMay 02, 2008

    Bwana Rais, 'Charity begins at home'If you mean what you say, please practice the same in your beloved country manake in Tanzania that is actualy in the last stage of cancer; i.e ajira za kujuana zimezidi. Tusihubiri injili kwa wenzetu wakati sisi tunaelekea motoni. "Toa boriti katika jicho lako kabla hujaona kibanzi kwenye jicho la mwenzako" Isn't it??

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...