JK akihutubi Mkutano wa awali kujadili zahama ya mfumo wa fedha duniani na jinsi ya kugharimia maendeleo duniani leo jijini Doha, Qatar
JK akihutubia mkutano wa awali kujadili zahama ya mfumo wa fedha duniani na jinsi ya kugharimia maendeleo duniani jijini Doha, Qatar, leo

JK akiteta na Mkurugenzi Mkuu wa World Trade Organisation WTO Director General Pascal Lamy jijini Doha, Qatar wakati wa mkutano wa awali kujadili zahama ya mfumo wa fedha duniani na jinsi ya kugharimia maendeleo duniani
JK akiongea na katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban-Ki moon wakiwa katika mkutano wa awali kujadili zahama ya mfumo wa fedha duniani na jinsi ya kugharimia maendeleo duniani huko Doha
JK wakibadilishana mawazo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban-Ki moon na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa Balozi Augustine Mahiga huko jijini Doha leo
JK akisalimiana na Rais wa Sudan Omar al Bashir katika mkutano wa awali kujadili zahama ya mfumo wa fedha duniani na jinsi ya kugharimia maendeleo duniani

Na Mwandishi Maalum,

Doha, Qatar
Mkutano wa awali kujadili zahama ya mfumo wa fedha duniani na jinsi ya kugharimia maendeleo duniani, umekubaliana kuwa matatizo ya sasa ya mfumo wa fedha duniani ni dhahiri yataziathiri nchi zote duniani, tajiri na masikini na kuzidisha umasikini.

Mkutano huo pia umekubaliana kuwa ufumbuzi wa matatizo ya sasa katika mfumo wa fedha duniani ni lazima yatafutwe kwa pamoja na nchi zote kwa sababu hilo siyo jambo linaloweza kuachwa mikononi mwa nchi chache tu, hata kama zina uwezo kiasi gani.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete ambaye amehudhuria mkutano huo leo, Ijumaa, Novemba 28, 2008 mjini Doha, Qatar amesema kuwa mkutano huo umekubaliana kuwa katika hili nchi zote duniani lazima ziogelee kwa pamoja katika bahari ya matatizo hayo.

“Tumekubaliana kuwa lazima tuogelee pamoja kwa sababu kuzama kwa kila mmoja wetu siyo ni jambo lisilokubalika,” Rais Kikwete amesema baada ya kikao hicho kilichoitishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki Moon.

Kikao hicho kimehudhuriwa na wakuu wa mataifa 20 yenye nguvu kubwa zaidi za kiuchumi duniani, taasisi za kimataifa za fedha pamoja na nchi chache zinazoendelea ikiwamo Tanzania.

Taasisi hizo ni Shirika la Fedha Duniani (IMF), Benki ya Dunia (WB) na nchi zinazoendelea ni Tanzania, Misri, Nigeria, Antigua, Norway, Kazakhistan, Philippines na Pakistan.

Rais Kikwete ambaye ameingia ukumbini kuhudhuria kikao hicho muda mfupi baada ya kuwa amewasili hapa jioni ya leo ameiwakilisha Tanzania na Afrika katika mkutano huo.

Mkutano wa leo ulikuwa wa utangulizi kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Kimataifa Kujadili Jinsi ya Kugharimia Maendeleo Duniani na Jinsi ya Kukabiliana na Zahama za Sasa za Mfumo wa Fedha Duniani unaoanza kesho, Jumamosi, Novemba 29, 2008, kwenye ukumbi wa
Salwa.

Rais Kikwete amesema kuwa wakuu wa nchi katika mkutano huo pia wamekubaliana kuwa matatizo ya sasa ya mfumo wa fedha duniani yasitumike kupunguza utashi wa kisiasa duniani katika kupambana na athari za uchafuzi wa mazingira duniani na jitihada za kupambana na umasikini.

“Tumekubaliana vile vile kuwa pamoja na kwamba duniani inakabiliwa na zahama kubwa ya kiuchumi kutokana na kuvurugika kwa mfumo wa fedha duniani, bado hakuna taasisi ya kupambana na hali hiyo,” amesema Rais Kikwete.

Ameongeza kuwa utafiti unaonyesha pia kuwa matatizo ya sasa ya mfumo wa fedha duniani yataathiri na kurudisha nyuma jitihada za kufanikisha Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDG’s) kwa kiasi cha miaka saba. Malengo hayo yamepangwa kufikiwa mwaka 2015.

“Matatizo haya yatasababisha ukosefu mkubwa wa ajira. Yatawatumbukiza mamilioni ya watu, hasa katika nchi masikini zaidi duniani, katika umasikini mkubwa zaidi,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Tusipokuwa waangalifu, matatizo haya yatasababisha zahama kubwa mno ya kibinadamu. Tunaweza kushuhudia watu wanarudi kwenye matatizo ya kichumi ya miaka ya 1930, wakati baadhi ya Wamarekani walipolazimika kuishi katika nyumba za maboksi.”

Ameongeza: “Ni dhahiri kuwa lengo la kupunguza umasikini duniani kwa nusu ifikapo mwaka 2015 kama MDG’s zinavyolenga litakuwa gumu mno kufikiwa kwa kutilia maanani matatizo ya bei za vyakula, bei za mafuta na matatizo ya mfumo wa fedha duniani. Yote haya, yanaongeza umasikini.”

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. JK the true statesman,naam kweli kaipandisha taifa letu kihadhi na heshima ambayo nchi yangu inastahili...continue with your voyages!!!

    ReplyDelete
  2. Huyu shujaa anampango gani kuhusu DRC? Nilidhani ataungana na mashujaa wenzake wakamafanyizie Nkunda. Wakuu kuna mtu anajua hili?

    ReplyDelete
  3. mpaka 2010 umemaliza dunia nzima

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...